in , , ,

MAMBO KUMI YANAYOISIBU MANCHESTER UNITED

Manchester United imekuwa timu ya kawaida kwa sasa, haiogopeshi tena kama kipindi kile. Kipindi ambacho kila ukiona taya la Sir Alex Ferguson unaona ushindi ndani yake.

Ndicho kipindi ambacho timu ilikuwa inapigana mpaka dakika za mwisho, haikuruhusu neno kupoteza mchezo liwepo katika akili yao.

Kwao wao kushinda mechi ilikuwa utamaduni wao na kikubwa zaidi wakaweka desturi ya kushinda vikombe. Ilikuwa sehemu ya vikombe. Timu ilishinda kila kitu tena ikiwa kwenye hali ya kupigana sana.

Kitu hiki kilianza kupoteza baada ya David Moyes kupewa timu, huyu alianza kubadilisha muonekano wa timu ya Manchester United. Ukawaida ulianzia hapa. Inawezekana Luis Van Gaal alikuwa na nafasi kubwa sana ya kuibadilisha Manchester United na kuwa timu yenye ushindani.

Sema muda hakumruhusu, kipindi ambacho yeye anawaza kupata muda wa kutengeneza timu yenye ushindani ndicho kipindi ambacho wenye timu walikuwa na uhitaji mkubwa sana wa kubeba makombe.

Walihitaji makombe, walihitaji kocha mshindi. Ndiyo maana macho yao yaliangukia kwa Jose Mourinho. Kocha ambaye ashaionesha dunia kuwa yeye ni mshindi.

Alishinda vikombe akiwa FC Porto tena kwenye kikosi chenye bajeti ndogo sana. Akaja kuambukiza ushindi wa vikombe katika timu ya Chelsea. Akawapa vikombe viwili vya ligi kuu ndani ya misimu miwili.

Hata alipoenda Intermillan alifanikiwa kuendeleza tamaduni yake ya kubeba vikombe. Tamaduni ambayo ilikuwepo kwenye timu ya Manchester United na inaonekana kupotea kadri siku zinavyozidi kwenda.

Sawa alifanikiwa kuipa Manchester United vikombe vitatu, lakini kwa muda huu hakuna dalili yoyote inayoonesha kuwa anauwezo wa kufanya tena makubwa ndani ya timu ya Manchester United.

Tatizo ni nini? Kipi kinaisibu Manchester United kwa sasa?

1: Kutokuwa na mwendelezo mzuri wa matokeo chanya. Msimu huu Manchester United imecheza michezo 9, ambapo amefanikiwa kushinda mechi nne (4) , akapoteza mechi tatu na kutoka sare mechi moja.

Hata katika uwanja wao wa nyumbani wamekuwa na matokeo mabovu, mpaka sasa wameshindwa kushinda mechi tatu (3) mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani tangu mwaka 2015.

Hii ina madhara gani ndani ya timu? , kutokuwa na mwendelezo mzuri wa matokeo chanya ndani ya timu kunawafanya wachezaji wapunguze kujiamini na presha kubwa inakuwa ndani yao kila wanapokuwa wanaingia ndani ya uwanja.

Unapokuwa na presha kubwa unakuwa na uwezekano mkubwa wa kufanya makosa mengi binafsi ndani ya uwanja.

2: Jose Mourinho alikuwa sahihi kutaka kusajili beki wa kati kwenye dirisha la usajili?

Hapana shaka, ni eneo ambalo kwanza limekuwa na halina wachezaji ambao wamejimirikisha eneo hili. Leo atacheza Smalling na Baily kesho atacheza Smalling na Jones. Na hii ni kwa sababu ya majeraha ya baadhi ya wachezaji wa eneo hili. Majeraha ambayo huwafanya viwango vyao kuwa vya kupanda na kushuka. Mpaka sasa wameruhusu magoli 11 katika michezo Tisa, wastani wa kuruhusu goli 1.5 kwenye kila mechi.

Timu ikiwa na wastani wa kuruhusu goli kila mechi inakuwa imejitoa taratibu kwenye tabia ya kuwa timu bingwa, siku zote bingwa huwa na safu imara ya ulinzi.

3: Lukaku ? , anafaa kusimama kama mshambuliaji wa mwisho wa Manchester United?. Kuna kitu kimoja hapa kabla sijajibu swali hili. Ukiangalia takwimu za Lukaku zinatia moyo sana,mpaka sasa amefunga magoli manne kwenye mashindano yote.

