Bodi ya Ligi Kuu ya Tanzania wametangaza rasmi kuwa baada ya michezo ya mwisho ya mzunguko wa kwanza ni rasmi sasa ligi hii pendwa na Bora Afrika Mashariki na kati itasimama mpaka mwezi machi ili kupisha michuano ya kombe la Mapinduzi ambayo mwaka huu inashirikisha timu za Taifa Bila kusahau kuwa baada ya michuano ya kombe la Mapinduzi itakua ni wakati wa michuano ya kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani ambapo itashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya nchi husika pekee.
Huu utakua ni wakati mzuri kwa Timu zetu ambazo zinashiriki kimataifa ambapo hapa tunazungumzia Yanga wanaocheza ligi ya Mabingwa pamoja na Simba wanaocheza Kombe la Shirikisho Afrika kujiandaa Vyema zaidi Kwa ajili ya michuano hii ambapo wapo katika hatua ya makundi wakipambana kuitafuta robo fainali.
Ukiachilia mbali Simba na Yanga ni wazi kuwa hiki ni kipindi ambacho Timu ambazo hazikufanya vizuri mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na wako katika wakati mgumu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kuutumia vyema muda huu kuangalia makosa yao na jinsi ya kuboresha changamoto ambazo wamekutana nazo ili waweze kupambana na kubakia Ligi Kuu.
Kusimama kwa Ligi Kuu kwa muda wa miezi miwili kunaathiri wachezaji na makocha kwa njia mbalimbali. Kwa wachezaji, kukosekana kwa mechi za ushindani hupunguza kasi yao ya mchezo na mazoea ya kushindana hali inayoweza kusababisha kushuka kwa viwango vyao ambavyo tumeviona katika mchezo ambayo wamecheza kwenye ligi. Aidha ukitazama zile timu ambazo wachezaji wao hawajaitwa timu za Taifa wala hawana Mechi za kimataifa za klabu kukaa kwao muda mrefu bila mechi za mashindano kutaongeza hatari ya majeraha wanaporejea kwa sababu ya kuathirika kwa mwili na mazoea ya kimchezo.
Ukitazama kwa upande wa makocha, kusimama kwa ligi kunaleta changamoto za kupanga upya programu za mazoezi na kuhakikisha wachezaji wanabaki katika hali bora ya kimwili na kiakili. Pia, kuna presha ya matokeo wanaporejea kwa sababu ya matarajio kutoka kwa mashabiki na viongozi wa klabu. Aidha, mapumziko haya yanaweza kusababisha ugumu wa kufuatilia maendeleo ya wachezaji na kuchangia changamoto za kiufundi.
Kwa ujumla, kusimama kwa ligi kunapunguza mwendelezo wa ushindani, kuathiri mapato ya klabu, na kudhoofisha morali ya timu, hivyo ni muhimu hatua za kukabiliana na changamoto hizi zichukuliwe mapema.
Comments
Loading…