*Real Madrid, PSG nao waibuka kidedea
Manchester United jana walikuwa na kicheko nchini Ujerumani baada ya kuwakandika Bayer Leverkusen mabao 5-0 katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).
United walicheza mechi hiyo baada ya mshikemshike wa ndege yao kushindwa kutua mara ya kwanza asubuhi walipotoka Manchester na kuwakumbushia hofu ya ajali ya ndege iliyoua wachezaji wao karibu wote waliokuwa kwenye ndege 1958 Munich, huko huko Ujerumani.
Hata hivyo, rubani alirejesha ndege juu baada ya kuwa ameshaishusha kwa mita 400 juu ya uwanja na akajaribu kutua mara ya pili kwa mafanikio. Beki Rio Ferdinand alieleza kushitushwa na hali hiyo.
United wameingia hatua ya 16 bora wakiwa nafasi ya kwanza, hivyo wanatumaini kupangwa na timu isiyo kali kwenye mtoano huo. Man U walianza kwa kubanwa, lakini baada ya Antonio Valencia kufunga bao la kwanza dakika ya 22, haikuwa tena tabu, ikawa kama mserereko.
Mchezaji wa klabu hiyo ya Ujerumani, Spahic alijifunga mwenyewe na kuiandikia United bao la pili kabla ya John Evans, Chris Smalling na Nani 88 kumpa faraja kocha David Moyes kwa kuandika mabao.
United walitolewa jasho mwishoni mwa wiki katika Ligi Kuu ya England kwa kulazimishwa sare ya 2-2 na Cardiff City, jambo lililomkera Moyes, kwa vile wameshuka katika msimamo wa ligi tofauti na nafasi tatu za juu walizozoea enzi za kocha Alex Ferguson.
MAN CITY WASOTA KUWASHINDA VIKTORIA PLZEN
Manchester City walipata ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Viktoria Plzen, mabao ya wana Etihad yakifungwa na Sergio Agüero kwa mkwaju wa penati, Samir Nasri, Alvaro Negredo na Edin Dzeko. Yale ya Viktoria yalifungwa na Horava na Tecl.
City hawakuonesha nguvu kama waliyokuwa nayo walipowakung’uta Tottenham Hotspur 6-0 Jumapili iliyopita na kwa kweli walikuwa na wakati mgumu kutoka kwa wageni hao walioonesha kudhamiria kuwaadhiri.
Matokeo hayo hayawapi City uhakika wa kuwa wa kwanza kwenye kundi lao, kwani wanazidiwa mabao na Bayern Munich watakaocheza nao kwenye uwanja wa Allianz Arena. City wameonesha uwezo mkubwa katika kufunga mabao, kwani kwenye mechi 10 tu wametikisa nyavu mara 41 msimu huu nyumbani, lakini tatizo ni wanapokuwa ugenini na pia beki yao ina tatizo kiasi.
REAL MADRID WAWAPIGA GALATASARAY
Wakicheza bila mchezaji wao bora katika ufungaji, Cristiano Ronaldo, Real Madrid walifanikiwa kuwafunga Galatasaray mabao 4-1 na kukata tiketi ya kuingia kwenye 16 bora.
Vijana hao wa Carlo Ancelotti walionesha uwezo mkubwa, ambapo kwa dakika 74 walicheza watu 10 baada ya Sergio Ramos kumchezea rafu Umut Bulut. Alikuwa ni mchezaji aghali zaidi, Gareth Bale aliyefungua kitabu kwa kufunga kupitia mpira wa adhabu ndogo kutoka yadi 25.
Vijana wa Roberto Mancini walichachamaa, ambapo Bulut alisawazisha lakini Alvaro Arbeloa aliongeza bao la pili kwa mpira wa chini chini kabla ya kumtengea pande Angel Di Maria aliyefunga la tatu. Mchezaji wao mpya, Isco alifunga bao na kulifurahia mno.
Madrid wamefikisha pointi 13, zikiwa ni saba zaidi ya Juventus wanaoshika nafasi ya pili.
MATOKEO MENGINE MECHI ZA UCL
Matokeo mengine katika ligi hiyo yalikuwa Shakhtar Donetsk kuwafunga Real Sociedad 4-0, Juventus wakawapiga FC Copenhagen 3-1, Paris Saint Germain wakawashinda Olympiakos 2-1. RSC Anderlecht walipoteza nyumbani kwa kufungwa na Benfica 3-2, kama CSKA Moscow walivyonyanyaswa na Bayern Munich kwa kufungwa mabaoa 3-1.
Comments
Loading…