Menu
in

KUFUZU AFCON

Taifa Stars

Taifa Stars

Fahamu mambo muhimu baada ya pambano la Tanzania Vs Tunisia

  1. Takwimu mbaya kwa Ndayiragije

Taifa Stars imefungwa mabao matano katika mechi nne walizocheza, huku wenyewe wakifunga mabao manne. Taifa Stars waliwachapa Guinea Ikweta mabao 2-1 yakifungwa na Simon Msuva na Abubakar Salum ‘Sure boy’. Libya waliichapa Taifa Stars mabao 2-1, ambapo la kufutia machozi lilifungwa na nahodha Mbwana Samatta. Mchezo wa kwanza dhidi ya Tunisia, Taifa Stars ilikubali kipigo cha 1-0, kabla ya kutoka sare ya 1-1 jijini Dar es salaam. Takwimu zinamkalia vibaya kocha wa Stars, Ettiene Ndayiragije.  

  1. Tunisia imeweka rekodi ya kipekee Afrika

Kwenye kundi J, Tunisia wamekata tiketi ya kushiriki michuano ya AFCON wakiwa na pointi 10 kileleni. Tunisia ni timu ya kwanza kuweka rekodi ya kufuzu mara 15 kushiriki michuano ya AFCON. Kwamba hii ni mara ya 15 nchi hiyo inafuzu tangu mwaka 1994,1996,1998,2000,2002,2004,2006,2008,2010,2012,2013,2015,2017, 2019, na sasa 2021.

  1. Goli la video 

Dakika ya 34 ya mchezo, kocha wa Taifa Stars Ettiene Ndayiragije alimtoa kiungo mkabaji Mzamiru Yassin na nafasi yake ikachukuliwa na Feisal Salum maarufumkama Fei Toto. Mabadiliko hayo yaliboresha Taifa Stars kumiliki mpira pamoja na kusukuma mashambulizi langoni mwa Tunisia. Matunda ya uamuzi wa benchi la ufundi yalikuja kipindi cha pili ambapo kiungo mshambuliaji Feisal Salum alipachika bao la kusawasisha kwa shuti kali dhidi ya vinara wa kundi J Tunisia

Kwa hakika shuti hilo  lilinirejeshea kumbukumbu za Nuno Gomes wa Ureno wakati wa fainali za Mataifa ya Ulaya mwaka 2004 nchini Ureno. Kwenye kikosi cha Ureno nilipendezwa na mashuti ya Nuno Gomes, Nuno Valente na ufundi wa Deco. 

Feisal Salum hajafiki viwango vya nyota hao lakini bao muhimu ambalo liliwapa Taifa Stars alama moja na kufikisha 4 kundini. Shuti hilo limeonesha namna ambavyo kiungo huyo alivyo hodari. Golikipa wa Yanga, Farouk Shikalo amewahi kuniambia kuwa katika maisha yake ya soka klabuni hapo anavutiwa na uwezo wa kupiga mashuti wa Feisal Salum. Ni wazi Shikalo anafahamu mashuti makali ya Fei Toto mazoezini na bila shaka alifurahia fataki lake dhidi ya Tunisia.

  1. Ubishi wa Taifa Stars utadumu?

Tunisia imezichapa baadhi ya timu katika kundi hilo nyumbani na ugenini ambapo wanaongoza kwa pointi 10 hadi sasa. Lakini kwa Taifa Stars mambo yamekuwa tofauti, mchezo wa kwanza ilinyukwa 1-0 nchini Tunisia lakini mchezo wa marudiano jijini Dar es salaam wametoka 1-1.

Taifa Stars walikosa utulivu katika kipindi cha kwanza cha mchezo, lakini kipindi cha pili walionesha namna gani wanaweza kuwa na matokeo chanya. Kumbuka wachezaji wa Taifa Stars asilimia 90 wanacheza soka Ligi Kuu Tanzania bara. Wachezaji wa kulipwa ni Simon Msuva (Wydad Casablanca ya Ligi Kuu Morocco), Himidi Mao (ENPPI ya Ligi Kuu Misri), wakati Tunisia wanacheza Ligi Kuu barani Ulaya. 

Ukiwatazama Taifa Stars walivyochza na kupambana na miamba ya Afrika kama Tunisia na kupata alama moja inaleta faraja kwamba uwezo wa wachezaji upon a wanakosa imani tu ambayo ingewapa ushindi. 

  1. Azam F.C ‘inahudumia’ Taifa Stars

Idadi ya wachezaji ambao wametoke akademi ya Azam imeongezeka. Wapo wachezaji ambao wamekuzwa na kituo cha soka cha Azam FC ama wamewahi kuichezea klabu hiyo na sasa kikosi kilichotajwa dhidi ya Tunisia kinaonesha wachezaji waliotoka huko. Majina kama vile Simon Msuva, Ditram Nchimbi, Aishi Manula,Himidi Mao, Farid Mussa, John Bocco, Erasto Nyoni,Farid Mussa,Robert Kisu,Abdallah Heri na Iddi Seleman ‘Nado’ ni baadhi ya wanakandanda waliopitia na kucheza Azam. Akademi ya Azam imetajwa na wachambuzi mbalimbali wa soka kuwa inaongoza kwa kuuza wachezaji kwenda timu mbalimbali za Ligi Kuu. 

