PAMBANO kati ya Simba na Al Masry kwenye Kombe la Shirikisho ndilo limekuwa gumzo zaidi kati ya mengine yanayotarajiwa kufanyika katika hatua ya robo fainali. Kwenye Ligi ya Mabingwa pambano maarufu zaidi ni kati ya Esperance na Mamelodi Sundowns. Katika mchezo wa kwanza Simba walibugizwa mabao 2-0, huku Mamelodi Sundowns wakiongzoa kwa 1-0.
Nimefuatilia hali ya mapambano mengine lakini hili ni wazi Wamisri wanalifikiria zaidi. Katika moja ya majadiliano kwenye tovuti mbalimbali baadhi ya wachambuzi wanasema uwanja wa Benjamin Mkapa ni machinjioni, huku mashbiki wa Al Masry wakiomba sapoti kutoka kwa mashabiki wa Yanga. Baada ya kuangalia majadiliano hayo ndipo nimehitamisha kwa mambo yafuatayo.
Wimbi la mashabiki toka Port Said
Al Masry ni klabu yenye makao yao kwenye mji wa Port Said nchini Misri. Kumekuwa na gumzo kubwa na hamasa baina ya mashabiki kusafiri kuja Tanzania kuishangilia timu yao. kwahiyo uongozi wa Simba na mashabiki wanatakiwa kuelewa hili pambano bado ni la moto sana na kuna kila sababu ya wao kujipanga vilivyo ndani na nje ya uwanja.
Kuja kwa mashabiki wengi wa Al Masry maana yake kutawahamasisha wachezaji wao na kuhakikisha wanasonga mbele. Hata hivyo Simba watakuwa nyumbani hivyo wana kila sababu ya kuzima ndoto za Al Masry kwenye mchezo huo. Mashabiki wa Simba wanatakiwa kuliamsha dude tangu dakika ya kwanza hadi ya mwisho ya mchezo bila kujali hali inayoendelea ndani ya uwanja. Lile shangwe au Vibes linapaswa kuwa la kutisha na kuzima kelele za mashabiki wageni watakaokuja hapa toka Port Said.
Mabao ya mapema
Al Masry wanafahamu kuwa Simba watakuwa wanatafuta mabao ya mapema sana. ama mabao ya haraka ambayo yatatumika kuwachanganya. Hata hivyo kadiri wanavyocheza wanaonekana kutokuwa na jambo la kutisha lakini eneo pekee ambalo watakuja kujipanga zaidi ni ulinzi. Bila shaka yoyote Simba watakuwa na kibarua kimoja tu kuhakikisha wanaipangua safu ya ulinzi ya Al Masry. Walinzi wa Al Masry sio wazuri katika kupandisha mashambulizi na huwa hawaondoki yadi 30 kutoka eneo la 18 langoni mwoa.
Kwahiyo mara nyingi walinzi wanne hadi watano wanakuwa kwenye eneo hilo wakichunga hatari zozote za pembeni, katikati au mashambulizi ya kushtukiza. Al Masry watakuwa wamejizatiti kuzuia kuanzia mwanzo hadi mwisho. Mchezo wao utakuwa na maana ya kujihami na kushambulia kwa kushtukiza.
Wanaelewa Simba wana uchu wa kupata mabao matatu ya haraka ili wamalize hesabu zao, lakini ukweli wa mambo ni mmoja tu; Simba wahakikishe wanakazana kujilinda na kushambulia kwa uwiano. Katika mchezo wa kwanza walifungwa kwa makosa madogo ya uwiano kati ya kushambulia na kujilinda, ndiyo maana walitoa mwanya kwa viungo wa Al Masry kusogea kwenye 18 za Simba.
Kiwango bora dimbani
Wachezaji wa Simba na benchi lote wanatakiwa kuwa na maamuzi ya haraka na kuwa katika kiwnago bora. Jambo hili pekee ndilo litakalowasaidia kuibuka na ushindi, huku wakiombea makosa yawe mengi kwa Al Masry. Kuanzia golini, mabeki wa kati na mabeki wa pembeni, kisha viungo wakabaji na mawinga hadi viungo washambuliaji na washambuliaji. Maeneo hayo yote yanapaswa kuwa kwenye kiwango bora ili waweze kuibuka na ushindi kwani mabao matatu si magumu kwa Simba ikiwa wameshawahi kuzichapa timu mbalimbali za Kimataifa.
Uchoyo na ubinafsi
Kinachoiua klabu yetu ya Simba kwenye kikosi hiki ni tabia ya uchoyo wakati inaposaka mabao katika eneo la ushambuliaji. Benchi la ufundi linapaswa kuwaonya wachezaji wake wa mbele kuwa robo fainali hii sio suala la kujionesha mchezaji mmoja anajua sana kuliko wengine bali kucheza kwa ajili ya timu. Uchezaji uwe wa muunganiko kila upande katika kusaka mabao sio kuonesha uchoyo.
Inaruhusiwa kuwa na uwezo binafsi lakini usizidi ushirikiano wa timu nzima. Kwa kawaida timu inawahitaji wachezaji ambao wanapangua safu ngumu za ulinzi ama mchango wao binafsi kuwa wa kipekee na kuipa ushindi. Lakini mchezaji wa Simba anapokabiliana na mabeki watatu hadi wanne kisha akataka kuwapngua huku wenzake wamefungua nafasi wakisubiri pasi, huo ni uchoyo na uchezaji binafsi ambao hausaidii Simba.
Umakini safu ya ulinzi
Benchi la ufundi linapaswa kuimarisha safu ya ulinzi kwa kuhakikisha wanakuwa makini na kuondokana na makosa mbalimbali. Makosa binafsi ya wachezaji au makosa ya kitimu lazima yakemewe kwa nguvu ili kuiwezesha Simba kuvuka hatua hii na kutinga robo fainali. Kwa maana hiyo mchezo huu utaamuliwa na maeneo mawili; umakini katika ulinzi na ubora katika ujshambuliaji. Washambuliaji watakuwa na kazi ya kupachika mabao ya kutosha, kisha walinzi watakuwa kazi ya kulind aushindi wa timu. Hapo ndipo mahali ambapo panaweza kuivusha Simba kuelekea Nusu fainali. Inawezekana Simba, inawezekana kwa Tanzania kutwaa kombe la Shirikisho.