Magoli manne ambapo timu imecheza mechi tisa tu, ni kitu ambacho kinavutia sana!, lakini tatizo moja kwa Lukaku ni moja tu. Lukaku siyo Clinical Finisher. Lukaku anapata nafasi nyingi sana lakini magoli anayofunga hayalingani na nafasi ambazo anazipata.

Manchester United inatakiwa kuwa na mshambuliaji wa daraja la juu. Mshambuliaji ambaye atakuwa na uwezo wa kubadilisha nafasi nyingi anazopata kuwa magoli.

4: Sanchez bado anasubiriwa lakini yeye hataki kabisa kuja. Alikuja na matumaini makubwa sana ndani ya mioyo ya mashabiki wa Manchester United lakini mpaka sasa hajafikiwa kufanya kitu kikubwa ambacho alikifanya Arsenal.

Hii inaiathiri vipi timu? Kipindi ambacho Lukaku hatumii vizuri nafasi anazopata kulihitajika msaidizi ambaye angetumika kama mtu wa ziada kuibeba timu kipindi kigumu. Hii kazi Sanchez alikuwa anaiweza kipindi yupo Arsenal, lakini kwa bahati mbaya kamba za viatu vyake amevisahau Arsenal kiatu chake kinalegea sana kwa sasa!.

5: Pogba Vs Jose Mourinho. Hii ni vita mpya ndani ya kikosi cha Manchester United. Vita ambavyo siyo siri tena , iko wazi na kibaya zaidi inaharibu mpaka hali ya hewa katika vyumba vya kubadilisha nguo katika timu ya Manchester United. Unapokosa maelewano mazuri kwenye vyumba vya kubadilisha nguo unakuwa na nafasi finyu sana kwa timu yako kuwa na maelewano ndani ya uwanja.

6: Wakati anaipa Chelsea ubingwa wa ligi kuu Mara mbili mfululizo, tulitegemea Jose Mourinho anaweza kukaa kwa muda mrefu ndani ya kikosi cha Chelsea lakini msimu wake wa tatu ukawa msimu wa mwisho kukaa pale darajani.

Alikaa kwa amani Realmadrid misimu miwili ya mwanzo lakini msimu wa tatu ukawa msimu ambao aligombana na baadhi ya wachezaji nyota kama golikipa Iker, Cristiano Ronaldo, Pepe , Sergio Ramos. Kitu ambacho kilipoteza sauti ndani ya vyumba vya kubadilisha nguo.

Hata aliporudi tena Chelsea msimu wake wa tatu ukawa msimu wake wa mwisho kama ilivyokuwa kwa Realmadrid. Aligombana na kina Hazard mwisho wa siku akaondoka. Hili limeanza kuonekana tena katika msimu wa tatu ndani ya Manchester United. Ashapishana na Martial, Pogba.

7: Kuibuka kwa wapinzani kama Manchester City kumekuwa na nafasi kubwa sana kwa anguko la Manchester United.

8: Kutoka kwa David Gill mpaka kuja kwa Edward Woodward kulikuwa na mabadiliko makubwa ambayo yalichangia kwa kiasi kikubwa kwa Manchester United kuporomoka ndani ya uwanja.

Kwanini? Kipindi Sir . Alex Ferguson anafanya kazi na David Gill asilimia kubwa akili zao zilikuwa zinawaza maendelo ndani ya uwanja. Lakini Edward Woodward amekuwa akifikiria namna ambavyo timu itatengeneza pesa kwa muda nyingi.

9: Hawana Director Of Football, hii inaweza kuwa moja ya sababu ya Manchester United kuporomoka?

Hapana shaka hili suala lina nafasi kubwa sana katika kiwango cha sasa cha Manchester United kwa sababu sajili ambazo zinafanyika katika timu ya Manchester United ni sajili za kibiashara zaidi ndiyo maana huwa zinakuwa hazina manufaa makubwa ndani ya uwanja. Kungekuwepo na Director Of Football kungekuwepo na uwezekano wa Manchester United kusajili wachezaji ambao wanafaida kubwa sana ndani ya uwanja kuliko kibiashara.

10: Manchester United kwa sasa haina viongozi ndani ya uwanja kwa wingi kama kipindi cha nyuma. Kuna kipindi aliwahi kuwepo Cantona, akawepo Keane, Rooney, Gary Neville, Vidic, Evra, Ferdinand, Giggs ambao kuna kipindi waliwahi kucheza kwa pamoja. Tofauti na sasa hakuna idadi kubwa ya viongozi ndani ya uwanja na kwenye vyumba vya kubadilisha nguo.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

JONAS MKUDE, HADITHI AMBAYO TULIKUWA TUKIITAMANI

Tanzania Sports

BEGI LA ROSTAND LILIFICHA KITABU CHA KAKOLANYA