Makocha wawili wa timu za vijana wa Bolton Wanderers ya Uingereza ndio wanatarajiwa kutua nchini kesho tayari kuanza zoezi la kuwanoa wanamichezo 100 kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Frederick Mwakalebela alisema jana kuwa mara baada ya kuwasili kwa makocha hao wataanza programu ya kuwapa mafunzo wachezaji hao chipukizi ambao watakuwa ni wa umri chini ya miaka 18.
Mwakalebela alisema kuwa wataalamu hao, ambao wanakuja kupitia mradi ya TFF na kampuni ya Kiliwood ya Uingereza, watakuwa wanawafanyia usaili wachezaji hao na kuwachuja hadi kubakia 25, ambao ndio watapatiwa masomo ya sekondari na ya soka katika kituo maalumu kilichojengwa mjini Bagamoyo.
“Kila kitu kiko tayari, wachezaji wanatarajiwa kuwasili jijini, Januari 2 na mafunzo yataanza siku inayofuatia,” alisema Mwakalebela.
Aliongeza kuwa kati ya chipukizi hao, ambao wataanza kufundishwa soka, 45 ni wale waliochaguliwa katika mashindano ya Copa Cocacola mapema mwaka huu na wengine wamechaguliwa kutoka katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
Alisema kuwa zoezi la kuchagua wachezaji kutoka mikoani limeendeshwa na wakufunzi wa mikoa yote hapa nchini ambao nao walipewa elimu na wakufunzi wa kimataifa.
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo nchini (BMT), Iddi Kipingu, ambaye ni mdau katika soka la vijana anatarajiwa kuwa mkuu wa kituo hicho, ambacho kilijengwa chini ya usimamizi wake na alisema kuwa endapo atapatikana mchezaji anayesoma katika Shule ya Msingi atatafutiwa shule iliyo karibu na kituo ili kuweza kujiendeleza.
TFF na Kiliwood ziliingia ubia wa kuendeleza soka la vijana na kwa kuanzia ndio linatekeleza programu hii ya kwanza chini ya wataalamu hao kutoka Uingereza.
[zoomer]50|400|0|Power Thumbnail|0|0[/zoomer]
Pia TFF imezitaka timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara kusajili wachezaji wa umri chini ya miaka 20 ili kuweza kuwaandaa vyema na baadaye kupata timu ya taifa iliyobora na imara.
Comments
Loading…