LEICESTER City wameandika historia mpya nchini hapa kwa kuwazidi nguvu
vigogo na kujitangazia ubingwa kabla hata ya Ligi Kuu ya England (EPL)
kumalizika.
Vijana hawa wa kocha Claudio Ranieri walijihakikishia ubingwa wakiwa
nyumbani, baada ya Tottenham Hotspur kulazimishwa sare ya 2-2 na
Chelsea, ikimaanisha sasa hakuna timu inayoweza kuwafikia tena.
Leicester walianza msimu wakichukuliwa na wengi kuwa si tu ni
wasindikizaji, bali moja ya timu ambazo zingeshuka daraja, kwani
Aprili mwaka jana walikuwa mkiani mwa ligi na walinusurika kushuka
daraja.
Msimu uliwaendea vyema, wakiongozwa na nahodha wao Wes Morgan na
washambuliaji mahiri Riyad Mahrez na Jamie Vardy waliochaguliwa kuwa
wachezaji bora na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA) na Waandishi wa
Michezo mtawalia.
Wapinzani wao wa karibu ambao ni Spurs, Arsenal, Manchester City,
Manchester United na mabingwa wa msimu uliopita, Chelsea walishindwa
kuwa na uendelevu wa ufanisi kwenye soka, huku Chelsea wakifikia
kumfukuza kocha Jose Mourinho, kwani aliwafikisha mahali pa kuelekea
eneo la kushuka daraja.
Arsenal walianza vyema lakini wakaishia kuteleza baada ya nusu ya
kwanza ya msimu, wakichangiwa na majeruhi na pengine kutojiamini.
Baadhi ya washabiki wamekuwa wakitaka kocha wao wa muda mrefu, Arsene
Wenger aondoke, lakini wamiliki wamesisitiza kwamba atakuwapo bado
Emirates.
Man City wanabadilisha kocha wao Manuel Pellegrini kwa kumleta yule wa
Bayern Munich, Pep Guardiola msimu wa kiangazi wakati Man United
wanafikiria kumfukuza Louis van Gaal na kumchukua ama Mourinho au
kocha mwingine wa kiwango cha juu. Chelsea watakuwa na huduma za
Antonio Conte msimu ujao.
Spurs hawana sababu ya kumfukuza kocha Mauricio Pochettino wala kuwa
na shaka naye, kwani ni mara ya kwanza baada ya miaka mingi kuwa
katika nafasi ya pili. Wamekuwa wakishika kuanzia nafasi ya nne shuka
chini.
Leicester walishaanza kusherehekea ubingwa baada ya kuona tofauti
kubwa ya pointi, ambapo Jumapili walicheza na Manchester United
wakaenda sare hivyo wakaahirisha. Washabiki wao Jumatatu hii
walikusanyika katika eneo la Uwanja wa King Power, Leicester
wakifuatilia mechi ya Spurs na Chelsea na wengine kwenye eneo kama
hilo kwa wamiliki wao nchini Thailand.
Leicester au Foxes kama wanavyojulikana, wamefikisha pointi 77 katika
michezo 36, na Spurs wana pointi 70 wataweza kufikisha pointi 76 tu
wakishinda mechi zilizobaki. Arsenal wanashika nafasi ya tatu wakiwa
na pointi 67 baada ya wikiendi kuwafunga Norwich 1-0. Man City wanazo
64 kutokana na kufungwa 4-2 na Swansea wikiendi pia wakati United
wamefikisha 60. West Ham United wanazo 59, Southampton wana 57 na
Liverpool 55. Ni katika hao watapatikana wa kucheza Ligi ya Mabingwa
Ulaya na Ligi ya Europa.