Mwanasoka wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Luis Fernandez ameteuliwa kuwa kocha mpya wa Guinea.
Fernandez (55) amesaini mkataba wa miezi 20, wenye kipengele cha kuuongeza, Shirikisho la Soka la Guinea limesema, likiongeza kwamba atakuwa na kazi ya kuwaongoza kufuzu kwa mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2017 na Kombe la Dunia 2018.
Kocha huyu alipoteza kazi yake ya kuwafundisha Israel na miaka iliyopita amepata kuwafundisha Paris Saint-Germain (PSG) kwa vipindi viwili tofauti.
“Nitakuwa na wachezaji wa zamani Amara Simba na Kaba Diawara. Lengo langu ni kuhakikisha tunafuzu kwa AFCON 2017. Kutegemeana na matokeo huko tuendako, ndipo tutajua kitakachoendelea,” anasema Ferndadez.
Ametumia miaka kadhaa iliyopita akichambua soka nchini Ufaransa na anachukua anfasi hiyo kutoka kwa Michel Dussuyer, aliyeondoka licha ya kuwafikisha Guinea robo fainali za AFCON nchini Guinea ya Ikweta Januari mwaka huu.
Guinea wanaanza kampeni za kufuzu kwa AFCON dhidi ya Swaziland Juni mwaka huu. Hata hivyo, kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa Ebola miezi iliyopita, bado Guinea hawaruhusiwi kuwa wenyeji wa mechi, hivyo mechi za nyumbani zitachezwa uwanja huru.
Katika tukio jingine, Ethiopia wamemteua Yohannes Sahle kuwa kocha mkuu wa timu yao ya taifa, akichukua nafasi ya raia wa Ureno, Mariano Barreto aliyeondoka baada ya kushindwa kuwawezesha Ethiopia kufuzu kwa AFCON ya mwaka huu.
Sahle (49) ni mchezaji wa zamani wa Ethiopia aliyechezea timu ya taifa kuanzia zile za vijana na sasa ameaminiwa akipewa mikoba ya ukocha. Amesema amefurahishwa kuteuliwa kushika wadhifa huo, na anaona fahari kuliongoza taifa lake kisoka.
Huu ni mwendelezo kwa makocha wazalendo kupewa kazi na mataifa yao ya Afrika, baada ya Stephen Keshi wa Nigeria kuteuliwa kuwaongoza ‘Super Eagles’ kwenye hatua za kufuzu kwa michuano hiyo mikubwa miwili.
Sahle, hata hivyo, ana uraia wa Marekani pia alikoenda kuishi baada ya kumaliza muda wake wa kusakata soka. Alirejea Ethiopia 2010 na kupewa kazi ya mkurugenzi wa ufundi katika Chama cha Soka cha Ethiopia.
Baada ya hapo amepata kufundisha timu ya taifa ya vijana (U-17) kabla ya kuwafundisha Dedebit waliopata kucheza nchini Tanzania katika michuano mbalimbali na kwa sasa wapo Ligi Kuu ya Ethiopia.
Comments
Loading…