MSIMU wa Ligi Kuu Tanzania Bara umemalizika, huku mabingwa wa zamani klabu ya Simba
wakiambulia patupu katika msimu wa pili mfululizo. Simba wamekosa mataji ya Ligi Kuu,
Shirikisho, na Ngao ya Jamii. Kwa hadhi yake, Simba haipaswi kumaliza msimu bila kunyakua
taji lolote. Ingawaje Simba wanayo rekodi ya kunyakua taji la Ligi Kuu mara nne mfululizo
wakiwatimulia vumbi watani wao.
Hata hivyo msimu wa mwaka 2022-23 ni kama ulivyokuwa msimu wa 2021-22, ambako Simba
walipoteza taji lao walilolishikilia misimu minne. Naam, ni namna gani Simba wamepoteza
umwamba katika Ligi Kuu Bara huku wakiwa miongoni mwa wababe wa soka la kimataifa
Afrika? Katika makala haya naangazia maeneo matano makuu ambayo yamedhoofisha ufanisi
wa Simba.
MAWINGA
Ukiangalia orodha ya majina ya wachezaji wa Simba yanatisha sana. Lakini katika idara ya
mawinga imekuwa na wakati mgumu, taarifa toka ndani ya Simba zimebainisha kuwa kocha wa
sasa Robertinho anamhitaji Hassan Dilunga ili awe sehemu ya kikosi cha kikosi chake. Idara ya
mawinga kwa Simba imekuwa changamoto licha ya kuwa na wachezaji kama Pape Ousmane
Sakho, Peter Banda,Kibu Denis kwa kuwataja wachache.
Ni Kibu Dennis pekee ambaye aliibuka katika kikosi cha kwanza cha kocha Robertinho.
Mawinga wa Simba wanatumika kama mbadala wa mbinu, jambo ambalo watani wao wa jadi
wamelitumia kwa msimu mzima kuwategema Jesus Moloko,Farid Mussa na Tusilla Kisinda.
Katika idara hiyo Peter Banda amekwua majeruhi mara kwa mara hali ambayo imekuwa
ikimweka benchi hata pale alipokuwa timamu kiafya. Kifupi Simba wanahitaji kuimarisha eneo
hilo kuwa na mawinga ambao wataleta ufanisi kwa timu yao.
KIUNGO MKABAJI
Kwa msimu mzima Simba wamekuwa wakiwategemea Saido Kanoute na Mzamiru Yassin.
Ikiwa wawili hawa wasipocheza vuziri Simba ilikuwa inapoteana kabisa eneo la katikati. Ujio
wa kiungo mkabajai mwingine Sawadgo hakuwa na tija, ndio maana kocha Robertinho aliamua
kumtupia benchi. Kimsingi Sawadogo hajafikia hata robo ya ufanisi ambao ungeletwa na Jonas
Mkude ambaye msimu huu muda mwingi amekuwa majeruhi pamoja na kushindwa kuonesha
kiwango kizuri.
Kuna baadhi ya mechi Kanoute akiwa majeruhi ilionekana wazi Simba walikuwa wanapata shida
katika mechi kadhaa za Ligi Kuu kwa sababu mategemeo ya injini yao yalikuwa kwa Yassin.
Hilo ni tofauti na watani wao wa jadi ambao wamekuwa na wachezaji watatu wa eneo moja;
Yannick Bangala, Khalid Aucho na Zawadi Mauya. Lakini Simba katika benchi lao kuna
mkongwe Erasto Nyoni, ambaye umri unamtupa mkono. Hili ni eneo ambalo linahitaji
kuimarishwa ili anapokosekana mmoja timu iwe katika uimara uleule.
WASHAMBULIAJI
Kapteni John Bocco ana heshima zake katika Ligi Kuu Tanzania. Majeruhi,kushuka kiwango na
mipango ya mbinu za walimu ni sehemu ya maisha ya wachezaji akiwemo John Bocco. Huyu wa
sasa si Yule aliyetamba misimu kadhaa iliyopita. Si kwamba ameishiwa makali lakini
inaonekana dakika zake kuwepo uwanjani zimepunguzwa na walimu, lakini wabadala wake
hawana uimara kumzidi.
