in , , ,

Ligi Kuu Ya Tanzania Ni Bora Au Pendwa?

Soka ni moja ya michezo yenye mvuto mkubwa na wa kipekee kwa jamii ya Tanzania, huku ligi kuu ya Tanzania (NBC Premier League) ikivuta hisia za wengi ndani na nje ya mipaka. Hata hivyo, mijadala mbalimbali imeibuka kuhusu ikiwa Tanzania ina ligi bora au ligi pendwa. Na wewe msomaji utatuambia mwisho kabisa wa Makala hii kwamba Ligi Kuu ya Tanzania ni ligi bora au ligi pendwa? 

Makala hii inachambua kwa kina masuala haya, ikiangazia sababu zinazofanya ligi ya Tanzania kuwa na sifa hizo na kutathmini kama inafikia vigezo vya kuwa ligi bora au inabakia kuwa ligi pendwa.

Vilabu vikongwe vya Simba na Yanga vimekuwa vikiunda kiini cha ligi kuu ya Tanzania kwa miongo mingi. Mashabiki wengi wa soka nchini hujihusisha na vilabu hivi kutokana na historia yao ndefu, umaarufu pamoja na mafanikio katika soka la ndani na kimataifa. Simba na Yanga si tu vilabu maarufu bali pia vina mafanikio makubwa katika mashindano mbalimbali barani Afrika. Vilabu hivi huvutia mashabiki wengi na kwa maana hiyo huchangia kwa kiasi kikubwa katika kufanya ligi ya Tanzania kuwa maarufu.

Pamoja na kuwa na idadi kubwa ya mashabiki, Simba na Yanga pia zina ushawishi mkubwa wa kifedha changamoto kubwa kutoka kwao ni kwamba zimekua ni klabu ambazo hazina miundombinu ya kisasa ambayo inaimiliki wenyewe zaidi sana wamekua wakikodisha maeneo kwa ajili ya kambi tofauti na klabu kama Azam ambao wao wana eneo lao rasmi kabisa linalowatambulisha.

Tanzania Sports
Mdhamini wa Ligi Kuu Ya Tanzania, NBC Bank

Ushawishi huu wa Simba na Yanga katika ligi kuu ya Tanzania unachangia kuifanya ligi hiyo kuvutia na hivyo kuitwa “pendwa,” kwani ushawishi wao unavutia hisia za mashabiki na kipaumbele katika vyombo vya habari. Hata hivyo, pendwa haimaanishi kuwa ni bora, kwani baadhi ya changamoto zimebaki kwenye ubora wa ligi yenyewe.

Ubora wa ligi yoyote duniani huathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya miundombinu yake. Tanzania imefanya maendeleo katika uboreshaji wa miundombinu ya soka, hasa viwanja vya kuchezea. Viwanja kama Benjamin Mkapa, Amani (Zanzibar),Azam Complex , KMC Complex , Meja Generali Isamuhyo na viwanja ambavyo vinamilikiwa na CCM vinaendelea kuboreshwa ili kuwa na viwango vya kimataifa.

Miundombinu ya viwanja, vifaa vya mazoezi, na hata usafiri kwa baadhi ya timu ni changamoto zinazoathiri ubora wa ligi. Timu nyingi zinazoshiriki ligi kuu zinakosa miundombinu ya kisasa, jambo linaloathiri utendaji wao na kushusha viwango vya mchezo. Kwa hiyo, wakati ligi inavutia, changamoto ya miundombinu huifanya isiwe bora sana ikilinganishwa na ligi zenye miundombinu ya kisasa zaidi.

Wachezaji ni moyo wa soka, na ubora wa ligi hupimwa kwa viwango vya wachezaji wake. Ligi kuu ya Tanzania imekuwa ikivutia wachezaji kutoka nchi mbalimbali za Afrika kama vile Ghana, DR Congo, Uganda, na Kenya. Kuongezeka kwa wachezaji wa kigeni kumechangia kwa kiasi fulani kuboresha ubora wa ligi na kuwafanya mashabiki wengi kuifuatilia kwa hamasa. Hata hivyo, wachezaji wengi wanaotua Tanzania si kutoka ligi zenye ushindani wa hali ya juu, jambo linaloathiri ubora wa ushindani wa ligi japokuwa wanakua wanafanya vizuri pale wanapokua wanapata nafasi za kucheza katika klabu ambazo zinakua zimewasajili.

Uwekezaji pia ni jambo muhimu. Licha ya Simba na Yanga kuonekana kuwekeza zaidi katika wachezaji na miundombinu, timu nyingine nyingi zinakosa uwekezaji wa kutosha. Hii inafanya baadhi ya timu kuathirika kwa kutokuwa na kikosi chenye nguvu. 

Kwa upande mwingine, ligi pendwa haitegemei tu ushindani wa timu, bali umaarufu wake kwa mashabiki. Hapa ndipo ligi ya Tanzania inapofikia sifa ya “pendwa,” kwani licha ya kuwa na ushindani mdogo, watu wengi hupenda na kuifuatilia. Mechi za Simba na Yanga huvutia mashabiki wengi sana na hata kupelekea uwanja wa Benjamin Mkapa kujaa, jambo linaloashiria umaarufu wa ligi licha ya changamoto za ushindani.

Vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vina nafasi kubwa katika kutangaza na kufanya ligi kuwa pendwa au bora. Kwa upande wa ligi ya Tanzania, mashabiki wengi hufuata habari za ligi kupitia vituo vya habari, blogu za michezo, na mitandao ya kijamii kama vile Instagram, Facebook, na Twitter. Vyombo vya habari pia vimefanikiwa kuhamasisha mashabiki, na hii imechangia ligi kuwa na washabiki wengi wanaopenda ligi kuliko ubora wa mchezo wenyewe.

Wakati huo huo, ligi bora pia hutegemea sana vyombo vya habari ili kuweza kushindana katika soko la kimataifa. Hata hivyo, ligi ya Tanzania inakosa upana wa usambazaji wa habari zake nje ya mipaka, jambo linalozuia kuitangaza kama ligi bora barani Afrika. 

Mimi naamini kuwa Ligi kuu ya Tanzania (NBC Premier League) inabakia kuwa na sifa ya “pendwa” zaidi kuliko “bora.” Umaarufu wa vilabu vikubwa kama Simba na Yanga, idadi kubwa ya mashabiki wa ndani, na mchango wa vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vinasaidia kufanya ligi hiyo kuwa ya kupendwa sana. 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

Tunazijua Vyema Sheria, Au Ni Mijadala Tu

Rúben Amorim

Matano yanayomkabili kocha mpya Man United