*Roberto Mancini wa Manchester City amedai kwamba yeye ndiye kocha bora zaidi England.
Ametoa kauli hiyo wakati pakiwa na tetesi za kusukwa mipango ya kumwondoa ukocha wa mabingwa hao watetezi, mwenyewe akisema hakuna kitu kama hicho.
Watu wamesema kwa miezi sita sasa kwamba Manchester City watabadili kocha, kwamba Guardiola anakuja, baada ya kwenda Bayern Munich sasa kuna mwingine.
“Nimetwaa kombe la Ligi Kuu, Kombe la FA na Ngao ya Jamii, hakuna kocha mwingine aliyeshinda kama mimi kwa miezi 15 iliyopita. Sina cha kufanya lakini huo ndio ukweli,” akasema Mancini.
Pamekuwa na madai kwamba hakuna uelewano kati ya Mancini na wachezaji waandamizi, akiwamo golikipa Joe Hart, jambo linalokanushwa.
Kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa timu dhaifu ya Southampton kiliwaacha City pointi 12 nyuma ya vinara Manchester United.
Zikiwa zimebaki mechi 12 pia Ligi Kuu ya England (EPL) kumalizika, inaonekana ni vigumu City kuwakamata jirani zao hao, kwa kuzingatia kasi waliyo nayo vijana hao wa Alex Ferguson.
Hata hivyo, Mancini anasema bado kuna muda, na kwamba hadi Aprili ndipo uhakika wa mwelekeo utapatikana, hivyo muhimu ni timu yake kuendelea kushinda.
Mancini ameonekana kutiwa moyo na ushindi wa Jumapili dhidi ya Leeds United katika Kombe la FA, na anasema umeifufua timu na utachochea ushindi kwenye mechi zilizobaki.
Mtaliano huyo ana mtihani mgumu Jumapili ijayo, kwani timu yake inakabiliana na Chelsea, timu yenye utata miongoni mwa kocha na wachezaji.
Kocha wa muda, Rafa Benitez, anadaiwa kumwomba Roman Abramovic achukue nafasi hiyo moja kwa moja, lakini hatarajiwi kudumu zaidi ya majira ya kiangazi.
Moja ya matatizo ya Benitez ni kutopendwa na washabiki wa Chelsea, wanaokumbukia uhusiano mbovu aliokuwa nao wakati akiwaongoza Liverpool kwa mafanikio.
Utakuwa mchezo unaokutanisha makocha wanaofikiria hatima yao, wote wakifarijika kwamba Pep Guardiola aliyekuwa Barcelona ameshachukuliwa na Bayern Munich.
Hata hivyo, zipo tetesi kwamba Abramovic anataka kumchukua Manuel Pellegrini wa Malaga – klabu ya La Liga nchini Hispania.
Abramovic wikiendi iliyopita alifunga safari hadi Malaga walipocheza na kuwafunga Atletico Bilbao bao 1-0.
Zipo tetesi pia kwamba matajiri wa City wanataka kumchukua Carlo Ancelotti atakayekuwa huru majira ya kiangazi, ili aiendeshe klabu hiyo kwa mfano wa Barcelona.
Yote hayo hayamnyimi usingizi Mancini, anayesema kwamba ubora wake England ni kwa sababu amefanikiwa klabuni, tofauti na makocha wengine.
Anasema iwapo yeye atafukuzwa, ni wazi makocha wengine wote watakosa kazi katika EPL, maana hawana kiwango bora kama chake.
Mancini alianza kuandamwa timu yake ilipotolewa kwenye michuano ya Ulaya katika hatua ya awali, kisha ilipoanza kusuasua nyuma ya United, ikipoteza au kutoka sare mechi muhimu.
“Katika miezi 15 iliyopita, mimi ndiye kocha bora England,” anasema Mancini aliyechukua hatamu za uongozi wa timu hiyo kutoka kwa Mark Hughes aliyefukuzwa kwa mwenendo mbaya wa timu.
Katika misimu mitatu iliyopita, Mancini amepewa na kutumia pauni milioni 285 kununua wachezaji, lakini pamoja na kutwaa kombe msimu uliopita, washabiki wangependa kuona wanatetea kombe msimu huu, jambo linaloelekea kuwa gumu.
Mkurugenzi wa ufundi wa zamani wa Barcelona, Txiki Begiristain ameajiriwa kama mkurugenzi wa soka, huku kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho akisema wiki iliyopita kwamba atakuja kunoa klabu ya EPL baada ya kuondoka Madrid, ila hakusema ni lini.
Pamekuwa na tetesi pia kwamba Mancini amekuwa akigombana na wachezaji wake, lakini nyingine zinadai amekuwa mkali wanapokosea, na analenga kupangua kikosi mwishoni mwa msimu, akijiamini kwamba atasalia kazini.
Comments
Loading…