Inawezekana kabisa alichelewa kuja kwenye timu ya Arsenal na kwenye ligi kuu ya England. Kuna uwezekano mkubwa huyu angekuwa mfungaji hatari kuwahi kutokea kwenye ligi kuu ya England.
Lakini kwa bahati mbaya kachelewa mno!, kaja na umri wa miaka 29. Umri ambao kwa mchezaji hufikiria mafao kuliko kucheza kwa kiwango cha juu.
Hana muda mwingi wa kucheza tena kwa ushindani kama ambavyo aliwahi kuwa akiwa na jezi ya Borrusia Dortmund.
Sehemu ambayo alikuwa anacheza huku moyo wake na mawazo yake yote yakiwa Realmadrid. Hii ndiyo klabu ya moyo wake.
Hii ndiyo sehemu ambayo alikuwa anaitamani sana tangu akiwa mtoto. Kuna wakati kwenye maisha siyo kila unachokitamani lazima ukipate.
Aubameyang ana nafasi kubwa sana ya kukosa nafasi ya kwenda kucheza Real madrid. Nafasi ambayo amekuwa akiiota tangu akiwa mtoto.
Leo hii tunamshuhudia akiwa kwenye ligi pendwa, ligi inayofuatiliwa sana. Ligi ambayo asilimia kubwa ya watu huwekeza muda wao mwingi.
Na kizuri zaidi Yuko na jezi ambayo iliwahi kuvaliwa na gwiji wa mpira, gwiji wa ligi kuu ya England na gwiji wa Arsenal.
Dunia ya mpira inampa heshima kubwa sana Thierry Henry kwa sababu tu aliutumikia ipasavyo mpira wa miguu.
Kitu ambacho kilifanya abaki ndani ya mioyo ya watu wengi. Kitu ambacho siyo rahisi. Ni kitu ambacho kinahitaji kazi ya ziada. Kazi ambayo Thierry Henry aliitimiza.
Leo hii Pierre Emirick Aubameyang yupo kwenye jezi yenye namba ambayo inaheshimika pale Arsenal. Jezi ambayo huzungumza neno moja tu nalo ni magoli.
Kwa Arsenal kuvaa jezi namba 14 kuna maana ya kuwa miguu yako inauwezo mkubwa wa kusukuma mipira ndani ya nyavu.
Miguu yenye Sanaa ya kufunga ndiyo huvaa jezi namba 14 kwa upande wa Arsenal. Ndiyo maana Arsenal haikujiuliza mara mbili kumpa Pierre Emirick Aubameyang.
Ni ukweli uliowazi kuwa Mwafrika huyu alizaliwa kwa ajili ya kufunga, pamoja na kwamba alikuja Arsenal mwezi wa kwanza lakini alifanikiwa kufunga magoli 10+.
Hii ikawa ishara yake ya kwanza kuonesha ni kipi kilichomleta Arsenal. Amekuja kwa ajili ya kufunga tu.
Ndiyo maana anafanya hivo. Lakini anafanya hivo vizuri zaidi akiwa katika mazingira yapi?.
Nilikuwa natazama mechi kati ya Liverpool na Arsenal. Aubameyang alikuwa amekabwa sana. Alifanikiwa kugusa mpira Mara 13 tu.
Hii ni kwa sababu moja tu. Liverpool hawakutoa nafasi kwa Arsenal kutengeneza uwazi kwa ajili ya Aubameyang.
Unadhani kwanini hakukuwepo na uwazi wa kumnufaisha Aubameyang?. Jibu ni moja tu , hakuwepo Alexander Laccazate.
Huyu ndiye mchezaji muhimu sana katika mfumo wa Unai Emery. Ndiye mchezaji ambaye huwa anatengeneza uwazi ambao humsaidia Aubameyang.
Hutengeneza vipi huo uwazi?. Alexander Laccazate muda mwingi hushuka chini kuchukua mpira.
Anaposhuka chini katikati kuchukua mpira, huwa anashuka na beki mmoja wa katikati wa timu pinzani. Anaposhuka na huyo beki wa kati husababisha uwazi eneo la nyuma.
Uwazi ambao huwa unatumiwa vizuri na Pierre Emirick Aubameyang. Kwenye mechi dhidi ya Liverpool , Aubameyang hakufanikiwa kupata uwazi eneo la nyuma.
Ndiyo maana aligusa mpira Mara 13 na alionekana kama amebanwa na mabeki wa Liverpool, lakini beki wa kwanza Aubameyang katika ile mechi alikuwa Unai Emery kwa kutomchezesha na mchezaji ambaye angeweza kusababisha uwazi (spaces) eneo la nyuma ya mpinzani.