*Swansea, West Brom zachekelea kukaa juu
*Brendan Rodgers, Villas-Boas bado wajiuliza
WIKI tatu za mechi na mbili za mechi za Ligi Kuu ya England (EPL) zimewachanganya kiasi washabiki wa soka.
Mapumziko ya muda ya EPL yameziacha Swansea na West Bromwich Albion zikitamba kwenye nafasi zisizo kawaida yao.
Haingekuwa rahisi washabiki kuwaza kwamba leo maeneo ya kujidai ya timu mbili hizo yangekuwa nafasi ya pili na ya tatu katika msimamo.
Wala haingeingia sana akilini kwamba Liverpool ya Brendan Rodgers iliyofanyiwa mageuzi kiasi ingekuwa kwenye eneo la zinazoshuka daraja.
Rodgers ndiye alikuwa kocha wa Swansea, aliyeitoa kwenye michuano ya Championship na kuipandisha daraja hadi EPL, ikavutia wengi kwa soka yake ya kumiliki mpira, naye Rodgers akatwaliwa na matajiri wa Kimarekani wa Liverpool.
Everton ambayo kwa kawaida huanza ligi kwa kusuasua na kushituka mwishoni mwake na kupata ushindi dhidi ya vigogo na sare za hapa na pale, nayo imeanza kivingine.
Vijana hao wa David Moyes hawapo pabaya kwenye msimamo, maana wapo katika sita bora, kama unaweza kuziita hivyo.
Zilikuwa wiki tatu za patashika nyingi, zikiwamo za kukamilisha usajili wa dakika za mwisho. Liverpool ni moja ya timu zilizojaribu kuuchangamkia usajili huo, japo wakuu wake wanalalamika hawakupata washambuliaji wa kutosha.
Sambamba Reds hao ni Tottenham Hotspur iliyosajili vyema, lakini Andre Villas-Boas anashangaa kwamba bado wamebakia nafasi ya 14 kwenye msimamo.
Si Liverpool wala Spurs waliofanikiwa kushinda mechi, huku Liverpool ikifungwa mara mbili na kutoka sare moja wakati Spurs wametoka sare mbili na kupokea kichapo mara moja.
Kwamba Chelsea wanashika nafasi ya kwanza si jambo la kushangaza, ila kwamba Fernando Torres amerejea kwenye makali yake, akijaribu kuvaa viatu vya Didier Drogba.
Torres aliwika kwenye michuano ya Euro 2012, japokuwa si wengi waliojali kuchukulia hilo kwa umakini. Hakufurahia msimu uliopita Stamford Bridge, lakini sasa katika mechi tatu kafunga mabao mawili.
Mshambuliaji mpya wa Manchester United, Robin Van Persie anaendeleza dozi za mabao, kwani katika mechi tatu tayari amezifumani nyavu mara nne, akifungana na mshambuliaji wa Swansea, Miguel Cuesta Michu katika nafasi ya kwanza.
Hao wanafuatiwa na Carlos Tevez, mwana mpotevu aliyerejeshwa kundini na kuitika mwito. Huyu ana mabao matatu aliyoifungua Manchester City ya Roberto Mancini.
Baada ya hao wanafuata wachezaji 15 wenye mabao mawili kila mmoja, kisha unakuja msururu wa wacheaji 43, kila mmoja na bao lake moja alilofunga.
Mabingwa Manchester City wamecheza taratibu, lakini wana pointi za kuridhisha, wakiwa nafasi ya nne. Hawakumwaga kitita kwenye usajili, tofauti na ilivyokuwa kawaida yao.
Kama Manchester City hawakuwa na makeke ya usajili, haina maana wengine walikaa kimya, kwani katika wale nyota wachache walio huru, alikuwapo Michael Owen.
Wapo wanaosema amebakiwa na mabao ndani mwake, hivyo alikuwa na mpango wa kufanya kila linalowezekana kudhihirisha hayo katika umri wake wa miaka 32.
