Manchester United na Sunderland wamefanikiwa kuvuka katika mechi za marudiano za michuano ya FA, ambapo United wamewafunga Cambridge United 3-0 baada ya kubanwa kwenye mechi ya awali.
Kocha Louis van Gaal alichezesha kikosi chake cha kwanza, kikiwa kinagharimu pauni milioni 231 huku kile cha Cambridge kikiwa hakigharimu chochote na kipo nafasi 79 chini ya Man U ambao sasa watacheza na Preston katika hatua ya tano ya mashindano hayo.
Wakicheza nyumbani Old Trafford, Manchester United walitishwa dakika za mwanzo ambapo mshambuliaji wa wageni,Tom Elliott alishindwa kukwamisha mpira kimiani baada ya makosa ya Daley Blind dakika ya kwanza tu.
Hata hivyo, United waligangamala na kupata mabao yao kupitia kwa Juan Mata, Marcos Rojo na James Wilson na kumaliza hatua hii ngumu na iliyowatoa jasho vilivyo. Van Gaal sasa amewaambia vijana wake wawe tayari kwenda hadi fainali na kulitwaa kombe hilo.
Katika mechi nyingine, Sunderland walipambana na kufanikiwa kuwafunga Fulham 3-1, baada ya kuwa nyuma kwa bao hilo moja hadi dakika ya 60, lililofungwa na Hugo Rodallega. Kipa wa Fulham walio ligi daraja la pili, Marcus Bettinelli alifanya makosa kwa kujifunga kabla ya wageni kuongeza mawili. Kwenye mechi nyingine Sheffield United walifungwa 3-1 na Preston.
Comments
Loading…