Jitihada za Kocha Jose Mourinho ‘The Only One’ kumpata mpachika mabao wa Manchester United, Wayne Rooney zimegonga tena mwamba.
Mashetani Wekundu wamekataa ofa ya pili kutoka Stamford Bridge kwa mshambuliaji huyo wa Uingereza anayelilia kuondoka Old Trafford.
Dau la safari hii linafika pauni milioni 25 pamoja na marupurupu mengine, lakini United wanadai kwamba Rooney (27) hauzwi.
Rooney aliyesajiliwa Manchester na Alex Ferguson kutoka Everton wakati kocha wa sasa wa United, David Moyes akiwa kocha wake United, ameomba mara mbili kuhama.
Alipata kugombana na Moyes Everton na pia na Fergie hapo Old Trafford, hivyo anaamini huu ni wakati mwafaka kwenda kukabiliana na changamoto mpya sehemu nyingine.
Rooney aliyewachezea United mechi 402 na Uingereza mechi 83, amewafungia Man U mabao 197 na England mabao 36 na alikuwa mchezaji bora wa England mwaka 2010.
Rooney aliachwa kwenye kikosi kilichokwenda
Stockholm kwa ajili ya mechi za kirafiki, akielezwa kukabiliwa na jeraha la bega, alilopata walipokwaana na Real Betis Jumamosi.
Dau la kwanza la Chelsea kwa United kwa ajili ya kumpata Rooney lilikuwa pauni milioni 20, ambapo walikataa, Moyes akisisitiza kwamba huyo atabakia kuwa mchezaji wao, lakini Mourinho anang’ang’ania kumchukua.
Inaelezwa kwamba Rooney amekasirishwa na kuchanganywa na habari za karibuni za United kukataa ofa za Chelsea kutaka kumchukua, hasa baada ya Moyes kusema chaguo lake la kwanza katika kikosi chake ni Mholanzi Robin van Persie na Rooney atasubiri benchi.
Mchezaji huyo anafikiria kutoa ombi rasmi la kuondoka, ili atie shinikizo zaidi kuondoka Old Trafford alikipata kulilia kuondoka 2010, kabla ya kusaini mkataba mpya wa miaka mitano.
Comments
Loading…