*Arsenal, Chelsea wajipanga kwa kumbo
*Real wawataka Kroos, Ramires, Suarez
Mshambuliaji wa Bayern Munich, Mario Mandzukic amethibitisha kwamba anaondoka klabuni hapo msimu huu.
Mandzukic amesema tayari amekutana Mwenyekiti wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge kujadili hatima yake na amemweleza kwamba hatabaki Ujerumani kwa msimu ujao.
Mandzukic, raia wa Croatia anayetarajiwa kujiunga na klabu ya Ligi Kuu England, anasema alifurahia muda aliokaa Ujerumani, hakutarajia angeondoka wakati huu, lakini amebaini muda umewadia.
Anasema kwamba hawezi kucheza kwa kiwango chake cha juu katika mfumo wa kocha Pep Guardiola hata ajitahidi kiasi gani, hivyo anataka kuondoka.
Guardiola anawapelekesha na mtindo wake wa tiki-taka aliokuwa akiutumia Barcelona na amepata kuchagizwa na wakongwe wa Bayern kwamba anaharibu soka yao.
Kutamka kwake kwamba anaondoka kunajenga hisia kwamba huenda Arsenal na Chelsea wanaotafuta washambuliaji wakamuwania, ambapo alifunga mabao 18 katika mechi 30 alizochezea mabingwa hao wa Ujerumani.
Mandzukic atafaa sana kwa soka ya kasi ya England na pia kiwango chake cha mshahara ni cha kawaida tu kwa Arsenal au Chelsea, ikitegemea watakaompata.
Ameshaingia Brazil na timu yake ya taifa, ambako anatarajiwa kuonesha uwezo wake chini ya kocha
Niko Kovac aliyesema majuzi kwamba Mandzukic atawahama Bayern na alitaka suluhu yake ipatikane kabla ya mechi kuanza Brazil.
Mandzukic angeweka ushindani unaotakiwa Arsenal kwa Olivier Giroud anayeonekana ‘mfalme’ tangu awasili Emirates.
Chelsea nao wana shida ya mpachika mabao licha ya kumsajili Fernando Torres kwa dau kubwa kutoka Liverpool ambalo halikulipa. Demba Ba na Samuel Eto’o nao wameshindwa kusaidia tatizo, hivyo Mandzukic atakuwa safi sana Stamford Bridge akicheza kama mshambuliaji pekee mbele.
REAL MADRID YATAJA WATATU INAOWATAKA
Mabingwa wa Ulaya na Kombe la Mfalme Hispania, Real Madrid wametangaza nyota watatu watakaotoa kipaumbele ili wawasajili kwa msimu ujao.
Wababe hao wanafundishwa na Carlo Ancelotti wanataka kuwasajili Luis Suarez wa Liverpool, Toni Kroos wa Bayern Munich na Ramires wa Chelsea.
Licha ya Liverpool kuwabania Arsenal msimu uliopita hata baada ya kutimiza matakwa ya kifungu cha mkataba wake kwa kutoa pauni zaidi ya milioni 40, Real Madrid wamejizatiti kumtwaa.
Hata hivyo, inaelezwa kwamba Kocha wa Chelsea Jose Mourinho atakataa kumuuza Ramires ambaye Ancelotti alipata kumtaka kabla.
Mourinho naye anataka wachezaji kadhaa wa Real, hivyo wakikaa chini wanaweza kuafikiana kubadilishana. Mourinho aliyehamia Chelsea kutoka Real, anawataka wachezaji wake wa zamani, Sami Khedira, Isco na Raphael Varane.
Kroos amekuwa akitakiwa kwa muda mrefu na Manchester United lakini inaelekea hataki kwenda huko na amebakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Bayern.
Real wakimkosa safari hii, watasubiri hadi mwakani wamchukue bure. Real wanamtaka ili asaidiane na Xabi Alonso ambaye ndiye injini ya timu.
Real wakiwapata watatu hao, wawili au hata mmoja watafaidika katika kampeni ya kutaka kunyakua Kombe la La Liga.
Comments
Loading…