Tarumbeta za “Vuvuzela” zinapulizwa na mashabiki wanashangilia kila kona ya Afrika Kusini kwenye mkesha wa kuamkia siku ya leo ya Kombe la Dunia, ambalo Waafrika wanatarajia kulitumia kubadili mitazamo hasi ya dunia dhidi yao.
Kwenye mahoteli na viwanja vya mazoezi vya taifa hili zuri, wachezaji na makocha wa timu zote 32 zinazochuana katika fainali hizi, wote wana lengo moja la mafanikio — kubeba kombe lenye thamani zaidi katika soka Julai 11.
Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amewataka isivyotarajiwa vijana wake wa “Bafana Bafana” (jina linalomaanisha wavulana) kubeba kombe hilo. Lakini mafanikio wanayotarajiwa kuyapata wenyeji ni heshima, utalii, uwekezaji na mshikamano mkubwa wa jumuiya.
Afrika Kusini wataingia katika mechi ya leo ya ufunguzi wa michuano dhidi ya Mexico wakiwa na hali ya kujiamini iliyotokana na kucheza mechi 12 zilizopita bila ya kufungwa.
Asilimia kubwa ya mashabiki 90,000 watakaofurika kwenye Uwanja wa Soccer City leo, watakuwa wakiisapoti Bafana Bafana kwa kelele za vuvuzela ambazo tayari zimekuwa ni nembo ya Afrika Kusini 2010.
“Hii ni historia kubwa, nashindwa kuamini,” shabiki wa ‘Sauzi’, Alice Satege alisema, huku akifuta machozi wakati akishangilia msafara wa timu ya Bafana Bafana mitaani juzi.
Mashabiki wa Mexico walikuwa wakifurahi na kuimba chini ya sanamu kubwa la Nelson Mandela katika mji uliotawaliwa na jua wa Johannesburg jana wakisema kuwa hawana mpango wa kuvuruga sherehe za wenyeji. “Tunataka kufanya sherehe yetu, sio kuvuruga ya wenyeji,” alisema shabiki mmoja. Mashabiki wengine walikuwa wakiimba kwa lugha tofauti mbele ya jengo la Nelson Mandela Square.
Uruguay wataikaribisha Ufaransa katika mechi ya pili kati ya mechi 64 za michuano hii katika siku ya ufunguzi leo. Miongoni mwa wageni wanaomiminika, hakuna waliofunga safari ndefu kuliko wanafamilia ya Uruguay ambao wamesafiri kwa umbali wa km 100,000 wakipita nchi 41 kwa kutumia gari yao ndogo katika safari waliyoianza tangu mwaka 2007 kabla ya kuwasili kwenye fainali za Kombe la Dunia hapa Afrika Kusini kwa kupanda meli.
Comments
Loading…