Man U suluhu, RVP akosa penati
Manchester City wamefanikiwa kupata ushindi muhimu na kujihakikishia kuvuka hatua ya mtoano, huku wenzao Manchester United wakienda suluhu.
United walikuwa wakicheza dhidi ya Real Sociedad ambao walikuwa wamepoteza mechi zote zilizopita.
Mmoja wa wafungaji tegemeo wa Man U, Robin van Persie ‘RVP’ alihaha kutafuta mabao bila mafanikio na hata bahati ya mtende ilipomjia ya kupata penati alishindwa kufunga.
Kocha David Moyes alilalamikia kushindwa kwa timu yake kutengeneza nafasi au kutotumia zile walizopata ambapo hawakuianza mechi vyema.
Hata hivyo, wamebaki katika nafasi ya kwanza kwenye kundi lao ambapo RVP pia aligonga mwamba kwa mpira mwingine alipotaka kufunga baada ya majalo ya Ashley Young.
Kiungo Marouane Fellaini alitolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika za mwisho kwa mchezo mbaya, na hii inaweza kuwa onyo kwake, maana msimu uliopita katika ligi kuu ya England alikuwa akishutumiwa kwa mchezo wa rafu pia.
PELLEGRINI ATAMBA KUMFUNGA YEYOTE
Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini ametambia ukali wa kikosi chake na kusema sasa wanaweza kuifunga tomu yoyote ile.
Alvaro Negredo alifunga mabao matatu nyumbani walipocheza na CSKA Moscow, katika mechi iliyomalizika kwa ushindi wa mabao 5-2.
Man City waliwafunga Warusi hao nyumbani kwao pia, ambapo katika mechi ya usiku huu wa Jumanne, Sergio Aguero alifunga mabao mawili.
Kipa namba moja aliyeonekana kuzorota kwenye mechi kadhaa zilizopita, Joe Hart aliachwa benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Costel Pantilimon wa Romania. Hart ndiye kipa namba moja wa timu ya taifa ya England pia.
Mabao ya CSKA Moscow yalifungwa na Seydou Doumbia.
MATOKEO MENGINE UCL
Katika mechi nyingine za usiku wa Jumanne, Shakhtar Donetsk walikwenda suluhu na Bayer Leverkusen na FC Copenhagen wakawafunga Galatasaray 1-0.
Juventus walienda sare ya 2-2 na Real Madrid katika mechi ambayo Gareth Bale na Cristiano Ronaldo walifunga bao moja kila mmoja.
Olympiakos waliwafunga Benfica 1-0; Paris Saint Germain wakatoka sare ya 1-1 na RSC Anderlecht huku Viktoria Plzen wakilala 0-1 kwa Bayern Munich.
Comments
Loading…