*Vermaelen, Cech, Ings kazi
*Guardiola na Mourinho kibri
Habari kwamba mshambuliaji wa Napoli, Gonzalo Higuain anataka kuondoka Napoli zimewasukuma Manchester United na Arsenal kumfuatilia.
Higuain (27) aliwindwa na Arsenal akiwa Real Madrid lakini akaamua kwenda kucheza chini ya bosi Rafa Benitez.
United wanataka kuimarisha safu yao ya ushambuliaji, ambapo Kocha Louis van Gaal amepata kutamka wazi kwamba hana washambuliaji mahiri.
Hata hivyo, Man U wanao Wayne Rooney ambaye ameamua kumchezesha kwenye kiungo, Robin van Persie ambaye ameshuka kiwango na huumia mara kwa mara na Radamel Falcao aliye kwa mkopo na hajacheza vyema.
Arsenal pia wapo vyema kwenye ushambuliaji japokuwa huenda wanataka kupata wenye uzoefu zaidi.
Manchester United wanatarajia kwamba mshambuliaji matata wa Burnley, Danny Ings (23) atawakataa Liverpool na kutinga Old Trafford. Everton wamepanga kumsajili beki wa kati wa Barcelona, Thomas Vermaelen (29) ambaye tangu asajiliwe hajacheza mechi hata moja.
Nahodha huyu wa zamani wa Arsenal alikuwa anatakiwa na Manchester United lakini Arsenal hawakupenda kumuuza kwa wapinzani wao ndani ya ligi kuu ya England.
Liverpool wameingia katika mipango ya kumsajili kipa wa Chelsea, Petr Cech (32), na lengo lao ni kumchukua kwa mkopo wa msimu mmoja kwa pauni milioni saba.
Kipa namba moja wa sasa wa Liver, Simon Mignolet alianza hovyo msimu huu akiruhusu mabao ya kushangaza lakini kadiri muda unavyokwenda anarudi kiwango cha msimu uliopita.
Southampton na Newcastle wameeleza kutaka kumsajili mshambuliaji mahiri wa Queen Park Rangers (QPR), Charlie Austin (25).
Manchester City wanataka kumsajili mlinzi wa Athletic Bilbao, Aymeric Laporte (20).
Beki wa Sunderland, Wes Brown (35) anafikiriwa kwamba ataondoka klabuni hapo mwisho wa msimu huu, maana mkataba wake unaisha na hakuna mazungumzo yoyote yaliyoanza.
Beki huyu wa zamani wa Manchester United yupo nje ya dimba baada ya kuumia goti na huenda asicheze tena msimu huu. Ni mchezaji muhimu kwa Sunderland lakini kuumia kwake mara kwa mara na umri kusogea kunaifanya klabu kufikiria kusajili chipukizi walio timamu wa mwili zaidi.
Udinese na Deportivo La Coruna wanaongoza katika mipango ya kumsajili kiungo wa Tottenham Hotspur, Grant Ward (20).
Makocha Jose Mourinho na Pep Guardiola wameonesha kujiamini katika nafasi zao na kuendelea kufanya kazi kama kawaida.
Guardiola wa Bayern Munich amebeza kitendo cha jopo la madaktari sita wa timu hiyo kuachia ngazi Alhamisi hii, akisema timu itaendelea kama kawaida.
Madaktari hao waliondoka kwa hasira baada ya madai kwamba ndio walisababisha Bayern wakafungwa 3-1 na Porto kwenye mechi ya mkondo wa kwanza ya robo fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Upande mwingine, Mourinho wa Chelsea amesema kibarua chake Stamford Bridge hakipo hatarini.
Mourinho amedai amehakikishiwa na Kocha Jurgen Klopp wa Borrusia Dortmund kwamba hajatangaza kuachia ngazi ili aje kuwa kocha wa Chelsea.
Mourinho pia amewataka wamiliki wa Manchester City wasimfukuze Kocha Manuel Pellegrini, kwa sababu haoni sababu. Pellegrini mwenyewe amesema kufukuzana si suluhu kwa City.
Sunderland wamesema wanataka kumchukua Kocha wa Swansea, Garry Monk (36).
Comments
Loading…