KOCHA mkuu wa timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Mart Nooij, amesema kikosi chake kiko tayari kuwavaa Zimbabwe katika mechi yao ya kwanza ya kuwania tiketi za kushirili fainali zijazo za Afrika itakayochezwa Jumapili Mei 18 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Nooij alisema hayo leo Ijumaa mchana na kueleza kwamba wamefanya mazoezi ya kutosha na anaamini wataanza vyema harakati za kusaka tiketi hiyo ya kwenda Morocco mwakani.
Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema timu yake inaundwa na wachezaji wenye uwezo na uzoefu wa kupambana na ushindani dhidi ya wageni hao maarufu kwa jina la Mighty Warriors.
” Tuko tayari kwa mchezo huo utakaofanyika Jumapili, tumefanya mazoezi ya kutosha kulingana na programu niliyoiandaa, nasema tutawakabili tukiwa imara”, alisema Nooij.
Alieleza kwamba mazoezi waliyofanya huko Mbeya na mechi mbili za kirafiki walizocheza zimesaidia kukiimarisha kikosi hicho cha Stars.
Aliongeza kuwa ujio wa wachezaji wengine wa timu hiyo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ni ishara kwamba kikosi chake kitaongeza nguvu.
“Nimewaona kupitia video ila mchango wao wakifika ni mkubwa kwa sababu wanauwezo”, kocha huyo aliongeza.
Nyota hao wawili wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam Jumamosi mchana wakitoea Sudan.
Taifa Stars na Zimbabwe zitarudiana baada ya wiki mbili .
Stars ilicheza fainali za AFCON mara ya mwisho ilikuwa ni 1980
Comments
Loading…