in ,

Ligi yetu inazungumza UONGO sana

Hakuna lugha sahihi ambayo inaweza ikakupa rangi sahihi ya tabia ya kitu Fulani. Ndiyo maana waswahili wanaamini kutokuamini kwenye kila kitu ambacho macho na masikio yanachosikia.

Kuna wakati kabisa hutakiwi kuvipa nafasi kubwa viungo hivi viwili (macho na masikio) bila kuruhusu ubongo wako utafasiri kitu ambacho unakiona au kukisia.

Ndiyo maana kaka yangu Israel Saria kila siku huwa ananiambia nisilaze akili. Nisiruhusu hata siku moja akili yangu ilale, ikapitiwa usingizi.

Nihakikishe kila muda akili yangu iko hai, inawaza kila wakati. Na hiki ndicho kitu ambacho natembea nacho kila uchwao.

Nimekuwa makini sana kwa kutoilaza akili yangu. Hata masikio yangu na macho yangu yakiniletea kitu huwa natafakari sana.

Ndiyo maana huwa naogopa kuingia kwenye mkumbo wa kusifia mpaka kupitiliza. Na hiki ndicho kitu ambacho kinafanyika sana kwenye ligi yetu.

Ligi yetu inakuzwa sana, inasifiwa sana na wakati mwingine kuna baadhi ya wachezaji hupewa vyeo ambavyo hawastahili na wenyewe huvipokea na mwisho wa siku hubweteka na kupotea.

Ndiyo ligi ambayo iliwahi kumuita Ramadhani Singano “Messi” lakini cha kushangaza mpaka sasa hivi hajawahi hata kwenda ligi kuu ya Rwanda.

Ndiyo ligi ambayo iliwahi kuwa na “Boban”. Boban asiyejielewa, Boban mwenye kipaji chake kikubwa, kipaji ambacho kilikuwa kinavutia sana.

Lakini mwisho wa siku Leo hii yupo Yanga anamalizia siku zake za mwisho za ustaafu katika soka huku akiwa hana kitu kikubwa alichovuna kutoka kwenye miguu yake.

Pembeni yake kuna Mrisho Khalfan Ngasa, yule ambaye aliwahi kupata nafasi ya kufanya majaribio katika ligi kuu ya England lakini kwa sababu hakuwa anajitambua alirudi hapa.

Na Leo hii yupo ananyanyasa watu kwenye viwanja vyetu vibovu. Ni kawaida sana kwa sasa timu zetu hasa hasa hizi kubwa kunyanyasa dagaa.

Ni kawaida sana kwa Azam Fc, Simba na Yanga kuonekana ni timu imara kwenye ligi yetu. Watakutana na Biashara , Biashara itafumuliwa.

Watakutana na Alliance FC, Alliance Fc watararuliwa mpaka huruma. Unajua hii kwanini inatokea hivi ?, hapa sababu ni ndogo sana.

Wachezaji wa timu za Azam Fc, Yanga na Simba Mara nyingi huwa wanapata matunzo mazuri kuzidi hawa ambao wanatoka kwenye hizi timu ambazo zinaonekana ndogo.

Na wakati mwingine timu hizi tatu (Azam Fc, Simba na Yanga) huchukua baadhi ya wachezaji ambao huonekana nyota hapa kwetu.

Hivi mzani huwa unakuwa hauko sawa kati ya hizi timu tatu (Azam Fc, Simba na Yanga) ndiyo maana ni rahisi kusikia Simba kamfunga Ruvu Shooting magoli 7-0.

Na siyo kumfunga tu , tena kutakuwa na habari za baadhi ya wachezaji kung’ara sana. Na wengine kubatizwa majina ya kishujaa.

Na wengine huonekana ndiyo wachezaji sahihi na wa kiwango kikubwa cha kucheza na timu yoyote ile.

Kwa kifupi washindani wa Simba , Yanga na Azam Fc hawatoi ushindani mzuri kwa hizi timu tatu. Ushindani ambao hutoa picha halisi za vikosi vya hawa wakubwa.

Hawa wakubwa mara nyingi ndiyo wamemuwa wakituwakilisha katka michuano ya kimataifa. Na wanapokuwa wanaenda kwenye michuano hii huenda wakiwa na sura tofauti.

Sura ambayo huonesha kuwa wao wana wachezaji bora kwa sababu tu hufanya vizuri kwenye ligi dhidi ya timu ambazo ni dhaifu.

Hatuna timu nyingi imara za kuwapa changamoto wawakilishi wetu kimataifa. Kipimo chetu tunachokitumia (ligi kuu) siyo kipimo sahihi kabisa.

Tofauti na timu zingine ambazo huwa tunakutana nazo kwenye michuano ya kimataifa. Ligi zao huwa ni kipimo bora kwa wawakilishi wao wa kimataifa.

Tunaweza tukawasifia sana wachezaji wetu kipindi wanapofanya vizuri kwenye michuano yetu ya ndani.

Lakini ukweli ni kwamba ligi yetu inatudanganya sana. Siyo kipimo sahihi kwa timu zetu. Na kibaya zaidi hakuna mazingira sahihi yaliyoandaliwa kuifanya ligi yetu Iwe sahihi.

Ligi ndiye mzazi , mzazi ambaye anatakiwa kutoa malezi bora kwa watoto. Watoto ambao wanatakiwa kufanya kitu chenye mafanikio kutokana na malezi ya mzazi ambaye ni ligi.

Cha kusikitisha mzazi ligi kuu hatoi malezi bora kwa wanaye. Hazalishi watoto ambao wanaweza kupigana nje ya ligi yetu.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
OLE

Ole Gunnar ni ZIDANE AU DI MATEO wa Manchester United ?

Tanzania Sports

Simba imeshinda lakini isisite kujifunza kwa Al Ahly