Utamaduni wa timu kushuka dimbani siku ya pili ya Krismasi katika Ligi Kuu ya England umeendelea kwa vigogo kupata ushindi.
Chelsea wameendeleza pengo la pointi tatu juu ya msimamo wa ligi, ambapo Diego Costa amefunga bao lake la 13 msimu huu, John Terry akitupia jingine kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya West Ham.
MAN CITY MBELE KWA MBELE
Manchester City wakicheza dhidi ya West Bromwich Albion, walitisha kwa kufunga mabao matatu katika kipindi cha kwanza kwenye ushindi wa 3-1.
Fernando ndiye alifungua kitabu cha mabao baada ya kipa Ben Foster kutema majalo ya Jesus Navas.
Yaya Toure alifunga bao la pili kwa penati baada ya David Silva kuchezewa rafu, naye akatia kimiani la tatu kwa uzuri.
West Brom walifuta machozi kwa bao la dakika za mwisho kupitia kwa Brown Ideye.
MAN UNITED NAO MAMBO SAFI
Manchester United wamefanikiwa kubaki nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kuwafunga Newcastle 3-1 na kuwa pointi 10 nyuma ya vinara Chelsea.
Vijana hao wa Louis van Gaal sasa wamefikisha mechi nane mfululizo bila kufungwa hata moja.
Wayne Rooney alifunga bao la kuongoza, kutokana na majalo ya Radamel Falcao. Nahodha huyo alifunga tena jingine na kisha Robin van Persie naye akatikisa nyavu kwa bao la kichwa.
Papiss Cisse alifunga bao dakika za mwisho
Newcastle walimlalamikia mwamuzi Mike Jones kwa kutompa kadi Juan Mata kwa kumchezea vibaya Yoan Gouffran ndani ya eneo la penati wakati timu zikiwa 0-0.
ARSENAL WASHINDA, GIROUD NJE
Arsenal wamefanikiwa kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Queen Park Rangers (QPR) kwenye mechi iliyoshuhudia mchezaji wao, Olivier Giroud akipewa kadi nyekundu mapema kipindi cha pili.
Ulikuwa ushindi wa 400 kwa Wenger kwenye ligi kuu hapa, lakini ulitiwa doa na Mfaransa mwenzake huyo kumpiga kichwa Nedum Onuoha baada ya kuchezewa vibaya.
Kadhalika Alexis Sanchez alikosa penati ambayo ingewaweka Arsenal mbele mapema zaidi, lakini akarekebisha makosa hayo kwa kufunga bao dakika ya 37.
Tomas Rosicky aliyerejea kutoka kwenye majeraha yake alifunga bao la pili baada ya Giroud kutolewa nje. Beki wa kulia Mfaransa, Mathieu Debuchy alimwangusha Junior Hoilett kwenye eneo la penati dakika 12 kabla ya mpira kumalizika, na Charlie Austin akafunga penati hiyo.
MATOKEO MENGINE
Katika matokeo mengine, Burnley walibanwa nyumbani kwa kufungwa 1-0 na Liverpool, Crystal Palace wakalala 3-1 kwa Southampton, Everton wakapigwa 1-0 na Stoke.
Kadhalika Sunderland walioga kichapo cha 3-1 kutoka kwa Hull na Swansea wakawafunga Aston Villa 1-0.
Comments
Loading…