Mambo 10 tuliyojifunza kwenye michezo ya EPL ya mwishoni mwa wiki
1. Ederson athibitisha thamani yake pale City
Katika mchezo uliomalizika kwa Manchester City kushinda 3-2 dhidi ya Fulham, mlinda mlango wa City, Ederson alikuwa na mchezo mzuri akiokoa michomo kadhaa muhimu hasa dhidi ya winga Adama Traoré. Mlinda mlango huyo aliyeisaidia City kushinda mataji manne ya Ligi Kuu mfululizo, ana thamani kubwa na ameionesha thamani hiyo mwishoni mwa wiki. Vilabu vya Saudi Arabia, vilimtaka katika dirisha la kiangazi, ingawa Kocha wa City, Pep Guardiola anasema hakukuwa na ofa rasmi iliyoletwa mezani.
Guardiola anaamini uwepo wa Stefan Ortega umempa changamoto Mbrazil huyo ambaye ni chaguo la kwanza. “Wakati mwingine Ederson lazima ajihisi kuwa anahitaji kucheza vizuri, vinginevyo Stefan anaweza kuchukua nafasi yake. Na ushindani huu mzuri, kwa sababu wanaheshimiana na wana uhusiano mzuri sana, unafanya timu yetu kuwa bora.”
2. United wanahitaji kurejesha kiwango kwa haraka
Mjadala usiokwisha unahusu mustakabali wa Erik ten Hag. Sare tasa ya 0-0 ya Manchester United dhidi ya Aston Villa ilidhihirisha changamoto zinazomkumba kocha huyo Mholanzi.
Ukiacha kosa kosa ya kiungo Bruno Fernandes kwa mpira wake wa adhabu kugonga mwamba, kama sio juhudi za Diogo Dalot kuzuia mpira wa Jaden Philogene kutinga wavuni, katika dakika za majeruhi, pengine huyo ungekuwa mwisho wa Ten Hag pale Old Trafford. Baada ya mechi, Mholanzi huyo alijaribu kutoa matumaini, lakini hali bado tete kwa timu hiyo. Kupata nafasi kwa mlinzi mkongwe Jonny Evans, ambaye atafikisha miaka 37 Januari, mbele ya vijana kama Matthijs de Ligt na Lisandro Martínez ulikuwa mjadala mwishoni mwa wiki. Lakini tatizo kubwa la United linaonekana liko kwenye ushambuliaji, kwani wamefunga mabao matano tu katika mechi saba. Joshua Zirkzee, aliyeingia badala ya Rasmus Højlund katikati ya kipindi cha pili, ambaye amefunga bao 1 kati ya hayo, lakini kuna wasiwasi kwamba usajili wake wa £36.5m kutoka Bologna unaonyesha kama haujaleta manufaa. Hata kama Ten Hag anasema :”Tunawaamini wachezaji, na siku moja mambo yatajipa,”, United hawawezi kusubiri kwa muda mrefu zaidi. Inapaswa kurejea kwenye ubora wake haraka.
3. Southampton wanaonyesha matumaini
Licha ya Southampton kuchapwa 3-1 na Arsenal mwishoni mwa juma, lakini kocha wake Russell Martin alionyesha kuridhika na uchezaji wa timu yake dhidi ya Arsenal Jumamosi kuliko alivyokuwa siku tano zilizopita dhidi ya Bournemouth ambapo walichapwa pia 3-1. Cameron Archer alifunga bao, lililoibua matumaini ya muda mfupi kwamba Saints wangepata ushindi wa kwanza wa msimu kwenye uwanja wa Emirates kabla baadaye safu ya ulinzi ya timu hiyo kuruhus mabao 3. Lakini kuna matumaini huenda mambo yakaka vizuri kwenye mechi zijazo hasa dhidi ya vibonde wenzao Leicester, Everton, na Wolves, ingawa watakuwa na mlima ugenini dhidi ya Manchester City. Kocha Martin alisema: “Tuna mechi tatu kati ya nne katika kipindi kijacho ambazo ni muhimu. Tunahitaji kufanya vizuri zaidi kwenye mechi hizo.”
