*Chelsea wakwama kwa vibonde West Ham
Kwa mara ya pili katika msimu huu wa Ligi Kuu ya England, Manchester City wamewaadhiri Tottenham Hotspur kwa kuwakandika idadi kubwa ya mabao.
Wakati usiku wa kuamkia Alhamisi Man City wamepeleka mafuriko ya mabao 5-1 White Hart Lane, mechi ya awali Etihad waliwafunga Spurs 6-0 na kusababisha Andre Villas-Boas kufukuzwa ukocha.
Wakicheza kwa kujiamini kutokana na rekodi nzuri tangu kocha mpya Tim Sherwood aingie kazini, Spurs walianza kupelekeshwa lakini walimudu kiasi.
Walifungwa bao la kwanza na Sergio Aguero ambaye hata hivyo baadaye aliumia na kutolewa nje na bao la Spurs la kusawazisha lilikataliwa kwa Michael Dawson kuotea kabla mpira wa adhabu ndogo haujapigwa.
Pigo lililowapoteza Spurs ni kutolewa kwa kadi nyekundu beki aliyecheza vyema kwa kupanda na kushuka, Danny Rose baada ya kumtega kwa nyuma Edin Dzeko aliyekuwa katika nafasi ya wazi ya kufunga. Yaya Toure alipiga penati na kufunga bao la pili.
Rose alitolewa nje baada ya wachezaji wa City kumzonga mwamuzi Andre Mariner aliyepata ushauri wa wasaidizi wake kabla ya kutoa kadi nyekundu.
Hata kwenye uamuzi kuhusu bao la kuotea la Spurs mwamuzi huyo alielekezwa na msaidizi wake na kuwaacha wachezaji wa Spurs wakiwa hoi.
Mabao mengine ya City yalitiwa kimiani na Stefane Jovetic, Dzeko na nahodha Vincent Kompany. Bao la Spurs lilifungwa na Etiene Capoue.
Ushindi umewafanya Manchester City kuwang’oa Arsenal kileleni mwa EPL kwa kufikisha pointi 53 ikiwa ni moja zaidi ya Washika Bunduki hao wa London.
Katika mechi nyingine, Chelsea walitoka suluhu walipowakaribisha West ham United walio katika eneo la kushuka daraja.
Ushindi kwa Chelsea ungewafanya washike nafasi ya pili lakini kutokana na West Ham kulinda lango lao barabara, Chelsea wamebaki nafasi ya tatu wakiwa na pointi 50.
Chelsea waliitawala mechi lakini wakachanganywa na vijana wa Sam Allardyce ambapo shuti la Oscar liligusa mtambaa wa panya na jitihada za John Terry hazikuzaa matunda.
Samuel Eto’o aliuendea mpira uliokuwa umetengwa na kipa Adrian wa West Ham kwa ajili ya kupiga naye akaujaza wavuni lakini akazuiwa.
Usiku huo ulishuhudia pia Sunderland wakijiondoa kwenye eneo la kushuka daraja kwa kuwafunga Stoke bao 1-0 na Aston Villa wakiwafunga West Bromwich Albion 4-3.
Msimamo wa ligi sasa unaonesha Liverpool wakishika nafasi ya nne wakifuatiwa na Spurs, Everton na Manchester United bado ni wa saba wakifuatiwa na Newcastle, Southampton na Aston Villa wanafunga 10 bora.
Timu tatu zilizo nafasi za kushuka daraja ni West Ham wenye pointi 19 sawa na Fulham wakati Cardiff wanashika mkia kwa pointi zao 18.
Comments
Loading…