Menu
in , , ,

Mambo 10 ya kubadilishwa Manchester United

Tanzania Sports

Man Utd squad

SIKU chache zilizopita tumeshuhudia matokeo mabaya ya mabingwa wa zamani wa EPL, Manachester United. Timu hiyo ipo chini ya kocha Ruben Amorim, na kwa kuzingatia muktadha wake TANZANIASPORTS ilifanya uchambuzi juu ya utamaduni wa klabu ya Manchester United linapofika suala la kufukuza wakufunzi wao. Katika makala hayo nilieleza kuwa Manchester United inaendeshwa katika taratibu za aina yake ikiwemo uvumilivu kwa makocha. Huo ni utamaduni wao, hata pale timu inapofanya vibaya kocha anavumiliwa na uamuzi wa kumfuta kazi unachukua muda mrefu kuliko kawaida. 

Sasa TANZANIASPORTS inaendelea kuchambua kwa kina kuhusiana na mwenendo wa Manchester United, ambapo yapo mambo 10 ambayo yanatakiwa kubadilishwa. Katika mambo hayo 10 mengi yanahusiana na utendaji wa kazi ndani ya uwanja, kuliko siasa za nje ya uwanja. Ni jukumu la Ruben Amorim kubadilisha hali ya mambo.

Kumweka benchi Bruno Fernandez

Huenda unaweza kudhani tathmini ya TANZANIASPORTS imechelewa lakini tangu awali alipopokea timu hiyo kutoka kwa Eric Ten Hag tumekuwa tukichunguza utendaji wa kazi wa kiungo huyu raia wa Ureno. Bruno Fernandes hatakiwi kuchezeshwa kwenye eneo la kiungo ili kuinusuru timu hiyo. Je ni wakati fani Bruno anaisaidia timu? Jibu ni pale alipofika bao, kupiga faulo au kona, lakini mengine yamekuwa nje ya uchezaji. Mfano anapotakiwa kucheza eneo la kiungo cha mbele akiwa nyuma ya mshambuliaji au washambuliaji wawili mara nyingi anategemewa kuanza kuzuia wapinzani kwa juu (high pressing) lakini kiungu huyo amekuwa si wa kuifanya kazi hii. Lipofika suala la kiungo mwenye uwezo wa kupenya ngome ya adui, huyu si mchezaji sahihi kumtumia wala kumtegemea. Uwiano wake wa kushambulia na kusaidia ulinzi havinanni kwa sababu mchango wake si ule unaokuja kwa ukubwa. Si nyuma ya washambuliaji, wala eneo la kiungo mshambuliaji ambalo linachezwa kwa ufanisi na mreno huyu. Nafasi ambayo anatakiwa kuitumikia ni pale kocha anapotakiwa kumpanga kama nambari 10 akimsaidia Sesko kwenye eneo la ushambuliaji kwani nyuma yake atahitaji viungo wa ulinzi wawili.

Hofu ya kumtoa nje ya uwanja nyota wake

Kocha Ruben Amorim amekuwa mwoga kumtoa Bruno Fernandes kama ilivyokuwa kwa Eric Ten Hag. Mara nyingi amekuwa akipangwa kikosi cha kwanza na kwa vile ni nahodha lakini ameshindwa kuitendea kazi nafasi yake. Ruben ameonesha wasiwasi au hofu ya kumtoa nje nahodha wake ama kumtaka aongeze bidii katika uchezaji. Katika mahojiano fulani amewahi kusema kuwa Kobi Mainoo anapigania namba na Bruno Fernandez, lakini ukweli ni kwamba mreno huyo amekuwa kimbeba mwenzake. 

Kwa maana hiyo hata pale Kobi Mainoo anapoingia uwanjani anaonekana kutokuwa na furaha na uchezaji wake umekuwa nje ya nafasi. Mara nyingi Kobi Mainoo anacheza kivyake (out of position) au kurudi nyuma zaidi kama kiungo wa ulinzi. Kobi Mainoo anamzidi Bruno kwenye uwezo wa kuipangua ngome ya adui. Kobi ana chenga na nguvu pamoja namaarifa makubwa ya kupenya ngome za wapinzani. Tofauti na Bruno ambaye hutegemea upigaji wa pasi kwa mtu kwa mtu kuelekea lango la adui, kwa maana hawezi kutoa kitu cha zaida ambacho anacho mwenzake.