Jean baleke alitoka TP Mazembe kuja kwa mkopo, lakini yeye si mshambuliaji ambaye Simba
wanatakiwa kujivunia au kujaribu kumlinganisha na Chriss Mugalu. Ikiwa uongozi wa Simba
unaweza kufanya maamuzi ya haraka basi Prince Dube wa Azam anaweza kuwa mchezaji wao
muhimu wa kuimarisha eneo la ushambuliaji. Upachikaji wa mabao umepungua sana Simba
kwa sababu ya washambuliaji kutokidhi viwango. Njia pekee ni kusajili washambuliaji wawili
wapya watakaosaidiwa na John Bocco huku Jean Baleke akipewa mkono wa kwaheri.
GOLIKIPA
Ukweli usemwe, nje ya Aishi Manula hakuna golikipa mwenye uwezo wa kukaa langoni mwa
Simba kwa wale waliopo kikosini. Si Ali Salim wala Benno Kakolanya, ni makipa ambao
hawaweza kuvivaa viatu vya Aishi Manula. Matokeo yake Simba kwenye Ligi ya Mabingwa
imefungwa mabao yenye kutia huzuni kama simanzi kwa sababu ya ufanisi hafifu uliopo katika
kikosi chake.
Ikiwa Simba wanataka kuimarisha eneo hilo, ni dhahiri wanatakiwa kutafuta Kipa mwingine
mwenye hadhi angalau ya Metacha Mnacha ambaye licha ya kukaa benchi pale Yanga
unafahamu kabisa ni aina ya golikipa mwenye uwezo mkubwa na uzoefu wa kutosha. Ali Salim
anaweza kusaidiwa kupelekwa mkopo katika timu nyingine ili kuimatishwa uwezo wake. Lakini
litakuwa tukio la uongo kuaminishwa kuwa ndiye mrithi sahihi wa Manula. Vivile Simba
wanahitaji golikipa mwenye uwezo wa kimataifa ambaye anakuwa mbadala wa Manula ili
kuboresha ufanisi wa idara ya makipa ya Simba. Kinyume cha hapo kauli za tumetolewa kiume
zitazidi kila msimu.
MABEKI
Idara hii si mbaya sana, lakini inaleta swali itakuwaje siku Hennock Inonga akichoka? Je
waliopo benchi wanakidhi vigezo vya kuchukua nafasi zao? Inonga ndiye beki ambaye amekuwa
akicheza kwa ufanisi mkubwa Simba. Lakini yeye si roboti kwa maana hiyo nahitaji mabeki
mbadala ambao wanaweza kumpumzisha wakati timu ikiendelea na mipango ya mechi nyingine.
Lakini hali iliyopo Simba iwapo Inonga akipata majeruhi inaonekana wazi wabadala wake
hawafiki hata nusu ya kiwango na ubora alionao Mkongamani huyo. Nini Simba wanachoweza
kufanya? Ni rahisi kwakuwa ni timu inayotikisa mara kwa mara soka la Afrika ni wazi itakuwa
inawavutia wachezaji wengi kupitia timu kwa maana ya kuonekana kimataifa. Ni jukumu la
Simba wenyewe kuimarisha eneo hili. Mabeki wa kuchezea Simba wawe na viwango na ubora
wa hali ya juu. Simba imefika hadhi ya kuwashawishi wachezaji kutoka vilabu mbalimbali hapa
Afrika. Naamini wapo mabeki ambao wanaweza kuisaidia zaidi kwa mbinu tofauti kulingana na
mechi.
USHINDANI LIGI KUU
Mwisho kabisa niwaambie mashabiki wa Simba, adui wa nyongeza ni ushindani. Ligi yetu
imekua na imepata wachezaji wazuri waliopo katika timu zingine. Kwahiyo ushindani kati ya
timu za Ligi Kuu umekuwa mkubwa hali ambayo inazifanya timu kongwe na kubwa kukutana na
wakati mgumu. Njia pekee ya kushinda katika hilo ni kusajili wachezaji wazuri zaidi yao na
kuweka malengo ya kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa. Kwa sasa Simba haiapswi
kumwambia mwalimu eti malengo ni robo fainali badala yake iwe fainali na akishindwa
anaruhusiwa kuondoka pasipo malipo yoyote ya fidia kwa vile atakuwa hajafikisha
walichokubaliana.