KOCHA wa Timu ya Taifa ya Uganda – The Cranes, Morley Byekwaso, amekiri kwamba timu yake ilizidiwa na shinikizo kwenye mechi dhidi ya Algeria ambapo walipigwa 3-0 kwenye mechi ya Kundi C la Total Energies CHAN 2024.
The Cranes walizidiwa tangu mwanzo, wakaachia mabao matatu huku wakishindwa kuwamudu wachezai wa Algeria walikuwa wakali kwenye ushambuliaji, na wakiwa wazuri kuwazuia Waganda kujaribu kupata bao.
Kwa Byekwaso, utendaji wat imu yake ulidhihirisha upungufu kisaikolojia lakini pia kiufundi na kimkakati.
“Tulikuja kutoa kila tulicho nacho kizuri, lakini tulishindwa hasa kwenye eneo la ulinzi na hivyo kuilipa kwa hali hiyo ya kuruhusu mabao matatu kabla ya filimbi ya mwisho.
“Timu walikuwa wanataka sana kupata ushindi na walijipanga. Hata hivyo, hatukuweza kubadili aina yetu ya mchezo Kadiri mechi ilivyoendelea na shinikizo lilikuwa moja ya sababu kubwa za kupoteza mechi ile,” akasema.
Mipangilio ya ukabaji wa Uganda ulisambaratika mapema, pale ndiposa Ayoub Ghezala akafunga kwa mpira wa kutengwa. Mabao zaidi kutoka kwa Abderrahmane Meziane na Soufiane Bayazid kuliongeza mzigo kwa The Cranes na hatimaye mkato wa tamaa.
Kwa upande wa pili, Kocha wa Algeria, Madjid Bougherra, amewapongeza vijana wake kwa adhabu waliyowapa Waganda ambao ni wenyeji wenza pamoja na Tanzania na Kenya.
Bougherra akawapongeza vijana wake kwa ufundi waliotumia kwenye mechi na nidhamu kubwa waliyoonesha kwenye mechi yao ya Kundi C jijini Kampala.
Wakicheza mbele ya washangiliaji wengi wa Uganda katika Uwanja wa Taifa wa Nelson Mandela vijana wa Bougherra waliwanyamazisha washabiki Waganda mapema kwa kucheza soka ‘iliyoenda shule kujihakikishia ushindi huo mnono.
“Ulikuwa ushindi mzuri. Matokeo yalithibitisha kwamba tulifanya kazi kubwa kwa weledi. Haikuwa rahisi – tulikuwa tunacheza kwenye ardhi ya kigeni, chini ya shinikizo kubwa – lakini tuliwatawala wapinzani wetu kiufundi na kimbinu,” Bougherra akawambia waandishi wa Habari baada ya mechi.
Algeria walifika fainali kwenye CHAN iliyopita.


Comments
Loading…