Golikipa asiye na kiwango

Hili ni tatizo ambalo Ruben Amorim amelitengeneza kwa mikono yake. golikipa wake Bayindir hana kiwango cha kuichezea Manchester United. Pengine Bayindir ni golikipa wa kudakia timu kama Fulham, Stoke City na nyinginezo zilizoko kwenye Ligi daraja la kwanza sio Ligi Kuu. Uwezo wa golikipa huyo ni mdogo; kufanya maamuzi, kutumia miguu yake, kasi na uanzilishi wa mashambulizi ni mdogo mno. Huyu ni golikipa ambaye ahawezi kuiletea mafanikio klabu kama Manchester United.

Kumpa nafasi Kobi Mainoo

Kama nilivyoeleza mwanzoni kuhusiana na uwezo wa Kobi Mainoo na Bruno, ni kwamba tofauti hizo zinampa nafasi kubwa ya kinda Kobi kucheza kikosi cha kwanza huku akiendelezwa kuliko kumtegemea Bruno. Kobi anaweza kumpa kocha kitu cha ziada pale anapokuwa nje ya 18; kwanza anweza kupiga mashuti makali, anaweza kupiga pasi mpenyezo nyingi sana kwa sababu anajua chenga na kupangua adui. Pia Kobi anao ujuzi wa kusababisha madhara katika eneo la adui kuliko Bruno. Kwahiyo kocha Ruben Amorim anatakiwa kutafuta namna ya kumjumuisha kinda huyo kwenye mfumo wake ili acheze nafasi ya kiungo. Kobi alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Gareth Southgate katika timu ya Taifa. Kabla ya kuichezea England, kulikuwa na vita kali na Ghana ambao walitaka kumtumia kinda huyo. Uwekezaji uliofanywa kwa Mainoo ni mkubwa na anacho kipaji kinachovutia zaidi kikosini hapo. Hivyo ni mchezaji anayetakiwa kuingizwa kwenye mfumo wa Amorim kuliko kumkalisha benchi huku anayepangwa mchango wake ni hafifu.

Kukosa beki wa kati wa kuaminika 

Harry Manguire, De Ligt na Leny Yoro ni mabeki wa kati wa Manchester United. Lakini katika upangaji wa kikosi wa Amorim anaonekana kukosa kombinenga ya mabeki wa kati. Beki ambaye angalau amecheza mfululizo ni De Ligt, lakini Leny Yoro na Harry Manguire wamekuwa wakibadilishwa badilishwa mara kwa mara. Katika mazingira hayo, hakuna beki mwenye uhakika katika kikosi cha Man United, hali ambayo inawavuruga wachezaji wenyewe. Kila mara beki mmojawapo anapotolewa huwa wanaonesha bayana kutofurahishwa na uamuzi wa kocha wao, lakini w anamheshimu. Ruben Amorim ametengeneza tatizo hili kwa mikono yake na kusababisha safu ya ulinzi isiwe na mwenyewe na uwajibikaji haueleweki ni mtindo gani. Kila mechi wanapangwa tofauti na hivyo wanashindwa kufahamiana. Mfano Rio Ferdinand na Nemanja Vidic ilikuwa panga au pangu lazima uwakute kwenye kikosi cha kwanza na walizoeana kiasi kwamba ni miongoni mwa mabeki bora kushuhudiwa Manchester United.

