Manchester United wameshutumiwa kwa jinsi walivyomfukuza kazi kocha wao, David Moyes.
Chama cha Makocha wa Ligi (LMA) kimedai kwamba Old Trafford hawakutumia weledi wala uanataaluma katika kushughulikia suala hilo.
Moyes mwenyewe anadaiwa kukasirika baada ya kujulishwa hatima yake tu.
Lakini alichosema hadharani ni kwamba kule kufanya tu kazi United ni sifa kubwa na anamshukuru Kocha Alex Ferguson kwa kumwezesha kufanya kazi hapo hata kwa miezi hiyo kumi tu.
Fergie anadaiwa alishirikishwa katika uamuzi wa kumfukuza, kumbe naye aliona hafai licha ya kumpendekeza kumrithi na sasa atapewa fursa kubwa kwenye uteuzi wa mtu mwingine.
LMA wanadai tatizo ni kwamba kabla ya Moyes kujua kwamba anafukuzwa vyombo vya habari vilishajua kwa kina kabisa kilichokuwa kikiendelea na hata juu ya nani angechukua mikoba yake kwa muda.
United walijidai kudai hakuwa amefukuzwa Jumatatu vyombo vya habari viliporipoti, lakini mchana siku hiyo hiyo, Makamu Mwenyekiti Ed Woodward alimpigia simu Moyes wakajadiliana hadi usiku na walipokutana Jumanne akamwambia kazi basi.
“David amekuwa akijiongoza kwa uadilifu na kitaaluma … hivyo inasikitisha kuona jinsi suala la mwisho wa muhula wake hapo United lilivyoshughulikiwa pasipo kuzingatia uanataaluma,” ikasema taarifa hiyo.
Jumatatu asubuhi karibu kila kona zilitanda habari kwamba Moyes angefukuzwa, na kwamba Familia ya Glazer ilishafikia uamuzi huo.
Moyes aliamini wamiliki na viongozi wa bodi walikuwa upande wake na kuwa tayari kumpa fursa kufanya usajili kwa ajili ya msimu ujao, akisema wachezaji aliokuwa nao walikuwa mzigo.
“LMA tumechukizwa sana na jinsi David alivyoondolewa Manchester United, hasa tulivyosoma ripoti zile kwa kina kwenye vyombo vya habari kuthibitisha kufukuzwa kwake kabla klabu haijamwita na kumwarifu mwenyewe,” ikasema taarifa ya chama hicho.
Hata hivyo, Man U wanakataa tuhuma na shutuma hizo, ambapo msemaji wake amedai kwamba uamuzi wa kumfukuza Moyes haukufikiwa hadi baada ya kukutana naye.
Moyes amewatakia kila la heri United ambao waliongozwa na Fergie kwa miaka 26 na kuzoa makombe 38 na kuja kupata aibu kubwa katika miezi 10 tu aliyowafundisha mabingwa watetezi hao walioshindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
“Kipimo cha ufanisi wa kazi kwa kocha wa United ni kikubwa sana, lakini sikupata hata siku moja kuacha kufanya kazi kwa juhudi kubwa.
“Ndivyo ilivyokuwa pia kwa benchi langu la ufundi. Nawashukuru kwa jinsi walivyokuwa wakijituma na kwa uaminifu mkubwa katika msimu wote huu,” akasema bosi huyo wa zamani wa Everton aliyefukuzwa baada ya klabu hiyo kumliza kwa mabao 2-0 wikiendi iliyopita.
Kocha mchezaji, Ryan Giggs (40) atachukua mikoba kwa muda tu wakati Man U wakifikiria kupata kocha wa kudumu.
Wanaotajwa zaidi kuchukua nafasi hiyo ni Kocha wa Timu ya Taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal na wa Real Madrid, Carlo Ancelotti.
Familia ya Glazers wanadaiwa tayari walishakutana na Van Gaal ambaye mkataba wake na Uholanzi unamalizika baada ya michuano ya Kombe la Dunia.
Comments
Loading…