Kujiuzulu ghafla kwa Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter kulichukuliwa kwa mshangao na wengi, lakini hatua yake hiyo inaelekea kufungua mkururo wa mambo mengi, ikiwa ni pamoja na maofisa wa chini yake kuamua kumwaga siri zake.
Makamu wa Rais wa Fifa wa zamani, Jack Warner, amesema katika mahojiano na kituo cha televisheni kwamba hana muda wa kuficha tena siri, bali ataanika yote anayojua juu ya rushwa katika ulimwengu wa soka leo hii.
Warner, 72, amesema anahofia usalama wake, lakini akasema anaihusisha Fifa na uchaguzi mkuu wa kwao Trinidad & Tobago uliofanyika mwaka 2010. Huyu ni mmoja wa watu 14 wanaoshitakiwa na Marekani kwa tuhuma za rushwa na utakatishaji fedha.
Makamu huyo wa rais alijiuzulu kujihusisha an masuala yote ya soka 2011 baada ya kuhusishwa na tuhuma za rushwa na baadaye aliachia ngazi pia katika nafasi ya Waziri wa Usalama wa Trinidad & Tobago wakati akichunguzwa pia kwa kujihusisha na mlungula.
Warner amesema kwamba tayari amewapa wanasheria nyaraka zinazoonesha jinsi wakuu wa Fifa walivyojihusisha na rushwa, fedha zilikotoka na masuala yake mwenyewe na uchaguzi wa 2010 nchini mwake, akidai hata Blatter alihusika.
“Sitakaa tena kimya juu ya mambo yaliyokuwa yakifanyika kwa ajili ya kuiharibu nchi yetu, nimeshavua glavu na sasa kila kitu kitaanikwa hadharani,” akasema kwenye televisheni na baadaye kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na washabiki wake wengi.
Huyu ni mwanamichezo na mwanasiasa anayetakiwa na Marekani kwa ajili ya kujibu mashitaka yake sambamba na wenzake 13 na wengine ambao huenda watakamatwa siku zijazo. Alikamatwa kisha akaachiwa kwa dhamana na polisi katika mji mkuu wa Port of Spain nchini Trinidad & Tobago wiki iliyopita.
Wakati haya yakijiri, Uingereza imeanza kupiga jaramba, wakuu wake wakisema kwamba wapo tayari kuandaa fainali za Kombe la Dunia 2022 ikiwa Qatar watapokonywa fursa hiyo, kwani wanahusishwa na utoaji mlungula ili kupewa uenyeji.
Urusi ndio waandaaji wa michuano ya 2018 na wamekuwa wakipinga kitendo cha Marekani kuchukua hatamu za uchunguzi wa hali ya Fifa, lakini Marekani wanasonga mbele na kazi hiyo.
Waziri wa Utamaduni wa Uingereza, John Whittingdale ndiye amenukuliwa akisema kwamba England wapo tayari kuwa wenyeji kwa mwaka huo, huku akisema kwamba kuna hoja nzito pia za kuangalia upya uenyeji wa 2018.
Ushahidi wa aina yake umeanikwa nchini Marekani na ofisa wa Fifa, Chuck Blazer ambaye amesema walikubaliana na wakuu wengine wa Fifa na kisha kupokea rushwa kiasi kikubwa kutoka kwa wadau mbalimbali, ikiwa kama ni ‘asante’ kwa kupewa ama uenyeji au kitu kingine.
Polisi wa Afrika Kusini nao wameanzisha uchunguzi juu ya madai kwamab Fifa waliwaomba maofisa wa taifa hilo rushwa na wao kutoa ili kupewa uenyeji wa fainali za 2010. Blazer amedai walipokea wote fedha hiyo, akiwamo Blatter, na sasa hali ya hewa imezidi kuchafuka.
Blazer anasema kwamba maofisa wa Kamati ya Utendaji ya Fifa na baadhi ya makamu rais wake walikuwa wakipokea rushwa kuanzia 2004 hadi 2011 ikiwa ni fadhila kwa kuunga mkono taifa hilo kuandaa fainali hizo, likiwa pekee Afrika lililopata kufanya hivyo.
Anasema hata Morocco walitoa fedha ili wapewe uenyeji wa fainali za 1998 lakini mambo hayakuwa, uenyeji ukaenda Ufaransa, ambapo mmoja wa wakuu wa maandalizi ya fainali hizo za Ufaransa alikuwa Michel Platini, rais wa sasa wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa) aliyekuwa akimshinikiza Blatter kuachia ngazi hata kabla ya uchaguzi wa wiki jana.
Blazer anasema yeye na wengine walipokea rushwa kubwa na kwa mara nyingi kuhusiana na haki za utangazaji wa michuano ya Kombe la Dhahabu la Concacaf miaka ya 1996, 1998, 2000, 2002 na 2003.
Tuhuma nyingine ni juu ya kusuka mipango ya kukwepa kodi nchini Marekani, taifa linalofuatilia kwa karibu haki ya serikali yake kulipwa kodi, tofauti na ilivyo kwa baadhi ya nchi ndogo na visiwa vya Ulaya kama Uswisi.