*Man United wapaa, Swansea, Reading taabani
*Arsenal wabanwa Southampton, Spurs wapeta
Licha ya Manchester United kuendelea kushinda, kocha Roberto Mancini wa Manchester City anadai msimamo wa ligi hauna maana hadi Februari.
United wameendeleza pengo la pointi saba dhidi ya mahasimu hao jirani, kwa kuwafunga Wigan mabao 4-0, City wakiwalaza Stoke City 3-0.
Vijana wa Alex Ferguson wamefikisha pointi 52 katika michezo 21, lakini Mancini anasema hakuna haja ya kuwa na wasiwasi, kwani mechi bado zipo nyingi.
Hata hivyo, katika mchezo wa mwaka mpya, City walipata pigo kwa mshambuliaji wao tegemeo, Sergio Aguero kuumia msuli wa paja, huku Samir Nasri akiwa amefungiwa mechi tatu kwa utovu wa nidhamu.
Kadhalika wanatarajia kuwapoteza kwa muda wachezaji wake watatu, Yaya Toure, Kolo Toure na Abdul Razak walioitwa Ivory Coast.
Wanakwenda kuchezea timu ya taifa lao kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini Januari 19 hadi Februari 10.
“Si muhimu sana kuangalia msimamo wa ligi sasa, kwa maana si tamati, lakini tunahitaji kutia juhudi na kushinda kabla ya kutupa jicho kwenye msimamo huo baadaye Februari,” anasema Mtaliano huyo.
Ushindani katika nafasi ya tatu, ya nne na ya tano upo kati ya Chelsea, Tottenham Hotspurs na Arsenal.
Spurs wanashika nafasi ya tatu baada ya kuwakung’uta Reading mabao 3-1, Chelsea wakishika nafasi ya nne na Arsenal ya tano, baada ya kutoshana nguvu na Southampton kwa bao 1-0.
Spurs walibanwa na Reading katika muda wa awali wa mchezo, lakini kadiri muda ulivyokwenda, Reading waliachia.
Emmanuel Adebayor, Clint Dempsey na Michael Dawson ndio waliowang’arisha vijana wa Andre Villas-Boas, wakati Reading walipatangulia kufunga kupitia Pavel Pogrebnyak.
Hata hivyo Spurs wamecheza mechi 21, Arsenal mechi 20 na Chelsea mechi 19. Arsenal watajilaumu wenyewe kwa aina ya mchezo walioonesha, kana kwamba gari liliendeshwa huku breki ya mkono imewekwa.
Pamoja na kuchezesha wachezaji nyota walio nao, Arsene Wenger ambaye juzi alidai bado wapo kwenye mbio za ubingwa, alishuhudia wakitangulia kufungwa.
The Walcott alichezeshwa namba tisa anayoililia kwa muda, lakini hakufurukuta hadi mpira wake wa adhabu ndogo ulipoingizwa wavuni na beki wa Southampton, Guly Do Prado.
Huenda Arsenal wangeangukia pua, kama si jitihada na ujuzi wa golikipa wao, Wojciech Szczesny, kwani beki ilikuwa ikikatika, Bacary Sagna akielekea kuachia hatari langoni, na hata wakati mwingine akielekeza mipira huko.
Ni Mfaransa huyo aliyechangia mabao mawili ambayo Arsenal walifungwa na Newcastle katika mechi iliyotangulia, kwa ukabaki wake unaogeuka kufunga tela.
West Bromwich Albion waliendelea kuugulia kipigo, baada ya kuchapwa na Fulham mabao 2-1, huku West Ham United wakizinduka na kuwafunga Norwich mabao 2-1.
Swansea walishindwa kuonesha cheche zake, kwa kubanwa na timu inayoelekea kudoda siku hizi ya Aston Villa.
Kwa matokeo hayo, Wigan wamechukua nafasi ya Southompton kwenye eneo hatari la kushuka daraja, wakiungana na Reading.
Mkiani wapo Queen Park Rangers (QPR) wanaochuana na Chelsea Jumatano hii, huku Liverpool wakiwavaa Sunderland.
Everton wa David Moyes wanakaribishwa kaskazini magharibi mwa nchi, walipo Newcastle wanaochechemea kwa vipigo vya mfululizo chini ya Alan Pardew.
Comments
Loading…