*Walijaribu kumuuza tangu Januari
*Radamel Falcao kujiunga Chelsea
Habari zimevuja kwamba Manchester United hawamtaki mshambuliaji wao wa kati, Robin van Persie na kwamba tangu Januari mwaka huu walijaribu kumuuza kwa klabu mbalimbali za Ulaya bila mafanikio.
Hata hivyo, United walikuwa wakiwasiliana na klabu mbalimbali ili kuwapa Mdachi huyo bila mwenyewe kujua,akiendelea kujitahidi kuwa na kiwango bora bila mafanikio na wakati mwingine akikumbwa na majeraha.
Mchezaji mwenzake wa zamani, Pierre van Hooijdonk ambaye pia ni Mholanzi, anasema kwamba mazungumzo yalishafanyika na Fenerbahce tangu Januari lakini RVP hakuwa na habari ya kinachoendelea juu yake.
Hivi karibuni Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal alimwambia RVP kwamba itabidi abadilike kwa kukuza kiwango chake ikiwa anataka kuwa na namba kwenye kikosi cha kwanza. Hata akiwa na utimamu wa mwili kuna wakati amekuwa akiachwa benchi sambamba na akina Angel Di Maria na Radamel Falcao.
United wanaelezwa kwamba katika msimu huu wa kiangazi wamefungua milango yao wakiwa tayari kusikiliza ofa kutoka klabu yoyote ili wawauzie Van Persie (31) kwani kiangazi kijacho hatakuwa tena na mkataba na anaweza kuondoka bure.
Akiandika kwa mara ya kwanza safu yake kwenye jarida la ‘Voetbal International’ mchezaji huyu ana haya ya kusema juu ya RVP:
“Tangu Januari mwaka huu nilikuwa Napata taarifa kutoka Uturuki juu ya jamaa yangu Robin kutaka kuuzwa Fenerbahce. Nilipopata taarifa hizi ni kwamba maofisa wa United walishaenda ‘kupima maji’ huko kuona uwezekano wa klabu hiyo kumnunua.
“Mawakala na watu wengine walikuwa wakiwasiliana na klabu kubwa zilizokuwa zimejiandaa kulipa ada kubwa kwa ajili ya mchezaji huyo. Mkataba wa Robin unamalizika mwaka kesho kwa hiyo huu ndio wakati ambao United wanaweza kutengeneza fedha kwa kumuuza, na ndicho wanahangaikia bado.
“Van Persie ana wakati mgumu. Akiwa nje ya United anadai kwamba ana furaha kuwa Old Trafford nami naweza kumwelewa katika hilo lakini ukweli ni kwamba Robin anajihisi vibaya kwamba United wanataka kuondokana naye. Klabu kubwa ya England, Hispania au Ujerumani ni fursa ya kumvutia zaidi lakini hadi mchezaji amaizi unakuta klabu mbili zimeshafanya dili kubwa.
“Ukweli ni kwamba nyakati kama hizi shinikizo linakuwa kwa mchezaji, unajihisi kwamba hupendwi wala hutakiwi na unasukumwa ili uondoke klabuni ambako uliajiriwa lakini mwajiri huyo huyo anakuzunguka. Huo ndio mchezo unaochezwa sasa kwa Robin.
“Ni wazi kwamba fedha ni kitu kizuri na maisha pia ni mazuri Istanbul, lakini ligi ya kule si kubwa kwa namna yoyote katika Ulaya wala si gumzo. Anatakiwa kufanya mambo makubwa kabla ya michuano ya Euro ambayo huenda ikawa ya mwisho kwake na kwa msingi huo lazima awe kwenye klabu anakopata muda mwingi wa kucheza.
“Nahisi pia kwamba uhusiano wake sasa na kocha Van Gaal si mzuri, tofauti na ilivyokuwa wakati wakiwa na Timu ya Taifa ya Uholanzi na wakisubririana kwa hamu kufanya kazi pamoja United. Namshauri aondoke United kiangazi hiki kwa sababu dalili zote zipo wazi kwamba klabu inataka kumuuza hivyo aondoke mapema.”
Iwapo Van Persie ataondoka, moja ya timu zinazomtaka kwa udi na uvumba sasa ni Besiktas, ikidhaniwa kwamba Fenerbahce hawamhitaji tena. Badala yake, wametoa ofa ya pauni milioni 3.5 kwa ajili ya kumsajili winga wa Man U, Nani, 28, aliyecheza kwa mkopo nyumbani kwao Ureno msimu uliopita, katika klabu ya Sporting Lisbon. Man U wamekataa ofa hiyo na wanamkadiria kuwa na thamani ya pauni milioni sita.
Habari nyingine zinasema kwamba mchezaji wa Monaco aliyecheza kwa mkopo Man United msimu uliopita, Radamel Falcao yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na Chelsea, familia ya mwanasoka huyo imesema.
Baba na mjomba wa Falcao wamethibitisha wiki hii kwamba dili limeshakubaliwa na mkataba kusainiwa jijini London, ikiaminiwa kwamba ni mkopo wa mwaka mmoja, huku kukiwa na kipengele cha kuwezesha klabu kumsajili moja kwa moja kiangazi kijacho.
Pamoja na kwamba Chelsea hawajatangaza rasmi, kocha wa klabu hiyo, Jose Mourinho alisema alikuwa na nia ya kumsaidia mshambuliaji huyo wa Colombia kurudia katika kiwango chake cha juu.
Mazungumzo yamefanyika kwa wiki tatu kati ya wakala wa Falcao, Mreno Jorge Mendes na maofisa wa Chelsea baada ya United kuamua kuachana naye kwani hakuwafaa chochote msimu mzima na badala yake akawa anachota mshahara wa pauni 265,000 kwa wiki.
Imekubaliwa na Chelsea kwamba atapunguziwa mshahara huo hadi pauni 180,000 kwa wiki na gharama za kumsajili kwa mkopo kutoka Monaco ni pauni milioni nne hivi. Baba yake Falcao, Radamel García, naye alikuwa mwanasoka na anasema kwamba mwanawe atajiunga na Chelsea kati ya Julai 19 na 20.