*MK Dons yawatupa nje ya Kombe la Ligi
Mauzauza ya Manchester United dimbani yameendelea, baada ya kuchakazwa mabao 4-0 na timu ndogo ya ligi daraja la tatu ya Milton Keyness Dons.
Wakitandaza soka kama wanavyopenda bila upinzani wa kutisha kutoka kwa vijana wa Louis van Gaal, MK Dons waliwatupa nje kabisa ya Kombe la Ligi, ambalo United walianzia hatua ya pili kutokana na kumaliza Ligi Kuu ya England (EPL) katika nafasi mbovu msimu uliopita.
United walipelekeshwa na MK Dons waliokuwa wakicheza mbele ya washabiki 26,969, rekodi ambayo haijapata kuwekwa tangu timu hiyo ianzishwe, 2004, na Mashetani Wekundu hawakufanikiwa kupiga mpira kulenga lango hadi dakika ya 72.
Will Grigg alianza kucheka na nuavu baada ya Jonny Evans wa Man U kufanya makosa dakika ya 25 na kutupia la pili dakika ya 63 na kumfanya Van Gaal kuanza kubadilika sura, lakini baada ya mechi alidai hakushitushwa na matokeo, akawataka washabiki wamwamini na kuielewa falsafa ya United.
Bao la tatu na la nne yalifungwa na Benik Afobe, la tatu akilifunga baada ya kugusa mpira wa kwanza tu tangu atoke benchi dakika ya 69 na la pili akatia kimiani kumshinda David de Gea dakika saba kabla ya mpira kumalizika.
Kichapo hiki kimekuja siku ambayo United wametangaza kumsajili rasmi winga wa Argentina aliyekwua akicheza Real Madrid kwa kitita cha pauni milioni 60, wakati MK Dons kwa pamoja wachezaji wake wote hawazidi gharama ya pauni laki tano. Hii inamaanisha Di Maria anawazidi mara 120 wachezaji wote hao.
Kwa msingi huu, Van Gaal anatarajia kusaka makombe mawili tu yaliyobaki mbele yake – EPL na Kombe la FA, akiwa ameambulia pointi moja katika mechi mbili za EPL, ya kwanza Old Trafford akifungwa na Swansea na ya pili akienda sare na Sunderland kwenye dimba la Stadium of Light.
Pamoja na kuwaanzisha wachezaji kadhaa wapya, United walikuwa na wazoefu kama Javier Hernandez ‘Chicharito’, Danny Welbeck, David De Gea, Jonny Evans, Anderson na Shinji Kagawa, hivyo hawawezi kujitetea kwamba ni kukosa uzoefu.
United walizidiwa kwenye kiungo, huku kijana mwenye umri wa miaka 18, Dele Alli, aliyetabiriwa tangu Jumatatu kwamba angewatesa, akitawala eneo hilo atakavyo huku mshambuliaji Ben Reeves akiwatesa mabeki wa United, na ndiye alipika mabao matatu kati ya hayo manne.
Chipukizi wa United, James Wilson na Adnan Januzaj walijaribu kuifufua timu katika kipindi cha pili, lakini ngoma ikaonekana ilishalala mapema na haiamki tena, kwa waliokuwapo miaka 19 iliyopita wakakumbukia jinsi United walivyopoteza kwa 4-3 kwenye hatua kama hii, walipocheza na York City.
Washabiki wa MK Dons walichukua muda mrefu kushangilia ushindi mkubwa namna hiyo dhidi ya moja ya klabu zinazoitwa maarufu zaidi duniani, huku Van Gaal akiwa mtulivu muda wote wa mchezo hadi anatoka nje, na sasa anajiandaa kwa safari ya kwenda Burnley Jumamosi hii kutafuta ushindi wa kwanza.
Comments
Loading…