Qatar yawadhalilisha wafanyakazi wageni
Maandalizi ya Kombe la Dunia 2022 yanakwenda ndivyo sivyo, kwani Qatar imezidi kuripotiwa kuwadhalilisha wafanyakazi wahamiaji.
Shirika la haki za binadamu la Amnesty International (AI) limesema kwamba wafanyakazi hao wanatendewa kama wanyama.
Tuhuma dhidi ya Qatar kwa wageni hao, wakiwamo wa Nepal zilishatolewa na Fifa ikasema ingechunguza, lakini inaelekea hakuna marekebisho yoyote yaliyofanywa.
Qatar ina asilimia kubwa ya wageni ambao ndio hufanya kazi mbalimbali, hasa za suluba, hivyo ujenzi wa miundombinu ya Kombe la Dunia unawategemea wao.
AI imesema wahamiaji hao wengi upokonywa pasi za kusafiria, hawapewi mishahara na hufanya kazi katika mazingira magumu.
Ilisharipotiwa kwamba wafanyakazi hao walifikia mahali pa kunyimwa hata maji ya kunywa wanapokuwa kazini, hali inayowafanya kunyongea sana na hata baadhi wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na mazingira ya kazi.
AI imekwenda mbali zaidi na kusema kwamba mmoja wa mameneja wa viwanja vinavyojengwa alipata kuwaita wafanyakazi hao kuwa ni wanyama.
Kuna upinzani mkubwa kwa Qatar kuandaa mashindano hayo yanayofanyika majira ya kiangazi, kwani nchini humo hali ya hewa huwa ya joto kali, kuzidi nyuzijoto 50.
AI inasema ilifanya majojiano na wafanyakazi 210, waajiri na maofisa wa serikali na kujiridhisha kwamba wafanyakazi hao wahamiaji hawapati haki.
Wanepali wametoa ushuhuda kwamba walifanyishwa kazi saa 12 kwa siku saba kwa wiki ikiwa ni pamoja na nyakati hizo za joto ambazo wadau wa soka wanasema haitakuwa rahisi kukaa viwanjani na wachezaji kucheza.
Baadhi ya wafanyakazi hao walitishiwa kupigwa faini au hata kurejeshwa makwao iwapo wangekosa kazi japokuwa hawalipwi chochote.
Mwaka jana wafanyakazi zaidi ya 1,000 walilazwa katika Hospitali Kuu ya Doha nchini humo baada ya kujeruhiwa wakiwa kazini, baadhi wakianguka kutoka vina virefu.
Qatar ni moja ya nchi tajiri zaidi duniani, kutokana na kuwa na hazina kubwa ya mafuta na watu wachache, ndiyo maana wengi wa raia wake huajiri wageni kutoka nje.
Wengi wa wageni hao wanatoka kusini mwa Asia, kwenye nchi masikini. Fifa hivi sasa inafikiria kuhamisha mashindano hayo nyakati za baridi, lakini kuna upinzani kutoka kwa baadhi ya wadau.
Comments
Loading…