Mseto wa kiwango, kichapo na ugomvi
SI mara nyingi amekuwa na utimamu wa mwili au tayari kuchaguliwa kwa ajili ya mechi kwenye timu, lakini kurejea kwa Neymar Santos hakujawachosha washabiki hata kidogo.
“Eu vou mas, eu volto!”
Hayo ni maneno ambayo Neymar aliyaandika ukutani kwenye chumba cha kubadilishia nguo cha Vila Belmiro mnamo 2013 kabla ya kuvuka Bahari ya Atlantiki kujiunga na Barcelona. Ujumbe wake kwa mashabiki wa Santos ulikuwa wazi: “Ninaenda lakini nitarudi!”
Mambo makubwa yalitarajiwa kutoka kwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 21 ambaye alilelewa katika akademi iliyomtoa Pelé.
Wabrazil walitumai angewaongoza kwenye Kombe lao la Dunia la kwanza katika ardhi ya nyumbani mnamo 2014, na kufuta maumivu ya 1950, na kuwa mshindi wao wa kwanza wa Ballon d’Or tangu enzi za Kaká mnamo 2007. Kama tunavyojua sasa, ushindi huu haukutimia.
Kushinda Ligi ya Mabingwa na mataji saba ya ligi barani Ulaya, pamoja na kuvunja rekodi ya ufungaji mabao ya muda wote ya Pele kwa Brazil, si mafanikio ya kupgiwa tambo.
Hata hivyo, akiwa hajapata kutambuliwa kama mchezaji bora wa dunia, wala kushinda chochote isipokuwa Olimpiki akiwa na Brazil, Neymar atakabiliwa na shutuma za kutotumia ipasavyo uwezo wake kwa mafanikio ya nchi.
Ametimiza ahadi yake kwa Santos kwamba angerudi, hata hivyo. Akiwa amecheza mechi saba pekee kwenye Ligi Kuu ya Saudia wakati wa kipindi chake alichokejeliwa huko Al-Hilal, alirudi nyumbani Brazil akiwa mtu tajiri zaidi, akiwa bado mchezaji ghali kabisa wa kandanda.
Alitia saini kandarasi ya miezi mitano na Santos mwezi Januari na akawa na mchezo wake wa kwanza katika mechi ya kuwania ubingwa wa jimbo la São Paulo huku akishangiliwa na mashabiki wa nyumbani.
“Ninaipenda Santos sana na siwezi kupata maneno ya kuelezea hisia nilizokuwa nazo nilipotoka uwanjani leo,” alisema Neymar.
“Leo ilikuwa siku ya kipekee sana. Asante kwa kila mtu kwa upendo na kwa kutushangilia hadi mwisho. Nina furaha sana kwa hilo, lakini zaidi sana kiujumla kwa kurejea hapa. Nitajitahidi, kama ninavyofanya siku zote – kuiweka Santos pale inapostahili kuwa, kileleni. Twende kitimu. Pamoja hatuwezi kushindwa. Amini,” akasema.
Miezi michache baada ya mwito huo wa kupambana, hata hivyo, Neymar na washabiki wa klabu hiyo wapo katika hatari ya mzozo na hata kutengana kiaina. Kumekuwa na vionjo vya Neymar. Bao lake la ushindi dhidi ya vinara wa ligi Flamengo mwezi uliopita lilikuwa ukumbusho wa ubora wake wa kiwango cha kimataifa usio na shaka.
Lakini, kama ilivyo kawaida nchini Brazil, ambapo mambo yanaweza kwenda kutoka viwango vya juu zaidi hadi vya chini kabisa katika muda wa siku chache. Kulikuwapo kichapo cha 3-0 kutoka kwa Mirassol iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani kisha kisag cha 2-1 kutoka kwa Internacional.
Vichapo hivyo vilifuta hisia zozote nzuri zilizokuwa zimeanza kujengeka baada ya ushindi dhidi ya Flamengo. Huku wakiwa wameshinda mara tano pekee katika mechi 17 msimu huu, Santos wanaelea juu ya eneo la kushushwa daraja, jambo linalotia wasiwasi kwa klabu ambayo ndiyo kwanza imerejea Ligi Kuu.
Neymar alimwita shabiki fulani kando ya uwanja kwa ajili ya kubadilishana maoni ambayo yalinaswa na kamera.
“Aliniambia ninyamaze na kunitukana akisema kama mimi ni mwanaume niende chumba cha kubadilishia nguo kuzungumza,” shabiki huyo alieleza. “Nilimweleza kwamba akiwa nahodha alitakiwa kudai kwa wachezaji moyo wa kujitolea na dhamira, sikuelewa kwa nini alikuwa akikasirika Katika kila mchezo ninaokuwa uwanjani.
“Nilikuwa na mwanangu na mpwa wangu na tulivamiwa na mashabiki wengine baada ya ugomvi huo. Shabiki mmoja alijaribu kunipiga kofi usoni. Mpwa wangu naye alipata kipondo akaumia jicho kidogo.,” akasema.
Neymar alipinga maelezo hayo juu ya tukio husika. Akasema kwamba mashabiki wana haki ya kukosoa uchezaji wake lakini hawapaswi kamwe kufanya hali hiyo kibinafsi kwake.
“Ana haki ya kutoa maoni yake ikiwa nilicheza vizuri au vibaya, wasichoweza kufanya ni kuniudhi,” alisema Neymar.
“Kusema mimi ni mamluki, kuzungumza juu ya familia yangu na marafiki si sawa. Hata hivyo ni ngumu kujidhibiti.”
Iwe iwavyo juu ya kilichotokea, haikuchukuliwa poa na Neymar. Sifa yake tayari ilikuwa imechukua vibao vichache. Alikosa mechi ambayo Santos walipigwa na Corinthians katika nusu-fainali ya michuano ya jimbo la São Paulo mwezi Machi kutokana na jeraha.
Ilitolewa picha akiwa Uwanja wa Sambadrome mjini Rio siku chache mapema. Alidhihakiwa sana kwa jaribio lake la lisiloonesha udhati wa kupasha viungo wakati wa mchezo na kisha kuketi tena sekunde chache baadaye. Mtazamo wake miongoni mwa wafuasi ulizidi kuzorota bab yaake aliposema amerejea Santos kwa ajili ya kujiuguza apone, na kwamba kucheza kwake ilikuwa bonsai tu kwa timu.
Walter Casagrande, mchezaji wa zamani ambaye sasa ni mchambuzi, aliwatuhumu Neymar na baba yake kwa kuigeuza taasisi inayoheshimika kama Santos kuwa ‘klabu ya soka la ufukweni’
Hata hivyo, Felipe Noronha, shabiki wa Santos na mchambuzi wa soka alionekana kutojifungamanisha na upande wowote kwa maoni kuhusu ujio wa Neymar kwa mara ya pili huko Santos.
“Mafanikio yametokea nje ya uwanja, kwa kuongezeka mauzo ya jezi na kuongezeka kwa watu wanaofuatilia klabu na mchezaji huyo kwenye mitandao ya jamii., na pia ujio wa wadhamini wakubwa,” anasema Noronha.
“Akiwa uwanjani, hajazaa matunda kama Santos walivyoota. Hakika, kuamini katika kupata mataji kwa haraka hivi ilikuwa ni jambo kubwa, lakini ushindi zaidi na soka bora zaidi vilitarajiwa. Mtu anaporejea Brazil, akipata pesa nyingi, tunatarajia soka bora.”


Comments
Loading…