*RVP shujaa, baadaye aumia
Manchester United wamefufuka na kufanikiwa kulipiza kisasi kwa Olympiakos na kuingia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Man U ambao wamekuwa wakidorora katika siku za karibuni, wamefanikiwa kuwatoa Wagiriki hao waliowafunga 2-0 kwao Athens wiki mbili zilizopita, ambapo Jumatano hii katika dimba la Old Trafford waliwapiga 3-0.
Shujaa wa mchezo alikuwa Robin van Persie aliyefunga mabao yote matatu, akianza kwa penati baada ya kuchezewa rafu na kumalizia mengine mawili, moja likitokana na pasi ya mshambuliaji mwenzake, Wayne Rooney.
Matokeo hayo yamempunguzia shinikizo Kocha David Moyes, ambaye baadhi ya wadau wameanza kutaka afutwe kazi kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya, yakiwamo ya kufungwa 3-0 na Liverpool wikiendi iliyopita.
Hata hivyo, Manchester walimpoteza RVP aliyetolewa uwanjani kwa machela dakika za mwisho baada ya kuumia goti na vipimo vinatarajiwa kuchukuliwa Alhamisi hii. Kipa wao, David De Gea alifanya kazi ya ziada pia kuwazuia Olympiakos kupata bao muhimu la ugenini walilohitaji ili kutibua mambo.
Wagiriki hao, hata hivyo, itabidi wajilaumu wenyewe kwa kushindwa kupata bao, kwani walikuwa na nafasi nyingi baada ya kuiyumbisha beki ya United, huku pia beki yao ikivuja mno kiasi cha kuruhusu mabao hayo.
United wanaungana na Chelsea kwa upande wa England kwenye robo fainali hizo, wakati timu nyingine zilizovuka ni za Hispania – Barcelona, Real Madrid na Atletico Madrid.
Ujerumani imevusha mabingwa watetezi, Bayern Munich na Borrusia Dortmund kama msimu uliopita wakati timu nyingine ni Paris Saint Germain ya Ufaransa. Droo ya robo fainali inapangwa Ijumaa hii.
Comments
Loading…