Moja ya maswali ambayo hadi sasa hayajapata majibu ni kulikoni katika soka ya kulipwa nchini England, hasa hasa Ligi Kuu ya England (EPL) kuna wachezaji wachache sana Waingereza wenye asili ya Asia.
Yaani unaweza kuhesabau kabisa idadi ya wachezaji wenye asli ya bara hilo, na hao ni jumla yao tangu kuanza kwa EPL – mashindano makubwa zaidi ya soka ndani ya England, ikiwa pia ndiyo ligi maarufu zaidi duniani.
Hali ikiwa hivyo huku juu kwenye klabu 20, ambapo tayari Norwich wamethibitishwa kushuka daraja kwa msimu ujao, hali haina tofauti sana huko kwenye madaraja ya chini. Katika kitabu chake kipya, Dk Daniel Kilvington – ‘Race, Ethnicity and Racism in Sports Coaching’, anazungumzia mengi na makubwa juu ya jinsi soka inavyotakiwa kwenda mbali kukabiliana na mpaka wake wa mwisho.
Dk Kilvington ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi na Mkurugenzi wa Kozi za Vyombo vya Habari, Utamaduni na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Leeds Beckett, akibobea kwenye kutafiti na kufundisha masuala ya utaifa, na ubaguzi kwenye muktadha wa michezo na vyombo vya Habari.
Mtaalamu huyu anazungumzia suala la Mwingereza mwenye asilia ya Asia aliyetumia jina lake halisi wakati akiomba kazi kwenye masuala ya soka, lakini hakuitwa hata kwenye usaili, na si mara moja. Baada yah apo akaamua kutumia jina lake la utani na tata, akionekana kama Mwingereza kwa asili, akavuka katika mchujo wa usaili kwa ajili ya kupata kazi kwenye nafasi mbalimbali.
“Mtu huyu kwa sasa ni ofisa wa ngazi ya juu na anaheshimika sana kwenye mchezo,” anasema Dk Kilvington, akihoji kwamba iwapo imeshagundulika hilo kwa huyo mmoja tu, kwa sababu za asili ya mtu kuwa Asio, ni wangapi wengine waliotendwa huko kusikojulikana.
Anahoji maswali mengi, akisema kwamba katika bodi za wakurugenzi na menejimenti hakuna ushirikishwaji mpana wa watu wenye damu mchanganyiko, bali wengi ni wale Waingereza kwa asili. Anasema tatizo hilo linaachwa tu au halitazamwi wala kujadiliwa kabisa wakati ni ubaguzi.
Anasema kwamba mada ya kukosekana kwa wanasoka Waingereza wenye asili ya Asia ni kubwa lakini wengi hawajali. Ukiachilia mbali Neil Taylor wa Aston Villa au Hamza Choudhury wa Leicester, unaweza kabisa kuwahesabu waliopata kucheza tangu kuanza kwa historia ya EPL na ndivyo ilivyo kwenye ligi za chini na vyama na bodi za soka.
Wakati robo ya wachezaji 3,700 wa ligi za kulipwa England ni weusi, Waingereza wenye asili ya Asia ni asilimia 0.25. miaka 40 iliyopita majibu kwa swali la idadi hiyo ndogo yalikuwa ni kwamba Watoto wenye asili ya Kiasia wanapenda zaidi kriketi na hockey. Majibu kama haya kwa sasa hayakubaliki tena.
Utafiti uliofanywa na chou kikuu kilichoko Manchester ulionesha kwamba 60% ya wavulana Waingereza wenye asili ya Bangladesh wamekuwa wakicheza soka mara kwa mara, pamoja na 43% ya Waingereza wenye asili ya Pakistan na kadhalika 36% ya Waingereza wenye asili ya India na 47% ya wavulana Wazungu.
Wapo wengine wanaoweza kudai kwamba watu wa jamii za Kiasia hawajapata kutaka kuungana na wengine kwenye soka. Hiyo nayo si kweli. Wasomi wamemaizi kwamba Waingereza wengi wenye asili ya Asia walijaribu sana kujiunga na klabu za Wazungu katika miaka ya 1960 na 1970 lakini wakakabiliwa na sera za kufukuzwa. Baadhi walitukanwa au hata kupigwa. Sasa kutakuwa na ajabu gani ikiwa wataamua kukaa kando au kuanzisha klabu zao na ligi zao wenyewe? Hakuna ajabu, wametengwa, wamebaguliwa.
