KOCHA Marcio Maximo ametetea uamuzi wake wa kumpumzisha kiungo Athuman Iddi ‘Chuji’ na kumchezesha chipukizi Kigi Makassi wakati Stars ilipotoka sare ya bao 1-1 na Malawi katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyofanyika Jumapili kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa.
Chuji, ambaye alifunga bao la kusawazisha wakati Stars ilipolazimisha sare ya bao 1-1 na kuiondoa Uganda mjini Kampala takriban wiki mbili zilizopita, aling’ara katika kipindi cha kwanza akiongoza mashambulizi ya Stars kwa kugawa mipira kwa washambuliaji.
Lakini, Maximo alimtoa kiungo huyo wa kimataifa wa Yanga wakati wa mapumziko na sehemu ya kiungo kuonekana kupwaya hasa kutokana na kiungo mwingine, Nizar Khalfan kuonekana kutofanya vizuri kazi ya kupokonya mipira na Stars kujikuta ikiruhusu bao mwanzoni mwa kipindi cha pili, bao lililotokana na shambulizi la kushtukiza.
“Iddi hakuwa amecheza vibaya hata kidogo,” alisema kocha huyo Mbrazili baada ya mechi. “Kipindi cha kwanza tulikuwa tumetumia sana wingi ya kulia kupeleka mashambulizi na kwa kuwa tulikuwa tumeshamiliki sehemu ya kiungo, niliona nipanue zaidi uwanja.
“Niliona ni vizuri nitumie na wingi ya kulia hasa kwa kuwa uchezaji wa Iddi ni kama ule wa Nizar na ndio maana uliona kipindi cha pili tulishambulia kwa kutumia wingi zote.”
Maximo, ambaye alifurahishwa na jinsi mashabiki walivyoishangilia timu hata iliporuhusu bao la kuongoza, alisema Kigi, mmoja wa wachezaji wanne ambao kocha huyo amekuwa akiwajumuisha kwenye kikosi chake kwa nia ya kuwapa uzoefu tangu mwaka jana, alicheza vizuri na amepata uzoefu mzuri.
“Mechi hii ilikuwa ngumu kwetu, lakini ilikuwa ni jaribio zuri kwa ajili ya mechi ijayo,” alisema. “Tumekutana na timu ambayo ilicheza kwa kujihami na kushambulia kwa kushtukiza.
Sikuwa naijua mchezo wake ndio maana nilijaza wachezaji wengi kwenye kiungo kabla ya kuanza kushambulia,” aliongeza Maximo, ambaye alimchezesha Chuji, Nizar, Iddi na Godfrey Boniface ‘Bonny’, ambaye alimudu sana sehemu ya kiungo wa chini, akituliza vizuri mchezo kila alipopokonya mpira wakati Stars ikishambulia.
“Ni vizuri kwamba tumecheza mechi ambayo tumejaribisha fomesheni tofauti na mikakati tofauti dhidi ya timu mmoja. Hiki ni kitu kizuri kinachoongeza uzoefu kwenye timu hii.
Kuhusu Emmanuel Gabriel, ambaye alionekana kutocheza kwa kiwango chake kutokana na kuwa majeruhi, Maximo alisema: “Tulimuuliza daktari na akatuambia kuwa Gabriel yuko fiti kucheza na ndio maana tulimpanga. Alicheza vizuri.”
Kwa upande wake, kocha wa Malawi, Kinnah Phiri aliisifu Stars akisema kuwa imedhihirisha ubabe wake kwa timu yake baada ya kushinda kwa mabao 2-1 wakati timu hizo zilipokutana kwenye Kombe la Chalenji mjini Addis Ababa, Ethiopia mwaka jana.
“Hii ni timu nzuri sana,” alisema kiungo huyo wa zamani wa Malawi ambaye alikanusha kwamba timu yake ilikuwa ikitafuta sare tu, licha ya wachezaji wake kuonekana wakipoteza wakati mwingi hata wakati timu zilikuwa hazijafungana.
“Hii ni timu nzuri. Kitu pekee inachohitaji ni kuungwa mkono na mashabiki.”
Comments
Loading…