Kumweka benchi Luke Shaw

Msimu huu Luke Shaw anaonekana kupata nafasi akishirikiana na Dorgu. Luke Shaw anapewa nafasi kama beki wa kushoto, huku Dorgu akipangwa winga wa kushoto mwenye jukumu la kumsaidia beki wake. hata hivyo Dorgu si winga teleza wa kushoto bali jukumu lake kuu ni ulinzi. Mara kadhaa amechachafya ngome ya timu pinzani, lakini hachezi kwa na kuonesha kipaji chake kilichosababisha mabosi wa Man United waingie sokoni kumsajili. Bahati mbaya tangu apngawe  kama winga wa kushoto amekuwa akiyumba na huenda naye akaanza kuelemewa na shetani llinalowaandama klabu hiyo. Suluhisho ni kumweka benchi Luke Shaw na kumpa majukumu Dorgu kama ilivyokuwa awali. Luke Shaw hana spidi, hagombanii mipira ya juu, ufanisi wake kushambulia si mkubwa na hivyo anasababisha timu iwe inayumba mbele na nyuma.

Kikosi cha kwanza cha kueleweka

Mchezaji kucheza mechi mbili vizuri lakini ya tatu anawekwa benchi inasababisha msongo wa mawazo. Wachezaji wanapochezeshwa mfululizo ndipo wanaweza kutengeneza kombinenga. Hali hiyo inasaidia wao kuwaelewa wenzao na kutengeneza mbinu nzuri za kusaidia timu. Lakini kila mchezo kikosi cha kwanza kinabadilika na hakuna mwenye uhakika. Wachezaji wakiishi mazingira ya namna hii maana yake hawana uhakika na utendaji wao wa kazi na kusababisha hofu isiyo na sababu. Kukosa mwendelezo wa kuwa na kikosi cha kwanza ni adui anayemtafuna Ruben Amorim.

Kukosa mchezaji wa tegemeo

Katika kikosi cha Man Unitd hakuna mchezaji ambaye anaweza kuonekana ni tegemeo. Huyu ni mchezaji ambaye anaaminika kuipa timu pointi au mafanikio pale inapojikuta katika wakati mgumu. Mara nyingi timu inamzunguka mchezaji huyo na kutengeneza nafasi au kila mbinu kuhakikisha anabeba majukumu ya timu nzima. Lakini si suala la mfumo tu hamna wakati ambao kocha huyo ameonesha angalau kumweka mchezaji fulani kuwa tegemeo. Amad Diallo alianza vizuri, lakini kila mara timu inafumuliwa na kushindwa kumsaidia kuwa nyota wa timu. Mara nyingine anawekwa benchi na hivyo kusababisha timu ikose mchezaji wa kumtegemea. Kifupi hakuna nyota tegemeo mwenye kubeba timu katika mabega yake.

Mabadiliko yasiyo na tija

Mara kwa mara kocha Amorim amekuwa akifanya mabadiliko kwa kile kinachoitwa kwa maslahi ya timu. Lakini mabadiliko yake mara kwa mara hayana msaada wala kuleta manufaa. Timu inakuwa ileile, hakuna njia zinazoweza kutumika kubadilisha hali ya mambo. Mfano dhidi ya Brendford walichapwa mabao 3-0 na kuifanya timu hiyo kuwa nyanya kabisa. Wachezaji hawakuwa wale ambao unaweza kuchagua mmoja wa kuibeba timu na hivyo kocha anatumia kila njia kuhakikisha inamtegemea yeye ikiwemo mabadiliko ya kumwongezea faida. Lakini hata mabadiliko yanapofanyika hakuna kitu kinachoonekana kubadilika.

Kuwatumia Mbeumo na Amad

Nyoata hawa wawili wanaweza kucheza kwenye mfumo wa Ruben Amorim, lakini wanachezeshwa nyakati mbili tofauti. Kama Luke Shaw angewekwa benchi kisha Dorgu akapewa nafasi ya kucheza beki wa kushoto basi winga wa upande huo angekuwa Mbeumo au Amad Diallo. Angalau mawinga hawa wangeweza kumsaidia kocha huyo, isivyo bahati Amad anaanzia benchi huku Mbeumo akipangwa kikosi cha kwanz ahadi mwisho. Lakini mafanikio yake huwa haba sana na hivyo kusababisha upande wa winga wa kushoto wa Man United kuwa dhaifu mno. Ni wakati wa kocha Ruben Amorim kuangalia namna bora ya kuipanga timu yake.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version