4. Kuwakosa nyota wake kwa kadi hakutawathiri Chelsea
Mapokeo ya kocha Enzo Maresca kuhusu wachezaji wawili wa Chelsea kuwa wa kwanza kwenye Ligi Kuu kufikishaa kadi tano za njano na kuwafanya wakose mchezo unaofuata, unaonyesha kwamba sheria za nidhamu siku zote zinaumiza zaidi vilabu vidogo kuliko vikubwa. Wesley Fofana na Marc Cucurella watakosa mechi ijayo dhidi ya ya Liverpool mnamo Oktoba 20 baada ya kupata kadi za njano kwenye mechi zote isipokuwa mbili kati ya saba za ilizocheza timu hiyo msimu huu.
Lakini Chelsea inajivunia kikosi kikubwa ilivchonacho, ambapo inaweza kubadilisha hata kikosi kizima na athari isiwe kubwa sana. Adhabu hii haionekani kuleta athari kubwa kama ambavyo ingeleta kwa vilabu vingine hasa vidogo. Maresca, baada ya kuwapongeza wachezaji wake kwa ari licha ya kwenda sare ya 1-1 dhdi ya Nottingham Forest, pale Stamford Bridge, alikuwa mtulivu kuhusu safari ya kwenda Anfield bila wachezaji wake hao wawili muhimu. “Tuna mapumziko ya kimataifa ya kujiandaa, na tutatumia wachezaji ambao hawakuwa katika kikosi cha kwanza,” alisema.
5. Welbeck anaonyesha uzoefu wake kwa Seagulls
Mwezi kamahuu miaka minne iliyopita mwezi huu, Danny Welbeck, alikuwa hana mkataba, alisajiliwa kuimarisha kikosi cha Brighton ambacho kilikuwa na upungufu wa washambuliaji. Atatimiza miaka 34 mwezi ujao na alichezea mara ya mwisho timu ya taifa ya England mwaka 2018, lakini bado ni mchezaji ambaye hajawahi kuwaangusha makocha kuanzia Sir Alex Ferguson hadi Fabian Hürzeler, ambaye ana umri mdogo kuliko yeye, akimzidi kocha miaka miwili. Welbeck hakuwa mshambuliaji wa asili, lakini uelewa wake wa jinsi ya kukimbia na kuunganisha wachezaji wengine ulichangia makocha kama Arsène Wenger na Roy Hodgson kumpa thamani. Brighton sasa inanufaika na uzoefu wake na ujuzi wake kwenye ushambuliaji. Alikuwa mwiba dhidi ya Spurs hasa kipindi cha pili, akifunga bao la ushindi baada ya Brighton kuwa nyuma kwa mabao 0-2 mpaka mapumziko, kabla ya kushinda 3-2. Hürzeler ni kocha kijana lakini inaonekana uzoefu wa wakongwe katika timu hiyo ulileta matokeo ya mwishoni mwa wiki. Welbeck aliweka wazi baada ya mechi kwamba wachezaji wakongwe ambao hukaa benchi, Jason Steele na James Milner, waliwakumbusha wenzao wakati wa mapumziko kuhusu umuhimu wa kupambana dhidi ya Tottenham. Mkongwe Welbeck kisha akaonyesha mapambano hayo kwa mfano akiwa uwanjani na kufunga bao la ushindi.
6. Pickford awafunga mdomo tena wazomeaji
Wakati Anthony Gordon alishindwa kufunga mbele ya timu yake ya zamani, pale Goodison Park, mlinda mlango wa Everton Jordan Pickford aling’aa katika mchezo huo wa sare ya 0-0 dhidi ya Newcastle. Kulikuwa na wakati ambapo kipa huyo mzaliwa wa Sunderland angeonekana kupambana na mashabiki wanaomzomea, lakini, kama alivyosema baada ya Everton kutoruhusu bao katika mchezo huo ambao ni wa kwanza kutoruhusu bao msimu huu: “Nilijifunza kutokana na yaliyopita, nakuwa mtulivu na nataka kufanya vyema kwa ajili ya klabu. Kuokoa penalti ya Gordon ilikuwa tukio kubwa la mchezo huo, lakini pia alionekana kuimarisha ubora na uwezo wake ukilinganisha na michezo ya hivi karibuni.
