Afrika yasubiri kuchuja timu 10
Mchujo wa kufika Fainali za Kombe la Dunia Brazil 2014 umefika pazuri, baada ya timu 10 za Afrika kuingia hatua ya mwisho ya mtoano.
Nchi zilizovuka hatua ya makundi ni mabingwa wa Afrika, Nigeria, Cameroon, Ivory Coast, Misri, Algeria, Ghana, Senegal, Burkina Faso, Ethiopia na Cape Verde.
Timu hizo 10 sasa zinasubiri kupangiwa zitacheza na nani katika mechi zitakazopigwa mwezi ujao, ambapo nusu yake zitavuka na kwenda Brazil.
Bara la Afrika limepewa nafasi tano katika michuano hiyo, ambapo timu zilizovuka zitacheza mechi mbili mbili tu, nyumbani na ugenini na kupata watakaokwenda Brazil.
Ethiopia na Cape Verde wameshangaza kufika hatua hii muhimu, ikizingatiwa kwamba ni mara ya kwanza kufanya hivyo, ambapo Cape Verde ni mwaka jana tu walifanikiwa kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika.
Cameroon wameponea kwenye tundu la sindano na kuvuka, lakini watatakiwa kugangamala ili kuepuka aibu ya kuachwa tena, kama ilivyowatokea kwenye mashindano mawili makubwa ya Afrika.
Timu hiyo ilikuwa ikiogopewa sio tu barani Afrika bali duniani, ikiwa na wakongwe kama Rober Miller na hata Samuel Eto’o ambaye bado anasakata kandanda na majuzi alisajiliwa na Chelsea.
Tanzania ilishapoteza matumaini ya kusonga mbele, baada ya Ivory Coast kuwaacha mbali, hata kabla ya mechi za wikiendi hii, ambapo walifungwa na timu dhaifu ya Gambia jijini Banjul na pia tayari ilishatolewa kwenye mashindano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani ya nchi.