Matumaini ya Manchester City kutetea ubingwa wake yameanguka baada ya kuchapwa na Crystal Palace 2-1 kwenye mechi muhimu ya Ligi Kuu ya England (EPL).
City waliokuwa wanatarajia kuwakimbiza Chelsea wanaoongoza ligi wamejikuta wakibaki pointi tisa nyuma yao, huku Chelsea wakiwa na mechi moja mkononi.
Hii ni mechi ya nne mfululio ugenini Man City wanapoteza, na sasa nafasi ya Kocha Manuel Pellegrini ipo shakani, kwani wamiliki wanataka kuona makombe.
Kadhalika mabingwa hao watetezi wamejikuta wakibakiwa na pointi zao 61, nyuma ya Manchester United wenye 62 na Arsenal wenye 63 ambao wanashika nafasi ya pili.
Kwa ushindi huo, Palace wamechupa hadi nafasi ya 11 na watajipongeza kwa uamuzi wao wa kumchukua kocha wa zamani wa Newcastle, Alan Pardew.
Glenn Murray aliwapa bao Crystal Palace bao la kwanza kabla ya Jason Puncheon kutia la pili kwa mpira wa adhabu ndogo nje kidogo ya eneo la penati.
Kiungo mahiri wa Ivory Coast anayedhaniwa atahama klabu hiyo, Yaya Toure alichomoa bao moja lakini haikutosha kuwaokoa kupoteza pointi.
Kazi ipo kubwa kwa Man City, kwani wikiendi ijayo kuna mechi na watani zao wa jadi, Manchester United wanaoelekea kuwa katika hali nzuri.
Liverpool waliopondwa na Arsenal 4-1 Jumamosi wanashika nafasi ya tano wakiwa na pointi 54 sawa na wanaowafuatia, Tottenham Hotspur wakati Southampton ni was aba, Swansea wa nane, West ham wa tisa na Stoke wa 10.
Mkiani wapo Leicester wenye pointi 22, QPR 25 na Burnley wenye 26. Wengine walio hatarini kushuka daraja ni Aston Villa wenye pointi 28 katika nafasi ya 17, pointi moja pungufu ya Sunderland.
Comments
Loading…