Tofauti ya Tanzania na Tunisia ni kwamba wamewekeza kwenye soka lao na wanauza nje vipaji vyao ama wengine kuzaliwa nje ya mataifa hayo.  Wachezaji wa Tunisia wengi wamepitia katika akademi halisi kuliko Tanzania. Kwahiyo akademi ya Azam kuibua wanasoka wengi wanaotamba kwa sasa ni ishara ya matunda ya uwekezaji uliofanyika na inahudumia Taifa Stars.

  1. Kasheshe ya taa kuzimika 

Tukio mojawapo lililoripotiwa sehemu mbalimbali duniani ni kuzimika kwa taa kwenye vyumba vya wachezaji wa Tunisia. Jambo hili limekuwa gumzo kwa pane zote mbili yaani Tunisia na Tanzania. kwa upande wa baadhi ya wadau wa michezo wamelalamika kuwa hatua hiyo inaharibu sifa ya Tanzania, huku wengine wakidai huenda zilikuwa ‘mbinu za mchezo. Baadhi wanasema ili kuwa na maendeleo ya kandanda haijatajiki mbinu chafu zozote ikiwemo kuzimwa taa vyumba vya wachezaji. Mpaka sasa hakuna taarifa rasmi iliyoelezwa juu ya sababu ya kuzimika huko, lakini tukio hilo limekuwa gumzo miongoni mwa wanamichezo nchini.

  1. Benchi la Erasto Nyoni lazua gumzo

Kocha wa timu ya taifa anaita wachezaji 18 hadi 21 kwa ajili ya kuanza mchezo. Wapo wanaosubiri kuingia wakitokea benchi. Mchezaji anapoitwa timu ya taifa maana yake ni bora kuliko wengine na anakwenda kupambanishwa na wachezaji wengine bora. Hivyo basi kuitwa kwa Erasto Nyoni timu ya taifa ina maana beki huyo ni bora na anawazidi uwezo wengine.

Wadau wa soka wanajiuliza ni kwanini kocha wa Simba Sven Vandebroeck anamweka benchi beki mkongwe Erasto Nyoni wakati amekuwa mhimili mkubwa katika kikosi cha timu ya Taifa. Kwenye kikosi cha Simba nafasi ya beki wa kati inachezwa na Joash Onyango na Pascal Wawa.

Nyoni anatajwa kuwa beki mwenye utulivu na uimara kikosini, na anatumia akili kubwa zaidi kuliko nguvu. Udhaifu wake pekee ni kwamba hana kasi mchezoni. Faida yake anaweza kucheza beki wa kulia,kushoto,kati, winga wa kulia, kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji. Uzoefu wake umekuwa mtaji tosha kwa kocha wa Taifa Stars.  

  1. Kocha Ndayiragije alivurunda?

Kutolewa kwa mshambuliaji John Bocco na kuingia Adam Adam Omari kumeibua mjadala. Wachambuzi na wadau wa soka wanasema kocha hakutakiwa kumtoa Bocco kwa vile timu ilikuwa inashambulia hivyo alimhitaji mshambuliaji huyo. Lakini baadhi wanapinga kwa kusema John Bocco alistahili kutolewa kwa vile hakuwa hatari langoni kwa Tunisia. Vile Idd Seleman Nado hana madhara kama anayoleta Deus Kaseke kutoka na spidi na kuwapangua ngome ya upinzani. Aidha, wanaeleza kuwa faida ya kutolewa Bocco inamsaidia Adam Adam kupata uzoefu wa michuano ya kimataifa.

  1. Mastaa wa kigeni kuunga mkono Taifa Stars

Wakogomani Serge Tonombe Mukoko na Tuisila Kisinda wa Yanga walivalia jezi ya Taifa Stars yenye majina ya wachezaji wenzao wa klabu hiyo ambao walikuwa kikosini kumenyana dhidi ya Tunisia. Katika jezi walizovaa na kuzua gumzo katika mitandao ya kijamii, Tonombe na Kisinda jezi zao zilikuwa na majina ya Feisal Salu, Abdallah Shaibu,Ditram Nchimbi,Farid Mussa,Metacha Mnata na Bakari Nondo Mwamnyeto.

Wakati huo huo Mwamba wa Lusaka, Cletous Chama alivaa jezi ya Tanzania ikiwa ni njia ya kusapoti na kuwataki kila la heri wachezaji wenzake wa Simba walioko kikosini humo. Simba walikuwa na wachezaji Aishi Manula, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Mohammed Hussein, na John Bocco.

  1. Kipute cha kundi J kutoa mwakilishi wa mchujo

Katika kundi hilo linajumuisha Tanzania,Tunisia,Libya na Guinea ya Ikweta linatarabiriwa kuwa na mwakilishi wa ziada. Taifa Stars itatakiwa kushinda mechi zake zote mbili zilizopo mbele yake. Kwanza kuwafunga Libya kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam kisha kwenda kupata alama moja au tatu ugenini nchini Guinea Ikweta. Pia kuombea Libya wachapwe tena na Tunisia, kisha Guinea Ikweta nae azabwe na Tunisia. Hayo yakitokea basi Taifa Stars itakuwa imevuna pointi 10 ikiwa itashinda michezo yote miwili. Au ikiwa Taifa Stars itashinda mchezo mmoja na kutoka sare mwingine itafikisha pointi 8 hivyo kushika nafasi ya pili. Msimamo wa kundi hili hadi sasa, Tunisia wana pointi 10, Guinea Ikweta wana pointi 6, Tanzania wana pointi 4 na Libya wana pointi 3.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version