MABINGWA wa soka barani Afrika na klabu bora ya karneΒ Β Al Ahly imetangaza rasmi kumsajili winga machachari Luis Miquissone kutoka kwa mabingwa wa soka nchini Tanzania. Al Ahly imefanya hivyo wakati ikimtangaza nyota wao mwingine Percy Tau kutoka Brighton ya England. Usajili wa Luis Miquissone umekuwa maarufu barani Afrika kutokana na hadhi ya klabu hiyo.
TANZANIASPORTS inakuleta masuala muhimu ambayo unapaswa kuyajua katika dili la usajili huo, ambapo Luis Miquissone anaungana na kocha bora na mwenye rekodi za aina yake barani Afrika, Pitso Mosimane. Kocha huyo amewahi kuwafundisha wachezaji hao wawili wakati walipokuwa wakicheza chini yake katika Ligi Kuu Afrika kusini maarufu kama PSL (Premier Soccer League).
Yafuatayo ni masuala muhimu ambao unatakiwa kufahamu kuhusu uhamisho wa Luis Miquissone kwenda Al Ahly.
MIQUISSONE WA KWANZA SIMBA
Usajili wa Luis Miquissone kwa dola 900,000 anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka klabu ya Simba kusajiliwa moja kwa moja na mabingwa wenzao Al Ahly. Ikumbukwe Luis Miquissone ndiye aliyewapiga bao Al Ahly ndani ya dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika. Bao lake lilikuwa matata mno ambalo golikipa wa Al Ahly alishindwa kufanya miujiza ya kuokoa mchomo huo.
Hata baada ya kutwa taji la Ligi ya mabingwa Afrika, kocha Pitso Mosimane alikiri mchezo wao na Simba jijini Dar es salaam ulikuwa mgumu mno katika mbio za kusaka taji hilo. Katika historia ya Simba hawajawahi kuuza mchezaji moja kwa moja kwenda Al Ahly.
MIQUISSONE WA KWANZA LIGI KUU TANZANIA
Unaweza kusema kiungo Himid Mao ni staa aliyesajiliwa na ENNPI ya Misri akitokea klabu ya mabwanyenye wa Azam fc wa jijini Dar es salaam inayoshiriki Ligi Kuu, lakini katika historia ya Ligi Kuu Tanzania hakuna mchezaji aliyesajiliwa na Al Ahly moja kwa moja. Hii ina maana kwa mara ya kwanza mabingwa kihistoria Al Ahly wametia mguu katika Ligi Kuu Tanzania na kunyakua kipaji kilichokuwepo katika klabu ya Simba.
MCHEZAJI WA KWANZA KUTOKA MSUMBIJI
Luis Miquissone ameweka rekodi mbili hapa; kwanza kuwa mchezaji wa kwanza raia wa Msumbiji kununuliwa na klabu ya Al Ahly akitokea Simba, lakini pia ni mchezaji wa kwanza wa Msumbiji kuchezea Al Ahly. Hata hivyo historia inaonesha kuwa Luis Miquissone sio mchezaji wa kwanza kucheza Ligi Kuu Misri.
Usichanganye msomaji, kuna mchezaji wa kwanza kutoka Msumbiji kusajiliwa Al Ahly na wachezaji wengine kucheza Ligi Kuu Misri. Twende sawa sasa, wachezaji raia wa Msumbiji waliowahi kuchezea klabu za Ligi Kuu Misri ni pamoja na Celso Halilo de Abdul au maarufu kwa jina la Mano.
Staa huyo alicheza katika klabu ya El Gournah mnamo mwaka 2006 hadi mwaka 2014. Mnamo mwaka 2014 hadi 2016 akajiunga na klabu ya ENPPI na baadaye mwaka 2016 akarejea klabu aliyoanzia El Gounah. Baada ya kuachana na El Gounah mwaka 2016 alirejea nchini kwao Msumbiji.
Mchezaji wa pili wa Msumbiji kucheza Ligi Kuu Misri ni beki Dario Ivan Khan mwaka 2009 alipojiunga na klabu ya Ismailia akitokea klabu ya Al Hilal ya Sudan. Dario alidumu Ismailia hadi mwaka 2011 kisha akaondoka kwenda Qatar.
Golikipa Rafael na mshambuliaji Danilo Manhonga βMbinhoβ alichezea klabu za Mahalla el kubra na Smouha zote za Ligi Kuu Misri.
MIQUISSONE WA PILI SIMBA
Simba imeuza wachezaji wengi kuanzia Ligi ya Afrika kusini, Jamhuri ya Kongo na sasa Ligi Kuu Misri. Simba imemuuza nyota wake mwingine Cletous Chotta Chama kwenda klabu ya Berkane sambamba na winga wa Yanga Tuisila Kisinda ambo wameungana na kocha Ibenge aliyehamia klabu hiyo akitokea AS Vita na timu ya taifa ya Kongo. Luis Miquissone anakuwa staa wa pili kuondoka Simba kwa kuuzwa msimu huu baada ya Chama.
Comments
Loading…