*Arsenal bado mauzauza
*EVERTON SASA WAWAPUMULIA ARSENAL
Manchester United wameendelea kuwa kichwa cha mwendawazimu msimu huu, ambapo usiku wa Jumanne hii wamekung’utwa mabao 3-0 na mahasimu wao wa jijini kwao, Manchester City.
Yalikuwa maudhi makubwa kwa washabiki katika uwanja wa Old Trafford ambapo vijana wa Manuel Pellegrini walicheza kwa kujiamini, bila hofu wala papara na kujipatia ushindi wao kiulaini huku wakiwazuia United kupata bao lolote.
Edin Dzeko alikuwa sumu kwa Mashetani Wekundu waliokuwa wamejipa moyo kwamba kutokuwapo kwa Sergio Aguero kungewaweka pazuri, lakini Dzeko alifunga dakika za mapema katika kila kipindi, huku Yaya Toure akifunga bao la tatu dakika za lala salama na kuwapa wakati mgumu United kwenda nyumbani.
Kocha David Moyes alionesha sura yake ya masikitiko kama kawaida, ambapo kikosi chake hakikuwa na nguvu wala kiwango. Baada ya ndoto za ubingwa kuisha na zile za kumaliza nafasi ya nne kuwa finyu, sasa si ajabu wasishike hata nafasi ya sita hivyo kushindwa kucheza hata Ligi ya Europa msimu ujao.
United walitaka kulipa kisasi kwa kichapo cha 4-1 walichopewa kwenye mzunguko wa kwanza katika dimba la Etihad, lakini kadiri mchezo ulivyokuwa unakwenda ilionekana dhahir shahir kwamba hawangeweza.
ARSENAL BADO WANAPOTEANA UWANJANI
Arsenal wameshindwa kutoka kwenye kizunguzungu cha kufungwa mabao 6-0 na Chelsea wikiendi iliyopita baada ya kulazimisha sare ya 2-2 na Swansea walio nafasi za chini katika msimamo wa ligi.
Mbele ya washabiki 59,937 kwenye dimba la Emirates, Arsenal hawakuonesha cheche tangu mwanzo na, ambapo waliruhusu kufungwa dakika ya 11 tu kupitia kwa Wilfried Bony na kuanza kujiondoa kwenye mbio za ubingwa taratibu.
Mambo yalionekana magumu hadi mapumziko ambapo baadhi ya washabiki wao waliwazomea na waliporejea uwanjani iliwachukua The Gunners hadi dakika ya 73 ambapo Lukas Podolski alipachika bao la kusawazisha na dakika moja tu baadaye Olivier Giroud akafunga la pili.
Wakati ikichukuliwa kwamba Arsenal wangeondoka kidedea, kiungo Mathieu Flamini alijifunga kwa kichwa baada ya Wojciech Szczesny kutema mpira uliompiga Mfaransa huyo na kutinga nyavuni. Swansea walikasirishwa kuondoka bila ushindi, kwani mwamuzi Lee Probert alipuliza kipenga cha mwisho wakati Jonathan de Guzman akikaribia kutikisa nyavu za Arsenal.
EVERTON SASA WAWAPUMULIA ARSENAL
Everton wameanza kutumia vyema udhaifu wa Arsenal kwa kuisaka nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, ambapo usiku wa Jumanne hii wakicheza ugenini wamewafyatua Newcastle 3-0.
Everton sasa wapo pointi sita tu nyuma ya Arsenal wanaoshika nafasi ya nne, huku Everton wakiwa na mchezo mmoja mkononi, hali inayoonesha kwamba vijana wa Roberto Martinez wamejizatiti, wakitaka nao mwakani wacheze Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mabao ya Toffees yalifungwa na Ross Barkley, Romelu Lukaku na Leon Osma, katika ushindi wao wa kwanza mkubwa zaidi ugenini msimu huu.
Kwa matokeo hayo Chelsea waliocheza mechi 31 wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 69, City waliocheza mechi 29 wana pointi 66, Liverpool mechi 30 pointi 65 na Arsenal walioshuka dimbani mara 31 wana pointi 63.
Comments
Loading…