Rais mpya wa shirikisho la soka nchini Jamal Malinzi ana mpango wa kuhamisha ofisi za TFF kutoka kwenye Uwanja wa Karume, jijini, ili eneo hilo lijengwe kitega uchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza kama rais wa TFF tangu achaguliwe Jumapili iliyopita, Malinzi alisema katika kuimarisha uwezo wa kifedha wa shirikisho amepanga kuamisha ofisi ili kutoa nafasi ya uwekezaji kwenye eneo la sasa la ofisi hizo.
“Najua kwa kanuni na sheria huwezi kuhamisha ofisi za shirikisho au Chama kilichosajiliwa kisheria bila ya maamuzi ya kamati ya Utendaji,” alisema Malinzi. “(Lakini) Nitalipeleka hili jambo kwa kamati ya utendaji na naamini litaungwa mkono ili ofisi zihame hapa (Karume) na kutafuta sehemu nyingine ili kutoa nafasi ya uwekezaji ambao unalenga kuliongezea kipato shirikisho.
” Pia alisema katika uongozi wake TFF itaimarisha kitengo cha masoko kwa ajili ya kufanikisha kupata udhamini kwa ajili ya timu zaidi za taifa. Mpaka sasa ni Taifa Stars tu ndiyo yenye udhamini kutoka kampuni ya bia ya TBL ambayo ilichukua jukumu lililokuwa likitekelezwa awali na SBL kuanzia mwaka 2006 huku timu za vijana na wanawake zikiwa kama yatima.
Wakati huo huo, rais wa shirikisho la soka (TFF) Jamal Malinzi amesema kuanzia mwakani kutakuwa na mashindano ya taifa ya vijana ya U-12 ya kila mwaka ambapo watakuwa wakiongeza umri wa wachezaji kwa mwaka mmoja. “Hii itatusaidia kujenga misingi ya wachezaji bora kwa ajili ya vilabu na timu za taifa,” alisema na kueleza zaidi kuwa lengo la kuongeza mwaka mmoja katika umri kila mwaka ni ili kufika mahali ambapo “tutakuwa na mashindano ya taifa kwa wachezaji wenye umri wa miaka 18.”
Comments
Loading…