7. Slot anaonekana kuiboresha Liverpool
Jambo la kuvutia kuhusu Liverpool chini ya Arne Slot ni kwamba kuna maboresho ameyafanya katika maeneo mbalimbali ya timu hiyo. Huko nyuma mara kadhaa chini ya Jürgen Klopp, Liverpool waliruhusu mabao ambayo yalihitaji muda na jitihada kuyarejesha. Virgil van Dijk sasa anaonekana kurejesha tena kiwango chake bora akiwa na Ibrahima Konaté. Ryan Gravenberch anaonekana kufanya vyema eneo la kiungo akiwa na imara kiumbo. “Ana urefu, na ni imara katika mapambano,” alibainisha Slot. Cody Gakpo alitoa pasi ya bao la Diogo Jota, na anaonekana kuwa bora akitokea pembeni. Katika mchezo wa mwishoni mwa wiki, ulimalizika kwa Crystal Palace 0-1 Liverpool.
8. West Ham wameanza kuimarika kwenye eneo la ushambuliaji
Kabla ya ushindi wa 4-1 dhidi ya Ipswich, idadi ya mabao kutoka kwenye safu ya ushambuliaji kwenye mechi zao sita za kwanza za Ligi Kuu lilikuwa bao moja kutoka kwa Jarrod Bowen na penalti kutoka kwa Lucas Paquetá. Si kiwango kinachotarajiwa chini ya kocha mpya, Julen Lopetegui lakini, kwa safu dhaifu ua ulinzi ya Ipswich, mechi hiyo ilitoa taswira ya kwanza ya mtindo wa kuvutia na wa kushambulia ambao mashabiki wa West ham wanatamani kuona baada ya enzi ya David Moyes iliyokuwa na mbinu za kujihami zaidi. West Ham walipiga mashuti 13 yaliyolenga lango, idadi kubwa zaidi katika mechi moja ya Ligi Kuu ndani ya miaka 19. Huku wachezaji wake wanne wa ushambuliaji; Michail Antonio, Mohammed Kudus, Bowen, na Paquetá wote wakifunga. Hata hivyo mechi mbili zijazo za West Ham dhidi ya Tottenham na Manchester United zitatoa kipimo kigumu zaidi kwa washambuliaji wake.
9. Cooper ashusha pumzi kwa ushindi wa kwanza Leicester
Baada ya Steve Cooper kupata ushindi wake wa kwanza wa msimu kwenye ligi, hakukuwa na shangwe kubwa, bali alichagua kuwashukuru mashabiki pamoja na wachezaji wake wa Leicester. Ni wiki moja na nusu tu iliyopita ambapo baadhi ya mashabiki walimkosoa Cooper baada ya timu yake kuitos Walsall kwa ushindi wa penalti kwenye Carabao Cup. Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bournemouth unaiondoa Leicester kwenye shinikizo kubwa, lakini Cooper anajua kwamba mengi zaidi yanahitajika. “Lazima nijenge uaminifu hapa,” alisema Mwalimu huyo kutoka Wales.
10. O’Neil amekalia kuti kavu huko Molineux?
Wolves hali tete, na mwishoni mwa juma walianza kuruhusu kufungwa bao baada ya sekunde 76, na mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi baada ya hapo. Walichapwa na Brentford 4-1 wakiadhibiwa kwa makosa yao wenyewe. Mario Lemina akicheza faulo ya kiholela dhidi ya Nathan Collins na kupelekea penalti ambayo iliwapa Brentford uongozi wa 2-1. Safu yas ulinzi ya Wolves ilikuwa dhaifu sana. Kocha Gary O’Neil alisema bada ya mchezo: “Tuliruhusu mabao ya ajabu”, akirudia maneno aliyosema mwezi Agosti walipolala 6-2 dhidi ya Chelsea nyumbani Molineux. Kuna dalili mbaya kulingana na takwimu na huenda uwezo wa O’Neil usitoshe kuokoa jahazi na kujiokoa mwenyewe. Haitashangaza akiwa kocha wa kwanza kutimuliwa msimu huu.
Comments
Loading…