Moja ya njia za kufanya hivyo ni kujiunga na Stoke City, baada ya miaka minane mizuri na Liverpool, msimu mmoja safi na Real Madrid, minne na Newcastle alikokuwa na masahibu ya majeraha.
Ni baada ya hapo Sir Alex Ferguson alimchukua Manchester United alikokaa misimu miwili bila kutumiwa sana, kabla ya kubaki mchezaji huru aliyevutwa na kocha Tony Pulis wa Stoke, na huko amemkuta mwana Liverpool mwingine, Peter Crouch.
Arsenal kuna nini? Golikipa anayevutia mchezoni, Mtaliano Vito Mannone ambaye ni namba tatu, lakini ameanza kudaka mechi mbili zilizopita.
Hii ni kwa sababu majeraha yameanza kuwaandama Washika Bunduki wa London, lakini hayajawadhuru. Mannone hajaachia bao na kwa ujumla timu haijafungwa bao lolote.
Kama unazungumzia magolikipa, Pepe Reina wa Liverpool ameanza kuonekana kuchuja, na ikiwa hatabadilika, akaendelea kucheza ataigharimu timu.
Maana unapokuwa na kigugumizi cha kufunga huku ukiruhusu mabao ya hovyo, si rahisi timu kusonga mbele. Katika umri wake wa miaka 30, bado ana umakini, lakini ni kama humpotea hivi, na Reds hawawezi kumpa muda mrefu akiutafuta.
Kwenye nafasi hiyo hiyo ya golikipa, kwa upande wa Tottenham wametaka kuonesha noti zao kwa kumchukua golikipa namba moja wa timu ya taifa ya Ufaransa, Hugo Lloris.
Huyu alitarajiwa ashike namba moja badala ya Mmarekani Brad Friedel ambaye umri unamtupa mkono.
Lakini ni Friedel aliyeonesha uwezo wa aina yake mechi iliyopita, hadi Villas-Boas akasema Lloris itabidi apiganie namba. Lloris anasemwa hajafurahishwa na kauli hiyo.
Queens Park Rangers (QPR) ni timu yenye mvuto. Kwanza ilikaribia kuitibulia ubingwa Man City mchezo wa mwisho msimu uliopita.
Lakini pia, kocha wake, Mark Hughes alipata kuchezea Man United chini ya Ferguson na baadaye akaja kuwa kocha wa Man City hadi alipofukuzwa.
Msimu huu anaweza kudhani kwamba amerejea City, maana naye alikuwa na kiburi cha kubeba kikapu cha fedha na kuingia sokoni kununua wachezaji muhimu, tena dakika za mwisho.
Kati ya wengi aliowapata ni kipa wa Kibrazili aliyekuwa Inter Milan, Julio Cesar. Wapo wanaojiuliza, Cesar kafuata nini hapo? Kichekesho ni kwamba QPR inashika nafasi ya 19 na uwiano wake wa mabao ni hasi saba.
Hughes anaweza kujitetea kwamba ndio kwanza ligi imeanza, lakini ni kweli pia kwamba hii ndiyo timu iliyoepuka kushuka daraja kwa ‘ngozi ya jino’ msimu ulipopita.
Southampton – wageni katika EPL, japo walishacheza miaka iliyopita, wanakamata mkia. Ni kwa vile ushindi katika soka ni magoli tu, vinginevyo Southampton hawangekuwa hapo.
Walicheza vizuri sana dhidi ya Manchester City na baadaye Manchester United, wakawapelekesha, tena wakaongoza kwenye mechi zote.
Hata hivyo, jamaa hao wa Manchester walikuja kusawazisha na kupachika mabao ya tatu – mechi zote mbili wakafungwa 3-2. Wigan nao waliwafunga 2-0.
Pengine wameanza na mechi ngumu mno, na bado mechi ijayo wanakabiliana na Arsenal. Yaweza kuwa wanakomazwa, lakini pia mfululizo wa kufungwa unaweza kuwaachia uchovu mbaya.
Comments
Loading…