*Chelsea wacheka, Sunderland gunia la mazoezi
*Everton wazidi kung’aa
Newcastle Mzunguko wa tano wa Ligi Kuu ya England (EPL) umeanza kwa Liverpool waliokuwa wakitambia ushindi mfululizo kupokea kipigo cha kwanza katika msimu huu.
Kigingi dhidi ya Liverpool walikuwa vijana wa pwani ya kusini mwa nchi, Southampton waliowanyuka kwa bao 1-0 lililofungwa na Dejan Lovren katika dimba la Anfield.
Vijana wa kocha Brendan Rodgers waliingia uwanjani kwa kujiamini, wakijua kama kawa wangeondoka na ushindi na kuendelea kuongoza ligi, lakini haikuwa hivyo.
Bao la Saints lilipatikana mapema kipindi cha pili baada ya mfungaji kumzidi ujanja Daniel Agger wa Liverpool kwenye sekeseke la kona iliyochongwa na Adam Lallana.
Chelsea nao walipoza machungu ya kufungwa kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) katikati ya wiki, kwa kuwafunga Fulham 2-0.
Kadhalika Chelsea wamekuwa na mwanzo usio mzuri sana wa ligi katika misimu 10 iliyopita, licha ya kuwa na kocha mkongwe, Jose Mourinho aliyerejea Stamford Bridge kwa mara ya pili.
Mabao ya Chelsea yalifungwa katika kipindi cha pili na Mbrazili Oscar na Mnigeria John Mikel Obi ambaye amekuwa haanzishwi na Mourinho kwenye mechi zilizopita.
Matokeo hayo yamepindua msimamo wa EPL, yakiwapandisha Chelsea nafasi ya kwanza na kuwashusha Liverpool hadi ya pili, wote wakiwa na michezo mitano na kujikusanyia pointi 10.
Everton waliowatesa na kuwafunga Chelsea kwenye mechi ya ligi iliyotangulia, Jumamosi hii wameendelea kung’ara, baada ya kuwafunga West Ham United 3-2.
Everton wanaofundishwa na kocha wa zamani wa Wigan, Roberto Martinez walipata mabao mawili kupitia mipira ya adhabu ndogo ya beki Leighton Baines.
West Ham walio chini ya Sam Allardyce ‘Big Sam’ walipambana na walikuwa wa kwanza kufunga kupitia kwa Ravel Morrison kabla ya Baines kusawazisha.
Wakicheza watu 10, West Ham walifanikiwa kupachika bao la pili kupitia kwa Mark Noble, lakini mchezaji wa Chelsea aliye Everton kwa mkopo, Romelu Lukaku aliwapatia Everton bao la ushindi.
Katika mechi nyingine Aston Villa waliwafunga Norwich 1-0; West Bromwich Albion wakawakung’uta Sunderland 3-0, huku mechi kubwa ikisubiriwa Jumapili hii kati ya mahasimu wa jiji la Manchester – Manchester City na Manchester United wakati Arsenal watapepetana na Stoke City.
Kwa matokeo ya Jumamosi, Arsenal wanashika nafasi ya tatu wakifuatiwa na Tottenham Hotspur, Everton, Southampton, Man City, Man United, Stoke na Hull. Sunderland wanashika mkia kwa kuvuna pointi moja tu katika mechi tano.
Comments
Loading…