*Ni Pulis wa Stoke, Benitez apigiwa chapuo
*Ukiacha Wenger, aliyekaa zaidi ni miaka 3
Msimu wa 2012/13 umeonekana mchungu kwa makocha, kwani Tony Pulis wa Stoke City ametema kibarua chake, siku chache baada ya msimu kumalizika.
Pulis (55) ameachia ngazi kwa kile kilichoelezwa ni maridhiano yaliyofikiwa kwenye kikao baina yake na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Thomas Coates, na tayari kura zinamwangukia kocha wa muda wa Chelsea anayemaliza muda wake, Rafa Benitez kuchukua nafasi hiyo.
Hatima ya kocha huyo ilikuwa shakani katika mechi kama tano za mwisho wa msimu, kwa vile timu hiyo ilionekana kulegalega na kutishiwa kushuka daraja.
Hata hivyo, ni Pulis aliyeipandisha daraja, na ameiongoza tangu 2002, akaondoka mwisho wa msimu wa 2004/5 baada ya kutoelewana na menejimenti ya awali ya raia wa Iceland na kurejea tena msimu wa 2006/7 na kufanikiwa kuwaacha ligi kuu hadi anaondoka.
Baada ya kujiuzulu kwa Sir Alex Ferguson Manchester United, David Moyes kuondoka Everton kuchukua nafasi yake United, Pulis alikuwa akishika nafasi ya pili kwa kukaa klabu moja kwa muda mrefu baada ya Arsene Wenger aliyekaa miaka 17, lakini sasa nafasi ya pili ni Alan Pardew aliyekaa Newcastle United miaka miwili unusu.
Pulis alishapewa dokezo kwamba huenda ukawa mwisho wake, kwani wadau hawakuwa wakipendezwa na mfumo wake wa uchezeshaji usiobadilika, ukiwa zaidi wa kukabiliana kwa nguvu na timu pinzani, ambapo Wenger alipata kusema hucheza kama rugby.
Stoke wamekuwa na kawaida ya kumaliza ligi katikati ya jedwali la msimamo wake, lakini mwaka huu hali ilielekea kuwa ngumu, na nusura waelekezwe kushuka daraja, kama si kufanya vibaya zaidi kwa timu nyingine.
Msimu huu walikuwa moja ya timu zilizo nje ya nne bora kutumia fedha nyingi kwenye usajili, lakini matunda hayakuonekana. Wachezaji wao maarufu ni pamoja na Peter Crouch, Charlie Adam na Michael Owen aliyetangaza kutundika daluga.
Desemba mosi mwaka jana walikuwa pungufu ya pointi moja kuwa miongoni mwa timu nne bora, lakini baada ya hapo walifanikiwa kupata ushindi kwenye mechi nne tu kati ya 23 za ligi, wakifungwa mechi 11.
Kuondoka kwa Pulis kunaongeza idadi ya makocha walioachia au wanaoondoka kwenye nafasi zao msimu huu kwenye klabu za ligi kuu, ambapo wengine ni Mark Hughes aliyefukuzwa QPR; Roberto Di Matteo wa Chelsea; Brian McDermott kutoka Reading na Nigel Adkins wa Southampton (aliyepewa kazi Reading lakini pia wakashuka daraja).
Roberto Mancini naye alifutwa kazi Manchester City dakika za mwisho wakati Fergie amestaafu United, Moyes amehama Everton kwenda United na Benitez anamaliza muda wake Chelsea, akisubiri pa kwenda, akisema angependa kubaki katika moja ya timu kubwa za England.
Comments
Loading…