HIVI karibuni Rais wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania, TFF Wallace Karia alibainisha umuhimu wa kuimarisha mashindano ya Ligi Kuu ya wanaume, wanawake na timu za Taifa. Kwenye mahojiano na Kituo cha Taifa cha Televisheni Wallace Karia alisema ni muhimu kuifanya Ligi Kuu iwe imechangamka na kusisitiza kuwa klabu zinatakiwa kuimarisha vitengo vyake vya fedha ili kuzikomboa zaidi. TANZANIASPORTS katika uchambuzi wake pamoja na mambo mengine imeibua mambo kadhaa muhimu ambayo yanawezesha kuimarisha Ligi Kuu Tanzania.
Viwanja vyenye hadhi na usalama
Thamani ya Ligi Kuu inapopamba maana yake miundombinu yake nayo inapaswa kuimarishwa. Mara tumeshuhudia TFF ikifungia viwanja mbalimbali kutokana na hali duni. Viwnaja vingi vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi, bila shaka kwa kushirikiana na serikali wanapaswa kuhakikisha viwanja vyetu vinavyotumika Ligi Kuu vinakuwa katika hadhi nzuri. Ligi yetu inafuatiliwa na wengi na hivyo inapaswa kuw ana hadhi kwenye viwanja vyake, majukwaa na sehemu za kuchezea (pitch). Hili ni jambo ambalo wadau wanaweza kulifanyia kazi kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanja kama ambavyo bilionea Said Bakhressa alivyofanya kwenye uwanja wa Azam Complex. Katika baadhi ya viwanja barani Ulaya vinamilikiwa na masnipaa au majiji na kuvikodisha kwa vilabu mbalimbali. Kwahiyo serikali kwa kushirikiana na wadau au wadau wenyewe wanaweza kuwekeza kwenye viwanja na kuhakikisha wanaviweka katika mazingira mazuri ya kuoneshwa kwenye televisheni huku viwanja viking’arisha ubora wa maeneo ya kuchezea na thamani ya Ligi. Kila mtaalamu wa mpira iwe kocha,utawala au wachezaji wanapendelea kucheza katika viwanja vizuri.
Ongezeko la wadhamini
Ukiangalia namna timu za Ligi Kuu zinavyonunua wachezaji wa kigeni utaelewa kuwa mazingira yetu kisoka yamebadilika na kuvutia wengi. Uwezo wa timu zetu kugharamia mishahara na malipo mengine ya wachezaji na makocha ni jambo muhimu. Kwahiyo kuna haja ya kufanya hamasa kubwa zaidi na endelevu kuwavutia wadhamini kuiona Ligi Kuu kama jukwaa muhimu la kutangaza bidhaa zao. Kuna kila sababu za wadhamini kuongezeka katika Ligi Kuu.
Jambo hili linapaswa kufanywa na vitengo vya masoko kwa kushirikiana na TFF pamoja na serikali. Serikali pia inaweza kushawishi au kuwaita mabilionea wa Tanzania kuzungumzia suala la uwekezaji katika michezo. Ifahamike michezo ni sehemu ambayo mapato yao yaongezeka kwa sababu ya kutangazika, kupata wateja wapya na washirika wapya. Pia wadhamini wapya watakuwa na nafasi ya kujitangaza kupitia wachezaji wa kigeni endapo kila klabu itakuwa na mikakati na mipango ya kuendesha kampeni maalumu kwa ajili ya kuwezesha.
Hamasa ya kuvutia w adhamini inapaswa kufanywa kwa ushirikiano na kikosi maalumu kinatakiwa kuandaliwa kwa pamoja TFF,Baraza la Michezo,Wizara yenye dhamana ya michezo. Wadhamini wanatakiwa kutafutwa na kuongezeka pamoja na kushawishiwa na kuwajengea uwezo juu ya umuhimu wao katika michezo pamoja na namna wanavyoweza kuvuna faida michezoni. Njia hii pia itasaidia kuinua uwezo wa vitengo vya fedha katika kuendesha vilabu vyetu.
Wachezaji na makocha wa kigeni
Katika kuimarisha Ligi Kuu ni muhimu kuangalia eneo la makocha wanaokuja kuajiriwa katika vilabu vya Tanzania. Kama ambavyo Rais TFF amebainisha suala la ada za makocha wa kigeni kuongezeka ni lazima tukiri kuwa makocha wenye sifa wapo wengi, lililo muhimu ni kuhakikisha kuwa mipango ya kuifanya Ligi yetu inakuwa imara na yenye kuendeleza hadhi ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na wtaalamu wanaoeleweka.
TFF isiishie kwenye suala la makocha pekee bali wanatakiwa pia kuangalia eneo la utawala kama linao watu wenye sifa zinazotakiwa. Mpira wa miguu ni sayansi ambayo kila mmoja angependa kuona mtaalamu anaonesha umahiri wake. Muhimu kuelewa wataalamu hawa wawe na vigezo vinavyoridhiwa na TFF pamoja na wizara ya michezo kuwa wanakidhi kutoa ujuzi hapa kwetu,. Njia hii itapunguza makocha uchwara ambao hawana sifa au wanatafuta namna ya kuanza kuandika sifa zao kupitia Ligi Kuu. Hadhi ya makocha na wataalamu inapaswa kuangaliwa pia.
Umri wa wachezaji wa kigeni
Hali kadhalika, matamanio yangu ni kuona hata suala la umri wa wachezaji linazingatiwa. Kwamba ni muhimu kuangalia kama inawezekana kuwa na wachezaji wazuri kutoka nje ya nchi ambao hawazidi umri wa miaka 30. Kwamba TFF na vilabu wanapaswa kujadiliana kuwa mchezaji wa kigeni anayekuja nchi lazima awe chini ya miaka 28 na isiyozidi 30.
Kufanya hivyo itasaidia kuwapa wachezaji wakiwa na ari ya ushindi na mafanikio kuliko kusajili wale waliochoka kiasi cha kushindwa kuchangamsha au kuleta kipya katika soka. Kwa mfano mchezaji mwenye umri zaidi ya 30 anapaswa kuwa na uzoefu wa kucheza hapa nchini si chini ya misimu miwili (miaka miwili). Wachezaji wengine chini ya miaka 28 wanaweza kuleta tija zaidi kwa wachezaji wazawa kwani wanaleta ushindani wa kweli na kuhakikisha wanashindana kwa mwendelezo na itaondoa hali ya kupotezewa muda kwa baadhi ya vilabu kwani vinakuwa vimesajili garasa.
Programu za makocha
TFF kwa kushirikiana na wanachama wake inaweza kuandaa utaratibu wa makocha wa kigeni wa vilabu kutoa mafunzo ya ndani ya mkoa zinakotoka klabu. Kwa mfano kama timu inatokea mkoa wa Dodoma na ina kocha wa kigeni, basi TFF kwa kushirikiana mzuri inaweza kuangalia namna ya kuandaa warsha kati ya kocha wa kigeni anayefunza timu hiyo na kuwasaidia kielimu makocha wazawa wa mkoa husika ambao wanakuwa wamesajiliwa na shirikisho hilo. Kwamba kocha wa Yanga, Simba, Azam wanaweza kutoa mafunzo kwa makocha wa Dar Es Salaam kwa ngazi ya Manispaa za Ilala,Temeke,Ubungo na Kinondoni. Kwahiyo hawa wanaweza kutoa mchango kuanzia ngazi za chini huku makocha hao wazawa wakilipa ada kidogo kuchangia warsha hizo.
Comments
Loading…