*Ni kijana mwenye umri wa miaka 37
Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) limeonyesha nia ya mageuzi baada ya kumchagua Moses Magogo kuwa rais wake mpya
Magogo ni kijana mwenye umri wa miaka 37, ambaye kitaaluma ni mhandisi wa umeme, ambaye kabla ya kuanza kazi yake mpya alikuwa akifanya kazi Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).
Magogo alipata kuwa makamu wa rais wa shirikisho hilo anayeshughulikia utawala, na sasa amekabidhiwa uongozi mkuu.
“Nafurahi sana kwamba mkutano mkuu umenipa mamlaka ya kuongoza soka nchini mwetu kwa miaka minne ijayo,” alisema Magogo.
Anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Lawrence Mulindwa aliyeongoza kwa miaka minane na wakati wa uchaguzi huu hakutaka kugombea tena.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Patrick Okanya alithibitisha kwamba ingawa Magogo ndiye pekee aliyepitishwa kugombea baada ya kukidhi vigezo, ilikuwa lazima kura zipigwe, ambapo alipata asilimia 92.3 katika uchaguzi uliofanyika Jinja Nile Resort mjini Jinja.
Kati ya wapiga kura 73, ni 69 waliompa kura za ndiyo, watatu walimkataa na kura moja ikaharibika.
Mjumbe wa Fifa, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Tanzania, Ledeger Tenga alieleza furaha yake kwa uchaguzi huo kwenda shwari na zaidi kwamba Uganda wanafanya vizuri kwenye soka.
Wajumbe wengine waandamizi waliochaguliwa kewnye uchaguzi huo ni pamoja na Justus Mugisha (Makamu wa Kwanza wa Rais), Darius Mugoye (Makamu wa Pili wa Rais) na Mujib Kasule anayekuwa Makamu wa Tatu wa Rais.
Wajumbe kadhaa pia walichaguliwa katika kamati ya utendaji ya FA hiyo ya Uganda.
Comments
Loading…