MASHINDANO ya mpira wa kikapu ya Kombe la Taifa yatafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 19 hadi 25, kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania, TBF.
Katibu Mkuu wa TBF, Lawrence Cheyo alisema mashindano hayo yatafanyika baada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Tumeona tufanye mashindano haya baada ya mwezi mtukufu wa ramadhani ili tuyafanye kwa uhuru zaidi na wachezaji wakiwa na nguvu,” alisema
Alisema mashindano hayo yatashirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara.
”Mikoa ianze kujiandaa mapema kuanzia nauli ya kuja katika mashindano na ya kurudi, pia kila timu iwe na wachezaji wasiozidi 12, tunatarajia mikoa husika itazisaidia timu fedha kwa ajili ya mashindano.”
”Tunataka mashindano ya mwaka huu yawe na msisimko hivyo timu zijitahidi kufanya mazoezi ya nguvu kuhakikisha zinafanya vizuri,” alisema
Alisema mwisho wa mikoa kuthibitisha ushiriki wao ni Agosti 30 na iwapo timu haitathibitisha ifikapo wakati ule itaondolewa mashindanoni. Bingwa mtetezi wa michuano hiyo ni Mkoa wa Dar es Salaam kwa wanaume na wanawake.
Comments
Loading…