Wakati kipa Joe Hart wa Manchester City ameambiwa kuna makipa wawili namba moja Etihad, timu hiyo inaingia kwenye mechi ya Ngao ya Jamii Jumapili hii bila nyota wake wanane.
Wachezaji wapya Frank Lampard aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka New York City na Bacary Sagna hawatacheza mechi hiyo, ikielezwa Lampard hayupo fiti kuanza sasa, ila Sagna na wenzake waliovuka hadi hatua za mtoano za fainali ya Kombe la Dunia wanapewa muda wa kupumzika.
Wengine ambao hawatakuwapo ni Sergio Aguero, Pablo Zabaleta, Martin Demichelis, Fernandinho na nahodha Vincent Kompany. Kwa upande wake, Alvaro Negredo anakosa mechi hiyo kwa vile ameumia wayo.
Kocha wa Man City, Manuel Pellegrini ameshamweleza Hart (27) kwamba watakuwa wawili wanaotambuliwa kuwa kiwango kimoja, na hiyo ni kutokana na kusajiliwa kwa Willy Caballero kutoka Malaga.
Hart alirejea kuwa chaguo la kwanza msimu uliopita baada ya kutupwa kando kidogo kumpisha Costel Pantilimon kwenye mechi kadhaa. Pantilimon sasa amejiunga na Sunderland.
Caballero alipata kucheza chini ya kocha Pellegrini huko Malaga, na amemnunua kwa pauni milioni 4.4 na anatarajiwa kucheza kwenye mechi hii ya Jumapili inayopigwa kwenye Uwanja wa Wembley. Caballero amecheza mechi zaidi ya 100 akiwa Malaga katika kipindi cha miaka mitatu.
“Nina uhakika Willy atakuwa muhimu sana kwetu lakini tunaye kipa bora zaidi wa England katika Joe Hart. Timu kubwa zinatakiwa kuwa na wachezaji wawili katika kila nafasi kwa sababu tuna mechi nyingi sana za kucheza katika msimu,” akasema Pellegrini.
Raia huyo wa Chile anasema kwamba njia bora zaidi ya kuwa na ufanisi uwanjani ni kuwa na ushindani mkubwa miongoni mwa wachezaji. Fernando aliyesajiliwa kiangazi hiki anaweza pia kuanza kwenye mechi hiyo.
Comments
Loading…