*Arsenal, Chelsea, Liverpool, Spurs safi
Kocha David Moyes alikuwa na wakati mgumu alipoikaribisha timu yake aliyoiongoza kwa miaka 11 ya Everton katika dimba la Old Trafford.
Kwa mara nyingine tena, Manchester United wamefanya vibaya katika mechi ya Ligi Kuu ya England (EPL), baada ya kukubali kichapo cha 1-0.
Katika mtangange uliokuwa mkali na wa kuvutia, vijana wa Roberto Martinez walifanikiwa kupata bao kipindi cha pili baada ya kosakosa kadhaa.
Huu ni ushindi wa kwanza kwa Everton katika dimba hilo kwa zaidi ya miaka 11, ikimaanisha kwamba kila Moyes alipopeleka kikosi hapo hakuweza kumshinda mtangulizi wake, Sir Alex Ferguson ambaye jana alikuwa jukwaani kwa masikitiko.
Arsenal waliendelea kugawa dozi, ambapo Jumatano hii waliwafunga Hull City 2-0 kwa mabao ya Nicklas Bendtner na Mesut Ozil.
Hull waliingia Emirates wakijiamini baada ya kuwafunga Liverpool 3-1 mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo, vijana wa Arsene Wenger walijiamini na kujizatiti kileleni mwa ligi, ambapo sasa wamefikisha pointi 34.
Chelsea nao walicheza kufa na kupona dhidi ya timu dhaifu Sunderland, na kuonesha kwamba kuna tatizo kwenye kikosi cha Jose Mourinho.
Chelsea walipata ushindi wa tabu wa mabao 4-3 katika piga nikupige na vijana wa kocha Gus Poyet.
Liverpool waliopunguzwa kasi walirejea kwa kishindo walipowachabanga Norwich 5-1, ambapo Luis Suarez alishafunga hat-trick katika kipindi cha kwanza tu.
Manchester City nao walipata ushindi wa tabu wa 3-2 nyumbani kwa West Bromwich Albion na kujihifadhia heshima yake.
Tottenham Hotspur ambao kocha wake alikuwa kwenye shinikizo la kujiuzulu kutoka kwa baadhi ya watu, wamepata ushindi mwembamba wa 2-1 dhidi ya vibonde Fulham.
Swansea nao waliamka usingizini na kuwavurugia mambo Newcastle waliokuwa na mfululizo wa ushindi. Swansea wanaofundishwa na Michael Laudrup waliwapiga Newcastle 3-0 huku Stoke wakienda suluhu na Cardiff katika mechi pekee isiyokuwa na bao kwenye mzunguko huu wa 14.
Southampton wakicheza nyumbani waliendelea kuwa doro baada ya kufungwa mabao 3-2 na Aston Villa.
Katika mechi ya Jumanne usiku, Crystal Palace walio chini ya kocha mpya, Tony Pulis waliwafunga West Ham bao 1-0 kwa bao la mchezaji wa zamani wa Arsenal, Marouan Chamakh.
Kwa matokeo hayo, Arsenal wanaongoza ligi ya tofauti ya pointi nne wakifuatiwa na Chelsea wenye pointi 30, Man City pointi 28, Liverpool na Everton 27.
Comments
Loading…