Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Afrika Kusini (SAFA) Dr.Danny Jordan kufuatia kifo cha nguli aliyewahi kuichezea timu ya Taifa ya nchi hiyo (BafanaBafana) John Lesiba “Shoe” Mashoeu kilichotokea jana Aprili 21.
Katika salamau zake kwa Dr. Jordan, Malinzi amesema nchi ya Afrika Kusini imepatwa na pigo kubwa katika tasnia ya mpira wa miguu, kufuatia kifo cha Mashoeu aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa Kansa ya Utumbo, na kusema watanzania wako nao pamoja katika kipindi hiki cha maombelezo.
John Lesiba “Shoe” Mashoeu aliyezaliwa Disemba 18, 1965 nchini Afrika Kusini, alikuwa ni miongoni wa wachezaji wa nchi hiyo waliotwaa Ubingwa wa Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) mwaka 1996 nchini Afrika Kusini na baadae kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Ufaransa mwaka 1998.
Wakati wa uhai wake Mashoe alipata kuvichezea vilabu vya Giant Blackpool, Kaizer Chiefs, Amazulu na Alexandria United vya Afrika Kusini, na timu Gencleribirligi, Kocaeilispor, Fenerbahce na Busrsapor za Uturuki.
MASHINDANO YA COSAFA
Baraza la Vyama vya Soka kwa nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA) limepanga kuyaandaa na kuyatangaza mashidano hayo yatakayofanyika mwezi Mei mwaka huu nchini Afrika Kusini kwa mafanikio makubwa.
TFF inawaomba waandishi wa habari wanaotaka kupata habari kuhusu mashindano hayo, watume mawasiliano yao kwa Afisa Habari wa TFF.
Mawasiliano hayo ni: Jina Kamili, namba ya simu, barua pepe na kituo unachofanyia kazi.
Taarifa hizo zitumwe kwa njia ya barua pepe kabla ya siku ya ijumaa kumalizika, ili ziweze kutumwa kwenye kitengo cha habari cha COSAFA.
NB: Kesho Alhamis saa 5 kamili asubuhi kutakua na mkutano na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa mikutano wa TFF- Karume, waandishi wa habari mnaombwa kuhudhuria.
Comments
Loading…