MANCHESTER United wameachana na kocha wao mwenye makeke, Jose Mourinho ‘The Special One, The Happy One, The Only One’ baada ya kuvunja rekodi ya miaka mingi ya kufanya hovyo uwanjani.
Wengi tulishangazwa na uamuzi wa Man U kumchukua kocha huyo, miaka miwili unusu iliyopita, kwa sababu kimsingi haendani na hali ya Old Trafford, taratibu zake, tamaduni na kwa ujumla uhafidhina ambao wamekuwa nao wakuu hapo.
Bwana huyu alianza kujenga urafiki na Sir Alex Ferguson kabla hajastaafu, na inadaiwa kwamba alikuwa akijaribu kujikomba ilia pate kazi hapo. Hata hivyo, Fergie aliondoka ghafla na kupendekeza kazi yake apewe Mskochi mwenzake, David Moyes aliyefukuzwa kabla hata ya mwaka, akaajiriwa Luis van Gaal naye akafukuzwa kabla ya mkataba wake kumalizika.
Ilivyo ni kwamba Mourinho alikuwa msaidizi wa Van Gaal enzi za Barcelona, kazi yake kubwa ikiwa ni tafsiri ya lugha na kujenga uhusiano baina ya kocha huyo mkuu wa zamani na wachezaji, jambo linalosemwa alilifanya vyema huko Uhispania.
Baada ya kufukuzwa kazi, Van Gaal alieleza kushangazwa na kitendo cha msaidizi wake huyo wa zamani kumzunguka na kuchukua kibarua chake hapo Old Trafford; kwamba Mourinho alishajua anafukuzwa kabla ya hata yeye na kwamba mkewe Van Gaal alipata taarifa kwa watu wengine naye Van Gaal akiendelea na mipango kwa ajili ya timu akashitushwa kuambiwa hana kazi tena.
Lakini naye Mourinho yamekuja kumfika hayo hayo,ikiwa ni baada ya kupokea kichapo kutoka timu ya mtu ambaye alipata kumpa kichapo na kupoteza kazi. Ni Jurgen Klopp ambaye kwa mara ya pili amemfukuzisha kazi – mara ya kwanza alikuwa na Borussia Dortmund na sasa akiwa na Liverpool, ambapo Liver waliwapiga Man U 3-1 kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).
Mourinho aliwaacha United katika hali mbaya wakiwa nafasi ya saba, wakati kawaida yao ni kutamba kule juu; kama si nafasi ya kwanza basi walau isizidi ya nne na hali ikiwa mbaya sana ya tano kama alivyofanya hivi karibuni na kuiingiza timu Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) kwa uchochoro wa kutwaa kombe la Ligi ya Europa.
Akiwaacha nafasi ya saba, akipoteza michezo lakini pia akikorofishana na wachezaji, wengine akiwatupa kando bila sababu za msingi na baadhi akiwasema vibaya hadharani, Mourinho alionekana kuwa ndiye mwenye matatizo.
Amekosana na hata aliyemnunua kwa bei mbaya baada ya United kuwa wamemwachia bure akiwa tineja, Paul Pogba, ambaye ameng’ara sana na timu nyingine, ikiwa ni pamoja na kutwaa ubingwa wa dunia akiwa na Timu ya Taifa ya Ufaransa.
Mourinho aliishia kulalamika kwamba haukufanyika usajili mzuri huku akitaka kuuza wachezaji wenye vipaji na umri mdogo ndipo akakataliwa na Makamu Mwenyekiti Mtendaji, Ed Woodward aliyesema lazima wakuze vipaji na kwamba atumie wachezaji waliopo ambao ni wazuri kama akina Alexis Sanchez ambaye hadi Mourinho anatimuliwa alikuwa akitafaari juu ya hatima yake.
Lakini wapo watu kama akina Pogba, Romelu Lukaku, David de Gea golini ambaye kwa mabao yale matatu ilikuwa kama fedheha kubwa kwake. Mourinho alifikia hata kukosana na Nahodha Antonio Valencial na ukishafika katika hali hiyo, ni ngumu kusema kwamba timu ingeweza kufanya vyema uwanjani, kwani misingi ya ufanisi na tija aliiharibu kocha.
Mchezaji mwingine ambaye alikosana na Mourinho kiasi cha kukaribia kufurushwa ni beki wa kimataifa wa pembeni, Luke Shaw ambaye kwa mechi tatu mfululizo za Mourinho alitupwa kando, lakini baada ya kocha mpya kuingia akampa dakika zote 90.
Amefikia kuwa chini kwa sana ya Liverpool na Manchester City, lakini akashindwa kupanda na kuwa sawa na akina Tottenham Hotspur, Chelsea na Arsenal na sababu si kwamba hakuwa na wachezaji wazuri, bali ni ile kuwa mtu wa kuwachanganya wachezaji na kukataa kubadili mifumo ili kuhakikisha mchezaji fulani anapata nafasi kama alivyomwondosha Henrik Mkhitaryan akaenda Arsenal na kuwa mtamu kuliko Sanchez aliyemnunua.
Ameingia kocha mpya (wa muda) Ole Gunar Soskjaer ambaye mechi ya kwanza alipata ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Cardiff, idadi ya mabao ambao United hawakumbuki lini walipata kuyafunga. Ni mapema kusema kwamba kocha huyu atafanya vyema hadi mwisho wa msimu, lakini ukweli ni kwamba United wangeweza au wanaweza kufanya vyema zaidi chini ya kocha mwingine kuliko Mourinho.
Naamini kwamba bado United ambao kabla ya Krismasi walikuwa na alama 29, Arsenal wakiwa nazo 37 sawa na Chelsea huku Spurs wakiwa na alama 42, mbili pungufu ya Manchester City na sita pungufu ya Majogoo wa Anfield – Liverpool, wanaweza kujikongoja na kupanda huko juu.
Nilikuwa namfuatilia kocha wa City, Pep Guardiola baada ya kuchezea kichapo cha 3-2 kwa Crystal Palace nyumbani kwao Etihad, Manchester sawa na Arsenal walichopata wiki ile nyingine kutoka kwa Southampton, kutoka, akisema si kitu kwani bado huko mbele kuna mechi nyingi na alama za kupigania.
Kwa mtaji huo huo, Man U bado hawajachelewa sana, pengine wamefanya vyema kumfukuza Mourinho kabla ligi haijafikia nusu au kusubiri Januari kwenye dirisha dogo, ili kocha mpya apate muda wa kuwatazama wachezaji wake na kusuka kikosi cha kwanza na kutoa maelekezo.
Ni wazi United wangependa kuwa kwenye zile nne bora kule juu sasa lakini lazima waende taratibu na kuhakikisha hawapotezi alama hovyo hovyo kama ilivyokuwa chini ya Mourinho. Msimu huu United wapo kwenye UCL tayari na kwenye mtoano ujao wamepangiwa dhidi ya mabingwa wa Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG) na Mourinho kafukuzwa kabla ya kuwakabili akina Neymar, Kylian Mbappe na wakali wengineo.
Kocha huyu ni mchezaji wa zamani wa United, anajua vyema utamaduni na utaratibu wa hapo Old Trafford na kwa kushirikiana na wengine wa benchi la ufundi, ni wazi anaweza kufanya vyema na kurejesha tena ile heshima ya Man United iliyokuwapo zamani. United kimsingi ndio watani wa jadi au mahasimu wa kinchi na Liverpool, lakini kuna wakati Liver walianguka mno na utani kutookana na sasa Man U wameanguka mno, pengine ni wakati wa kurejesha kiwango kile.