Aina nyingine ya ubaguzi, kwa mujibu wa Dk Kilvington, ni kwamba kuundwa kwa chombo cha Waingereza wenye asili ya Asia kunapokewa kwa mshangao na vyombo vingine vya soka. Hili linasababisha watu kukuna vichwa, ikizingatiwa kwamba mchezo huu unapendwa na wote na katika ngazi zote, urefu, unene na rangi – awe Peter Crouch au Adebayo Akinfenwa hadi kwa Ryan Fraser.
Kocha mmoja Mzungu kwenye klabu ya soka ya kulipwa alipata kumwambia mhadhiri huyu kipindi fulani kwamba hawapendi kugusana, na kwamba hilo inaonekana ndilo tatizo lao, akihoji kwamba kulikoni wamekuwa wazuri kwenye kriketi. Kwa hiyo anachotaka kushawishi ni kwamba ikiwa mchezaji ni mzuri lazima ataingia kwenye klabu na kusakata soka na wengine bila kujali rangi ya ngozi yake.
Hiyo inaweza kuwa sawa, lakini lazima uwe na viwango vya juu sana kama akina Lionel Messi au Raheem Sterling – almasi inayong’aa tangu kwenye umri mdogo. Lakini ukweli ni kwamba wachezaji wengi wa kulipwa wamekuwa wakihitaji msaada kuweza ‘kutoboa’; iwe kupata usaidizi kutoka kwa kocha wa Chama cha Soka (FA), mtonyo kufanywa kwa klabu ya ligi au kocha kumpa mchezaji wa aina hii mkataba badala ya yule wa upinzani. Tofauti ndogo ndogo kwa kawaida huwa na athari kubwa.
Jhai Dhillon – beki wa kushoto mwenye kipaji kikubwa kwenye Akademia ya Chelsea na Stevenage anajua hili fika. Huyu alimaizi kwamba angeweza kupata nafasi tu ikiwa ni bahati yake na ikiwa balaa ingemwepuka.
Kwa maoni yake, wachezaji wenye asili ya Asia bado wanachukuliwa na klabu nyingi kwamba kuwasajili ni kama kucheza patapotea au kucheza kamari – na ili kubadili hilo na mawazo ya jinsi hiyo, inabidi wapatikane wengi wa Asia wa kupigiwa mfano, lakini nani anaanza?
“Hali ilikuwa hivi hivi kwa wachezaji weusi miaka ile ya ’70 kabla ya Viv Anderson kuanza kwa England. Hiyo ilibadili mawazo ya watu ambayo yalikuwa hasi dhidi ya weusi,” anasema Dhilon ambaye kwa sasa ni mchezaji wa kulipwa-usu kule Hitchin, akiwa ameanzisha biashara ya kuuza vyakula kwa watu wa sokaa, biashara ikienda kwa jina la ‘Rice n Spice’. Amebaki kwenye soka kwa maana hiyo na si vile alitarajia ingekuwa.
Ni wazi kwamba baadhi ya makocha na maskauti wa wachezaji wamekuwa wakishawishiwa au vinginevyo kutokana na rangi ya ngozi ya mtu. Dhilon anasema hilo ni baya na linaumiza. Wakiona Mweusi kipande cha mtu utasikia wakisema huyu ni beki wa kati au mshambuliaji wa kati.
“Wakiona mchezaji Mzungu anayeonekana kuwa bora kiufundi, basi mara moja wanasema huyo atakuwa kiungo mzuri au namba 10. Lakini wakiniona mimi au Waasia wengine ni kana kwamba wanajiuliza; ‘atacheza wapi?’ mara nyingi Waasia wengi wanachukuliwa kwamba hawapo imara vya kutosha kimwili, ndiyo maana wakati wote nilihakikisha kwamba ninajituma na kuwa mchezaji mwenye kufanya kazi kwa nguvu zaidi kwenye timu,” anasema Dhilon.
Miaka michache iliyopita, FA iliwaomba Sporting Equals – wakfu inayoongoza Uingereza kupigania usawa bila kujali rangi, watengeneze mfuatano wa makubdi na jamii za Kiasia na kupata mapendekezo ya jinsi watakavyoingiza wachezaji wengi zaidi kwenye soka kutoka jamii hizo. Kutokomeza ubaguzi wa rangi ni ajenda muhimu na inatakiwa kuwa ya kwanza.
Baadhi ya watu waliofikiwa kwenye jamii hizo walitoa maoni kwamba wanahisi jamii zenyewe zingeweza kufanya zaidi. Kule Luton, kwa mfano, ilielezwa kwamba baadhi ya wazazi wa Kiasia waliona gemu hiyo kama hobi tu na si kazi na hawakutoa ushirikiano uliotakiwa. Maendeleo yalitatizwa baada ya kuibuka kwa virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu hivyo shughuli nyingi kufungwa na watu kulazimika kubaki majumbani mwao.
Comments
Loading…